Serikali kupitia Wizara ya Nishati na Madini imesema umeme ni huduma ya lazima kwa Watanzania na itafanya kila liwalo kuhakikisha kila Mtanzania anapata umeme. Msimamo wa Serikali umetolewa na Katibu Mkuu wa wizara hiyo, Eliakim Maswi, wakati akizungumza katika kipindi cha Tuambie kupitia runinga ya Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC), wiki iliyopita.

“Serikali yetu inaamini kwamba umeme ni kitu (huduma) cha lazima kwa Watanzania,” amesisitiza Maswi.

 

Katibu Mkuu huyo alikuwa akitoa taarifa ya utekelezaji wa miradi ya umeme ya Wizara ya Nishati na Madini kwa kipindi cha miezi mitatu iliyopita chini ya mpango wa Matokeo Makubwa Sasa (BNR).

 

Amesema wizara inaendelea kutekeleza miradi 29 ya ufuaji, usafirishaji, usambazaji umeme na ujenzi wa bomba la gesi asilia kutoka Mtwara hadi Dar es Salaam.


Amefafanua kwamba kitengo cha ufuaji umeme kimebeba miradi saba, kitengo cha usafirishaji nacho kina miradi saba wakati kitengo cha usambazaji kimebeba miradi 14.


Kwa mujibu wa Maswi, tayari Serikali kupitia Wizara ya Nishati na Madini imeshatiliani saini na wahisani na wakandarasi mbalimbali kwa ajili ya utekelezaji wa miradi husika.


Kuhusu usambazaji wa umeme vijijini, Maswi amesema Wakala wa Umeme Vijijini (REA) imeshapokea fedha kutoka serikalini kwa ajili ya utekelezaji wa miradi kadhaa ya umeme.


“Tayari wakandarasi wako katika mikoa husika kwa ajili ya kuanza utekelezaji wa miradi ya usambazaji umeme vijijini,” amesema.


Katibu Mkuu huyo wa Wizara ya Nishati na Madini amefafanua kuwa kasi ya utekelezaji wa miradi ya umeme inaridhisha na ameahidi kuwa wizara hiyo itatoa taarifa ya utekelezaji zaidi baada ya miezi sita ijayo.


Ametumia nafasi hiyo pia kutoa wito maalumu kwa wananchi kulisaidia Shirika la Usambazaji Umeme Tanzania (TANESCO) kulinda miundombinu ya umeme kwa manufaa ya umma.


Ameongeza kuwa Wizara ya Nishati na Madini itaendelea kushirikiana na Watanzania kukabili changamoto zilizopo ili kuhakikisha huduma ya umeme inawafikia wananchi wengi na kuwa nyenzo muhimu ya maendeleo ya kiuchumi.


Wizara ya Nishati na Madini imekuwa ya kwanza kati ya wizara yote kujitokea hadharani kutoa ufafanuzi juu ya hatua ilizochukua kutekeleza BRN hali iliyopongezwa na wengi.


By Jamhuri