Mwalimu Nelson Bashulula anayefundisha katika Shule ya Sekondari ya kutwa ya Rubale iliyopo Halmashauri ya Wilaya ya Bukoba Vijijini mkoani Kagera, anatuhumiwa kwa kosa la kumtia mimba mwanafunzi wa kidato cha pili shuleni hapo (jina linahifadhiwa).

Kwa mujibu wa chanzo chetu cha habari, mwalimu huyo, ambaye kwa sasa ametoweka na haifahamiki alikokimbilia, amekuwa akijihusisha na vitendo vya mapenzi na binti huyo mwenye umri wa miaka 17 aliyekuwa kidato cha pili.

 

Taarifa zaidi zinasema kwamba kabla ya kugundulika kuwa ni mjazito, binti huyo alitoweka  nyumbani kwao bila kutoa taarifa alikokwenda. Baada ya siku chache alipatikana na ndipo alipogundulika kuwa ni mjamzito, kabla ya kuulizwa na kumtaja mwalimu huyo kuwa ndiye aliyempa ujauzito.

Hata hivyo, haijafahamika iwapo binti huyo alipotoweka alikuwa akiishi na mwalimu huyo au la, kwa sababu hajataja alipokuwa ametorokea, zaidi ya kumtaja Mwalimu Bashulula kuwa ndiye mhusika wa mimba hiyo.

Mkuu wa Shule ya Sekondari ya Rubale, Pontian Ndyanabo,  ameithibitishia JAMHURI kutokea kwa jambo hilo. Amesema kesi hiyo kwa sasa iko mikononi mwa polisi.

“Ni kweli tatizo hili lilitokea, na kulikuwa na kikao pande zote, kwa maana ya mzazi, upande wa uongozi wa shule na yule mwalimu anayetuhumiwa, ila siwezi kuliongelea zaidi kwa sababu liko mikononi mwa Jeshi la Polisi,” amesema Ndyanabo.

Kuna taarifa kwamba Mwalimu Bashulula ameamua kutoweka nyumbani kwake, na haifahamiki mpaka sasa yuko wapi.

“Huyu jamaa ametoweka tangu Jumatatu ya wiki iliyopita na haifahamiki yuko wapi,” kilisema chanzo cha habari. Juhudi za kumpata mzazi wa binti huyo hazikuzaa matunda.


1524 Total Views 1 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!