NA CLEMENT MAGEMBE

Wezi wa fedha kwa njia ya mtandao wamevamia akaunti za barua pepe za mapadre wa Kanisa Katoliki na kuwaibia mamilioni ya fedha zilizotumwa kutoka kwa rafiki zao waishio nje ya nchi.

Wizi huo umefanyika kati ya mwaka 2016 na mwaka jana, huku watekaji wa barua pepe za mapadre wanne wa Kanisa Katoliki zikidukuliwa na kuwaibia kwa nyakati tofauti dola za Marekani 43,000 (Sh 97,600,000) na Euro 545 (Sh 1,450,000).

Padre Paschal Luhengo, Paroko wa Parokia ya Lupiro, Jimbo la Mahenge, Mkoa wa Morogoro kati ya Oktoba na Novemba 2016, akaunti yake ya barua pepe luhengop4@gmail.com ilivamiwa na wezi hao wa mtandao na kuiba fedha kutoka kwa rafiki zake wa Australia na Ujerumani.

Padre Luhengo ameibiwa zaidi ya dola 15,800 za Marekani (sawa na Sh milioni 35.8) na wahalifu hao zilizotumwa kupitia Western Union na kupokewa na wahalifu hao katika benki za Ecco, Tawi la Msimbazi, Equity Benki matawi ya Mbagala na Temeke na United Bank for Africa, Tawi la Maktaba jijini Dar es Salaam.

Oktoba 28, 2016 Padre Luhengo alimwandikia ujumbe kupitia barua pepe rafiki yake wa Ujerumani, Padre Leopold Mlimbo akiomba amtumie Euro 545 kwa ajili ya shughuli zake na siku hiyo hiyo alituma fedha hizo kupitia Western Union.

Alipokwenda kuchukua fedha hizo katika Benki ya Posta, Ifakara, Morogoro ambayo ni wakala wa Western Union akaelezwa kuwa fedha zake zilichukuliwa siku hiyo hiyo muda mfupi baada ya kutumwa na namba ya utambulisho ya mpokeaji ni 0739615019.

Baada ya kuibwa kwa fedha hizo, anasema alipigiwa simu na rafiki yake wa Australia anayefahamika kwa jina la Dk. Winfrid kuwa amepata ujumbe kwenye barua pepe kuwa hali yake kiafya ni mbaya na figo zote mbili hazifanyi kazi, hivyo anahitaji kubadilishiwa figo.

Anasema baada ya kupata ujumbe huo, Dk. Winfrid alituma zaidi ya sh milioni 7 ambazo ziliibwa na matapeli hao walioteka barua pepe yake na kutoa taarifa za uongo kuwa anasumbuliwa na figo.

Pamoja na hayo anasema kutokana na taarifa hiyo na kitendo cha kuibwa kwa fedha alizokuwa ametumiwa na rafiki yake akagundua kuwa akaunti yake ya barua pepe imevamiwa na wezi wa mtandao akaripoti katika kituo cha Polisi Ifakara ambao walimshauri aende Dar es Salaam kufungua shauri.

Desemba 5, 2016 aliripoti katika Kituo Kikuu cha Polisi, Dar es Salaam ambako alishauriwa aende katika Kitengo cha Uchunguzi wa Makosa ya Kifedha (Financial Crimes Unit) kilichopo Kamata.

Alipofika katika kitengo hicho alielekezwa aende katika kituo cha Polisi Msimbazi kufungua jalada ambako alifungua majalada mawili Na. MS/IR/6525/2017 na CC.402/2017.

Yaliyojitokeza baada ya uchunguzi

Uchunguzi uliofanywa na Financial Crime Unit (FCU) unaeleza kuwa tuhuma hizo zilizoripotiwa katika Kituo cha Polisi Msimbazi na Padre Paschal Luhengo zinahusu tuhuma za kughushi na wizi kwa njia ya mtandao.

Kwa mujibu wa taarifa hiyo ya uchunguzi ambayo JAMHURI inazo nakala zake, Padre wa Lupilo Wilaya ya Ulanga aliripoti kughushiwa vitambulisho vyenye, jina lake na kuibiwa kiasi cha Sh 1,117,000 na mtu mwenye nambari ya simu +256702490536 (namba ya Uganda) kupitia Western Union Money Transfer.

Mlalamikaji ameeleza kuwa watu hao walifanya wizi baada ya kuteka anuani yake ya barua pepe Luhengop4@gmail.com na kubadili namba zake za simu kutoka +255784429628 na kuweka namba ya Uganda (ambayo aliihusisha na mtu aitwaye Kalumuna) na kuibadilisha barua pepe yake kutoka Luhengop4@hotmail.com kuwa sgs.africa@yahoo.com.

Alieleza kuwa watuhumiwa walifungua akaunti Na. 01646030005 katika Benki ya BOA tawi la Kariakoo, Dar es Salaam na kufanya jaribio la kujipatia kiasi cha dola 200,000 za Marekani kutoka kwa St STEWART wa Australia walizodai ni za ujenzi wa Parokia ya Lupilo Mahenge.

Taarifa za uhalifu huo zilipokewa na upelelezi ulianza katika Ofisi ya Mkuu wa Upelelezi Wilaya ya Kipolisi Kariakoo kwa kufuatilia nyaraka mbalimbali zikiwamo za akaunti iliyopo Benki ya BOA ambako jaribio hilo lilizuiwa.

Hata hivyo, imebainika kwamba wizi huo ulihusisha matumizi ya mtandao wa kimataifa wa kutuma pesa na teknolojia ya mawasiliano na kitengo hicho kulihamishia suala hilo Makao Makuu ya Upelelezi kwa ajili ya upelelezi wa kina.

“Baada ya jalada hili kuhamishiwa Ofisi hii, hatua za haraka zilichukuliwa ili kuzuia wizi huo hasa ukizingatia kuwa mlalamikaji hakuwa na uwezo tena wa kuingia katika anwani yake ya barua pepe kutokana na kutekwa na wahalifu wa mtandao.

“Kwa kushirikiana na kitengo cha Cyber Crime cha Kamisheni ya Uchunguzi wa Kisayansi (FB) mlalamikaji alifunguliwa anwani nyingine ambayo ilitumika kuwasiliana na Google Inc na marafiki zake kuwajulisha utekaji huo wa anwani na kuwataka wapuuze maombi yoyote ya misaada ya kifedha kupitia anwani hiyo ya barua pepe,” imeeleza taarifa hiyo.

Taarifa hiyo pia imeeleza kuwa ofisi hiyo kwa kushirikiana na Western Union Money Transfer ilikusanya taarifa za miamala yote ya kutuma na kupokea fedha kwa jina la mlalamikaji (Padre Luhengo) na kuifanyia uchunguzi kisha ikabaini wizi uliotokea.

Kumbukumbu za Western Union zilionyesha jumla ya miamala 22 iliyofanyika katika nyakati tofauti kwa jina la Paschal Luhengo na kati ya miamala hiyo 6 ilikuwa ya upokeaji wa pesa kutoka nje ya nchi yenye utata.

Miamala hiyo ilifanyika kati ya Oktoba 17 na Novemba 14, 2016. Miongoni mwa vitu vilivyoleta mashaka ni tofauti ya namba ya kitambulisho cha mpigakura cha mpokeaji, tofauti ya tarehe ya kuzaliwa mpokeaji na mahali pesa zilipopokelewa.

Mlalamikaji alithibitisha kuwepo miamala sita ya kupokea pesa isiyo halali kwa jina lake kutoka kwa rafiki zake walioko nje ya nchi. Inayoonesha Claudia Keim Ehrhardt alituma dola 271.12 zilizolipwa na wakala Benki ya Equity Novemba 14, 2016 kwa mpokeaji mwenye namba ya kitambulisho 1467332894.

Miamala mingine ni dola 3,328.79 za Marekani zilizotumwa na Christoph Doppelreiter na kulipwa kupitia Benki ya Equity Novemba 4, 2016 kwa namba ya utambulisho 5717135242, Padre Leopold Mlimbo aliyetuma Euro 545.29 zilizolipwa Benki ya Equity Oktoba 28, 2016 kwa namba 0739615019.

Christoph Doppelreiter alituma tena dola 2,632.07 za Marekani  zilizolipwa kupitia Benki ya ECCO Oktoba 21, 2016 kwa namba 2315774331, Gabriella Bare alituma dola 5,747.83 za Marekani, zilizolipwa na Benki ya ECCO Oktoba 19,2016 kwa namba 8614699384, pia Bare alituma dola 3,352.89 za Marekani zilizolipwa na UBA Bank Ltd Oktoba 17,2016 kwa namba 1949905024.

Padre Luhengo baada ya kuikomboa barua pepe yake aligundua pia wahalifu hao walifanya miamala mingine mitatu ya kupokea fedha wakitumia jina Paulina Mkama na kuchukua dola 8,100.

Wezi hao wa mtandao kwa kushirikiana na Mila Ladesma wa 384 River Terry, Toms River, New Jerssey, Marekani ambaye alivamia akaunti ya barua pepe ya Padre Luhengo alifanya miamala fedha kutoka Western Union kwenda kwa Paulina Mkama ambako Oktoba 28, 2016 alituma dola 1,500 za Marekani zilizopokelewa kwa wakala Benki ya Posta kwa Namba 3093166177.

Pia Novemba 4, 2016 Ladesma alituma dola 3,300 za Marekani zilizolipwa kupitia Benki ya DTB kwa namba  8539195680 na kiasi kingine cha dola 3,300 za Marekani kilitumwa kupitia Benki ya DTB na kulipwa kwa namba 8197899798 Novemba 11, 2016.

Uchunguzi unaonesha kuwa kutumia taarifa za miamala zikiwemo fomu za kupokelea fedha na nakala za vitambulisho vya wapokeaji kutoka katika benki ambazo ni wakala wa Western Union wote walijitambulisha kwa jina la Paschal Luhengo.

Vitambulisho vya mpiga kura vilivyotumika katika wizi huo vilikuwa na namba tofauti ID No. T-1004-9876-507-2 na T-1004-9876-507-4 huku wahusika wakiwa na umri tofauti.

Tume ya Taifa Uchaguzi katika barua yake ya Machi 27, mwaka jana yenye kumbukumbu namba CEA.182/183/01/157 ilithibitisha kuwa vitambulisho hivyo ni batili kwa kuwa namba zake hazimo katika Kanzidata (data base) ya Tume hiyo.

Watuhumiwa waliokwenda katika benki ya Ecco, Equity na UBA na kupokea fedha kwa njia ya Western Union wanaonekana kwa sura tu katika vitambulisho vya mpiga kura vyenye picha za black & white huku wote wakijiita jina la mlalamikaji huyo.

Taarifa hiyo ya uchunguzi inaeleza kuwa kutokana mwonekano katika picha za watuhumiwa hao upatikanaji wao umekuwa mgumu, lakini mlalamikaji amemtaja mtu anayejulikana kwa jina la Kalumuna kuhusika na uhalifu huo kwa kuwa ametajwa katika kesi nyingine ya mtandao BUG/IR/20/2017 ambayo mlalamikaji ni Padre Charles Limuhela.

Agosti 7, 2017 Kalumuna alijisalimisha Ofisi za Upelelezi za FCU, Kamata na kuhojiwa juu ya tuhuma zinazomkabili lakini alikanusha kuhusika na uhalifu huo. Watuhumiwa wengine wawili waliotajwa kuhusika na wizi wa mtandao kwa Padre Limuhela walihojiwa na kukana madai hayo.

Taarifa hiyo inaeleza kuwa waliohojiwa ni Amood Abdallah, mkazi wa Tabata Segerea na Andrew Kamugisha, mfanyabiashara na mkazi wa Mbezi Mwisho jijini Dar es Salaam. Pia kuhusu mtuhumiwa Paulina Mkama uthibitisho wa kuhusika kwake umekuwa mgumu kutokana kumbukumbu kuwa tofauti na zile zilizopo katika akaunti yake Benki ya NMB na picha katika kitambulisho cha mpiga kura.

Taarifa ya uchunguzi wa Polisi inaonyesha kuwa waliohusika kufungua akaunti kwa nyaraka za kughushi katika Benki ya BOA tawi la Msimbazi, Dar es Salaam kwa kutumia jina la Parokia ya Lupiro, Jimbo la Mahenge kupitia barua pepe ya Padre Luhenge ni Andrew Richard mmiliki wa shule ya Maximilian, Tabata Ferdinand Urassa, Meneja wa Benki ya BOA Tawi la Msimbazi na Fredy Kayombo mtumishi wa benki hiyo.

JAMHURI limekwenda Makao Makuu ya Benki ya BOA, Mtaa wa Kivukoni, jijini Dar es Salaam kuthibitisha taarifa hizo za uchunguzi wa FCU na hatua zilizochukuliwa kwa watumishi wake waliohusika kufungua akaunti hiyo Na. 01646030005 lakini maofisa wa benki hiyo wamegoma kutoa majibu.

Wengine walioibiwa

Padre Charles Limuhela wa Jimbo la Mahenge aliibiwa Sh milioni 7 baada ya wahalifu hao kuteka barua pepe yake na kumwomba rafiki yake anayeishi Uswisi awatumie fedha hizo kupitia akaunti ya Mbega Jengo Abdallah ambaye alitambulishwa kuwa ni Mhasibu wa Benki ya DTB kwa madai kuwa akaunti yake ya NMB Ifakara imefungwa na fedha zikatumwa kama walivyoelekeza.

Abdallah alipokamatwa ilibainika kuwa ni dereva wa Kampuni ya Mafuta. Pia aliwataja wenzake wanne waliovamia barua pepe ya Padri Limuhela na kumwibia kiasi hicho cha fedha ambazo waliahidi kuzirejesha chini ya usimamizi wa polisi.

Padre Limuhela amelieleza JAMHURI kuwa wahalifu hao wa mtandao waliahidi kumlipa, lakini hadi sasa hakuna kilichofanyika na amefatilia FCU na kuelezwa kuwa Abdallah amehukumiwa kutumikia kifungo katika gereza la Mkoa wa Tabora kwa wizi wa mafuta.

Amesema haijulikani ni lini suala hilo litapatiwa ufumbuzi ili arejeshewe fedha zake. Pia DTB walikiri kuwa mtuhumiwa huyo ni mteja wao hivyo Polisi bado wanaendelea na uchunguzi.

Mapadre wengine walioibiwa na genge hilo la wahalifu wa mtandao ni Godfrey Nyangi wa Jimbo la Mahenge, Benjamin Mfaume wa Jimbo la Iringa. Mei 30, mwaka jana Padre Mfaume aliibiwa dola 4,013 za Marekani ambazo alitumiwa na rafiki zake Marianne na Bob Lee Robert kwa ajili ya ada ya masomo yake nchini Uganda kupitia Western Union.

Padre Mfaume amesema genge hilo la wezi wa mtandao linalindwa na vyombo vya dola likiwemo Jeshi la Polisi kwa kuwa limeshindwa kuchukua hatua dhidi ya wahusika licha ya kuwahoji na kuthibitisha jinsi walivyoshiriki katika uhalifu huo.

Katika madai mengine ya mapadre hao wanatishiwa maisha kwa kupigiwa simu na watu ambao bado hawajawafamu, hivyo wanawaomba Waziri wa Mambo ya Ndani, Kangi Lugola na Mkuu wa Jeshi la Polisi IGP, Simon Sirro kuingilia kati suala hilo ili kukomesha vitendo vya uhalifu.

Mhashamu Askofu Agapiti Ndorobo wa Kanisa Katoliki, Jimbo la Mahenge, amelieleza JAMHURI kuwa wanaojiingiza katika vitendo vya utapeli wa aina hiyo ni watu waliojaa tamaa, lakini hawataki kufanya shughuli halali.

“Uovu uko kila mahali duniani, lakini kazi yetu kama watumishi wa Mungu ni kuwasisitiza waumini wetu kuacha uvivu na badala yake wafanye kazi,” amesema Askofu Ndorobo.

JAMHURI limezungumza na Naibu Mkurugenzi Makosa ya Jinai, Charles Kenyela, ambaye alikuwa anashughulikia malalamiko hayo, ambaye hata hivyo amesema yeye si msemaji.

Msemaji wa Jeshi la Polisi nchini, Kamishna Msaidizi wa Polisi (ACP) Barnabas Mwakalukwa alipoulizwa na JAMHURI kuhusu madai hayo ya kutapeliwa fedha mapadre na watuhumiwa kuachiwa katika mazingira ya kutatanisha, amesema mwenye uwezo wa kutoa ufafanuzi ni Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai (DCI).

DCI Robert Boaz hakuweza kupatina ofisini kwake ambako wasaidizi wake walieleza kuwa yuko safarini. 

4058 Total Views 18 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!