Kwa muda mrefu wanachama wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) walikuwa wamekata tamaa na chama chao. Walikuwa na hakika kwamba chama chao kingeangushwa  katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015. Kwa nini!

Kwa sababu Serikali iliendelea kufanya vibaya katika mambo mengi. Na iliendelea kufanya vibaya kwa sababu CCM ilikuwa imeacha siku nyingi kufanya kazi yake ya kusimamia Serikali.

 

Serikali iliachwa kusimamiwa na chama tawala siku nyingi. Ikabaki inafanya inavyotaka kwa kukosa msimamizi.

 

Basi, wakati huu wa kukata tamaa alitokea Abdulrahman Kinana, Katibu Mkuu mpya wa CCM. Akautangazia ulimwengu kwamba utendaji wa Serikali utakuwa unafuatiliwa kwa karibu sana na Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM. Alisisitiza kwamba mawaziri wangehojiwa kuhusu utendaji wao na halmashauri kuu hiyo.

 

Wanachama wa CCM waliposikia kauli hiyo ya Katibu Mkuu wao, walianza kuchangamka. Wakajiaminisha kwamba kwa njia hii ya Serikali kusimamiwa, itaweza kufanya vizuri katika mambo ambayo imeendelea kufanya vibaya. Kinana alikuwa ameleta matumaini mapya kwa wanachama wa CCM waliokuwa wamepoteza matumaini.


Kitendo cha Serikali kusimamiwa na chama tawala si kigeni. Chama Cha Mapinduzi kilikuwa kinafanya vizuri sana kazi hiyo wakati Mwalimu Nyerere alipokuwa Mwenyekiti wa CCM. Mwongozo wa CCM wa mwaka 1981 ulisisitiza sana umuhimu wa CCM kusimamia Serikali yake na kupima matokeo ya utekelezaji unaofanywa na Serikali na vyombo vyake. Wakati ule CCM ilikuwa na utaratibu wa kukutana na kujadili sekta zote za maisha ikiwa ni pamoja na masuala ya siasa, uchumi, elimu, afya, na kadhalika.


Leo kuna kila dalili kwamba CCM ikikutana katika  vikao vyake mbalimbali, inazungumzia zaidi mapambano ya kisiasa kuliko mambo yenye maslahi kwa umma wa Watanzania.

Chukua, kwa mfano, udini uliota mizizi katika Tanzania yetu ya leo kiasi kwamba kila mtu anataka rais wa dini yake mwaka 2015. Kwa upande huo Wakristo wamechachamaa. Sababu wanaona makanisa yanachomwa moto na viongozi wa makanisa wanauawa na hakuna anayekamatwa.


Hata hao mashehe wanaotoa CD za kuchochea vurugu na mauaji ya viongozi wa makanisa hawakamatwi kiasi cha Wakristo kuona kwamba Serikali na mashehe lao moja. CCM inasimamia Serikali yake katika hili?


Halafu wananchi wa Dar es Salaam wanasikitika kuona ongezeko la kila siku la ombaomba na watoto wanaosumbua abiria na wenye magari. Na tuna Idara ya Ustawi wa Jamii ambayo ni sehemu ya Wizara ya Afya.


Hakuna anayewalaumu ombaomba, lakini inalaumiwa Serikali kwa kushindwa kuwasaidia vilema ambao mikono yao inaweza kufanya kazi. Wakusanywe na wapewe nyenzo za kufanyia kazi.


Kwa upande wa watoto wanaowasumbua wenye magari mitaa ya Dar es Salaam, kwa kuingiza mikono yao ndani ya magari hata katika magari ya wageni Serikali inahitaji msaada kutoka nchi za nje kutuondolea aibu hii?


Kama Idara ya Ustawi wa Jamii imeshindwa kuwaondoa barabarani watoto hawa, kwa nini wasitumike polisi na mgambo? Wazazi wao wakitafutwa na kutishwa, watoto wataondoka barabarani.


Halafu kuna suala la Tanzania kuwa nchi ya tatu duniani kwa biashara ya dawa za kulevya zinazoharibu afya na akili za vijana wetu. Huko serikalini wamekiri kuwa wana orodha ya wauzaji wa dawa hizo, lakini wanashindwa kuwachukulia hatua!


Kwa nini kisitumike kikosi cha kuzuia ghasia? Serikali imetufikisha mahali ambapo mabosi wa dawa za kulevya wanatawala nchi kama ilivyo Amerika ya Kusini? CCM itafakari hilo.

 

Na sasa kuna kigogo wa Ikulu aliyeandaa njama za kuchota shilingi bilioni tatu kwa ajili ya safari hewa ya rais. Kumbe safari ya rais inakula hela kiasi hicho? Na kigogo huyu mhujumu uchumi hakufikishwa mahakamani. Ndugu Kinana, fufua matumaini ya wanachama wako kwa vitendo.


930 Total Views 2 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!