Kumekuwa na malalamiko yanayozidi kushika kasi kutoka kwa wadau wa soko la muziki wa Bongo Fleva siku za hivi karibuni, kwamba nyimbo nyingi zinazotungwa na kuimbwa na wasanii wa muziki huo zimekuwa na kasoro za kimaadili, hazina viwango vya kutosha vya ubunifu na kubwa zaidi, zimesheheni lugha ya ‘matusi’.

Hiyo ni mitazamo ya wadau hao ingawa kwa upande mwingine huenda hali halisi si hiyo.

Ni misigano ya kiumri baina ya kundi fulani dhidi ya kundi jingine, vijana wanaukubali muziki huo lakini kwa upande mwingine wazee na watu wa umri wa kati wanakosoa.

Pengine muziki wa Bongo Fleva utazidi kupata mabadiliko kadiri miaka inavyosonga mbele. Ahadi hiyo ipo tangu dunia inaumbwa kwamba vitu vyote vitakua na kuufikia umri, ni sheria ya ulimwengu, hakuna wa kuipinga wala kupingana nayo.

Kwa mantiki hiyo, hawakui binadamu tu, dunia nayo inakua, vitu navyo vinakua, hata ubinadamu wenyewe hukua siku hadi siku.

Ndiyo, watu wengi hatujui kama ubinadamu unakua, tumekariri kwamba anayekua ni binadamu, mti na viumbe hai peke yake kwa maana ya kukua kutoka udogoni, utu uzima na kufa.

Mabadiliko yapo tangu Adamu na Hawa walipoumbwa. Walikuwa na ufahamu lakini ufahamu wao sidhani kama ulilingana na ufahamu tulionao binadamu wa siku hizi. Tukilinganishwa nao, sisi tumeendelea kifikra zaidi kuliko wao, hilo halina ubishi.

Waliumbwa na ufahamu finyu kwa mujibu wa maandiko. Lakini ufahamu wao ulianza kupanuka na kukua mara tu walipoanza majukumu ya kimaisha nje ya bustani ya Eden. Tangu kipindi hicho hadi leo ufahamu huo unakua na unazidi kupanuka.

Kupanuka kwa ufahamu huchochea mabadiliko, hivyo hatuwezi kuyazuia mabadiliko yasitokee kwenye muziki wetu wa Bongo Fleva.

Muziki uliofanywa na kina Sugu na Profesa Jay hauwezi kufanana na muziki unaofanywa na kundi la Weusi ama Ney wa Mitego.

Wasanii wengi kulaumiwa na kuwaona kama hawafanyi chochote ilhali hawalali usiku kucha wakiwaza namna ya kutuburudisha hata kwa nyimbo zao za ‘matusi’ ni kuwavunja moyo nasi kujinyima furaha.

Ni vema tujifunze kuwapa moyo na tuwasaidie kubuni mbinu za kuuboresha muziki wetu. Tuache kung’ang’ania mambo ya wakati uliopita. Kuna vitu havipingiki wala kukwepeka, kimojawapo ni mabadiliko kwenye sanaa ya muziki.

Tuwapongeze, tuwaunge mkono vijana wetu badala ya kubuni mbinu za kuwashusha kila kukicha, wanaofanya vema ni wakati wao wala hayupo wa kulipinga hilo.

Hata hivyo, pamoja na mabadiliko ya kimuziki yanayotokea duniani na kuwalazimisha vijana wetu kubadilika katika utunzi wao, bado kuna vijana wanaonyesha ukomavu na kuwapa wapenzi wao kile wanachokitaka.

Msanii wa nyimbo za kufokafoka, maarufu kama Hip Hop, Kala Jeremiah, katika kibao chake cha ‘Nisamehe’ ameonyesha kwamba bila ‘matusi’ ama maneno tatanishi katika tungo za msanii bado jamii inaweza kumuelewa na kumpokea vema.

Kwa muktadha huo, ni vema walaji wa burudani hii tuelewe nyakati tulizomo na tujifunze kwenda nazo.

491 Total Views 3 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!