Mauaji yanayofanywa si silka ya Watanzania

Watu wachache wasioitakia mema nchi yetu wameanza kuchafua sifa nzuri tuliyojipatia kwa miongo mingi.

Mauaji ya albino, vikongwe na ajuza; na sasa haya ya kuchinja watu ndani ya nyumba za ibada na katika makazi, si ya kuvumiliwa hata kidogo.

Taarifa hizi mbaya zinasambaa duniani kote na kuwaaminisha walimwengu kuwa Tanzania si mahali salama pa kuishi.

Kumekuwapo sintofahamu ya watu wanaojihusisha na mauji haya. Wapo wanaodhani kuwa ni mauaji yanayosababishwa na visasi, wengine wanadai ni ya kiimani; na wapo wanaosema ni njama za maadui wa nani na nje walioamua kuichafua nchi yetu ili tusipate wawekezaji na watalii.

Vyovyote iwavyo, mauaji haya hayana budi yakomeshwe ili kurejesha imani ya wananchi kwa Serikali yao, na pia kuwavutia wageni wenye kiu ya kuja kuwekeza au kutalii nchini mwetu.

Suala la usalama wa jamii na nchi yetu ni la kila Mtanzania mzalendo. Kudhani kuwa mauaji haya yatakomeshwa na vyombo vya dola pekee, ni kujidanganya na kujaribu kukwepa wajibu wetu kama raia katika mapambano haya.

Wauaji mafedhuli tunaishi nao mitaani mwetu. Wanajulikana. Ni wajibu wa kila mzalendo kuvisadia vyombo vya dola kuwanasa wahusika ili waadhibiwe kwa mujibu wa sheria za nchi yetu.

Kamwe wananchi wasikubali kuona nchi yetu ikiwekwa kwenye kundi la mataifa hatari yasiyostahili kuwekeza au kupokea wageni wenye kuja kutalii na hivyo kutuingizia fedha za kigeni.

Wala Watanzania hawana sababu ya kuwalea wauaji hawa wanaoathiri dhana ya Serikali ya Awamu ya Tano ya “Hapa Kazi Tu”. Kila mwananchi anastahili kupata wasaa mzuri wa kufanya kazi za uzalishaji mali akiwa mwenye amani bila hofu yoyote ya kuuawa.

Kwa sababu hiyo, tunachukua fursa hii kuwaasa viongozi wetu kutazama upya suala la kuwa na Mabalozi wa Nyumba Kumi kwa kuondoa utaratibu huo ni wa chama fulani.

Tanzania ya amani tuliyojivunia kwa miongo mingi iliwezekana kwa kuwa na mifumo shirikishi ya ulinzi iliyokuwa imara kuanzia ngazi ya kaya na Nyumba Kumi.

Tunapaswa kuwa na mfumo wa kuwatambua wageni wote wanaoingia katika kaya zetu, hoteli na maeneo yote ndani ya nchi yetu.

Suala hili la kuwa na Mabalozi wa Nyumba Kumi hatudhani kama linahitaji ukinzani kwa sababu faida zake ziko wazi.

Wakati tukiwapa pole wote waliofikwa na athari za mauaji haya, tunasisitiza Watanzania wote wazalendo kuungana katika kuwatambua na kuwafikisha kwenye vyombo vya dola wauajia hao. Mauaji si silka ya Watanzania. Kwa umoja wetu tuungane kuyakomesha.