Nimepata kuandika katika safu hii, kwamba hali ya udini nchini ni mbaya tofauti na wengi wetu tunavyodhani. Bahati nzuri, wananchi wengi wameshaanza kuiona hatari hii, ambayo si tu inatarajiwa, bali pia imeshaingia katika jamii yetu. Huu ni wakati wa kila mmoja wetu kutumia mbinu halali anayoijua, kushiriki mapambano ya kulinusuru Taifa letu kutoka kwenye hatari hii.

Kwa wiki zaidi ya moja sasa nipo bungeni. Nawasikiliza wabunge wanavyochangia. Nawasikia mawaziri wanavyojibu hoja. Suala la udini, kama yalivyo mambo mengine yanayoligawa Taifa letu, linajadiliwa. Nikiri mapema kwamba sijakunwa na mchangiaji yeyote – awe mbunge, au waziri – ambaye ameweza kuzungumza kwa hisia kuhusu jambo hili hatari.

 

Ukiacha majibu mepesi, mbinu ya kujibu hoja za udini, kwa tafakuri yangu, naona nazo zinachochea badala ya kupunguza moto huu.

 

Kwa mfano, mawaziri kadhaa wameweza kutoa mifano ya namna Rais Jakaya Kikwete asivyo mdini. Wakaona hawawezi kueleweka isipokuwa kwa kututajia vyeo na aina ya waumini wanaovishikilia. Tukaambiwa kuna mawaziri kadhaa Wakristo, naibu mawaziri, makatibu wakuu, na kadhalika.

 

Inawezekana nia ya mawaziri hawa ilikuwa ku- “prove wrong” wale wanaosema Rais wetu ni mdini, lakini sidhani kama kulikuwa na umuhimu wa kwenda mbali kiasi hicho. Hii maana yake nini? Maana yake ni kwamba wamesaidia kuwaandaa Watanzania kuuliza swali moja muhimu kila unapofanywa uteuzi – huyo aliyeteuliwa ni dini gani?


Waziri Mkuu wakati akihitimisha hotuba yake, alitumia muda mrefu kwelikweli kumjibu Kiongozi wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni, Freeman Mbowe. Sawa. Zipo hoja kama za “Serikali haijafanya hili au lile” ambazo alipaswa kuzijibu, lakini hapakuwapo sababu ya msingi ya kuimba mwanzo-mwisho na Mbowe, ilhali tuna matatizo makubwa kabisa ya udini, ukabila na ukanda.


Kwa mtazamo wangu, nilitarajia Waziri Mkuu atumie muda mrefu kukemea suala la udini, na pengine kuja na hoja mpya ya kupambana na hali hiyo. Kutaja tu kwamba zimekamatwa CD na watu fulani (kama alivyosema Waziri Stephen Wasira), hakusaidii kuupunguza na hatimaye kuuzima moto wa udini.


Wiki kadhaa zilizopita nilikuwa mjini Geita. Niliumwa na tumbo. Nikaenda zahanati moja iliyo mjini hapo. Wakati wa kuandikiwa cheti, nikaulizwa dini yangu! Nikagoma kutaja. Walipolazimisha, nikawaambia nipo tayari kuwalipa na kuondoka kwa kuwa kadi yao tayari imeshaharibiwa kwa kuandikwa jina langu. Wakawa hawana chenji ya Sh 10,000. Nikaamua kuondoka. Nikawasiliana na daktari wangu, akaniandikia dawa zinazofaa. Nikaenda duka la dawa nikanunua. Nikanywa. Nikapona.


Ninachojaribu kusema hapa ni kwamba Waziri Mkuu alipaswa kukemea viashiria vya udini vya aina hii. Kuna hoja kwamba kuulizwa kwangu dini kunasaidia endapo nikifia hospitali, niweze kuzikwa kwa mujibu wa imani yangu! Kwangu, hoja hii sidhani kama ina msingi. Tusisubiri Taifa letu likomae ndipo twende huko.

 

Mihadhara isiyokuwa na tija inaendeshwa na madhehebu mbalimbali. Haya yalipaswa kukemewa na mawaziri na Waziri Mkuu. Kinyume chake, viongozi hawa wanapokemea, wanakemea kilainilaini tu kana kwamba haya si mambo ya hatari.

 

Kuna ujumbe mfupi wa maneno unaosambazwa na waumini mbalimbali ukihamasisha Wakristo kutowaachia Waislamu fursa ya kutamba kwenye Mabaraza ya Katiba ya Wilaya. Mimi ni miongoni mwa waliotumiwa ujumbe huo mara kadhaa. Nimepanga kumfungulia kesi mmoja wa wasambazaji wa ujumbe huo, ili kuonesha namna ninavyokerwa na ujinga huo.

 

Ndugu zangu, Tanzania imejipatia sifa kemkem kutokana na wananchi wake kuishi kwa upendo kwa miaka mingi. Masuala haya ya kidini ni lazima kila mmoja wetu ashiriki kuyapiga vita.

 

Mara kadhaa nimetofautiana na Mzee Reginald Mengi, lakini alipozungumzia suala la Wakristo kuwaachia Waislamu waendelee kuchinja, amenishawishi niendelee kumwamini katika maono yake ya kutokomeza aina zote za ubaguzi.


Tukitaka kuifanya Tanzania kuwa ni mali ya Watanzania wote, na kama tukiamua kuishi kwa kuvumiliana, hakika hapa patakuwa mahali pazuri pa kila binadamu kuishi. Tuiandae Tanzania njema kwa ajili ya wajukuu, vitukuu na vilembwe vyetu.

Mungu Ibariki Tanzania.


877 Total Views 1 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!