Mahakama ya Wilaya ya Siha mkoani Kilimanjaro, imemhukumu kifungo cha miaka 60 jela mkazi wa Kijiji cha Lawate wilayani humo kwa makosa mawili ya kubaka na kumwingilia kinyume cha maumbile mwanamke (jina tunalihifadhi).

Hukumu hiyo ilitolewa mwishoni mwa wiki na Hakimu Mfawidhi wa mahakama hiyo, Jasmine Athuman, baada ya kuridhishwa na ushahidi uliotolewa na upande wa mashtaka.

Ushahidi huo ni pamoja na taarifa ya daktari aliyemfanyia uchunguzi mwanamke huyo ambaye ana mume.

Mshtakiwa huyo, Peter Kimath (48), mkazi wa Kijiji cha Lawate, anadaiwa kutenda kosa hilo Januari 20, mwaka huu kijijini hapo baada ya kumlazimisha mwanamke huyo kwenda kulala naye nyumbani kwake muda mfupi baada ya kutoka kwenye klabu cha pombe.

 

Mwendesha Mashtaka wa Jamhuri, Simon Feo, aliieleza mahakama kuwa siku ya tukio mshtakiwa alifika klabuni hapo na kuwa na mwanamke huyo.

Alieleza kuwa baada ya kunywa pombe mshtakiwa alimlazimisha wakalale nyumbani kwa mshtakiwa, lakini mwanamke alikataa.

Baada ya kukataa, mshtakiwa alimshika kwa nguvu na kumpeleka hadi nyumbani kwake ambako alimlamizisha kufanya naye mapenzi, lakini alikataa na ndipo alipombaka na kumwingilia kinyume cha maumbile.

Mwanamke huyo alisema tukio hilo lilimuumiza mno, kiasi cha kushindwa hata kumweleza mumewe.

 

Mume wa mwanamke huyo akitoa ushahidi, alisema siku ya tukio mkewe hakulala nyumbani, aliporejea asubuhi alionekana kama anaumwa.

Baada ya kuona hali inazidi kuwa mbaya, aliamua kueleza yaliyomsibu na wakaenda kuripoti polisi.

Hakimu Jasmine alieleza kuwa uchunguzi ulionyesha mlalamikaji alibakwa na kuingiliwa kinyume cha maumbile.

 

Kuhusu utambuzi wa mshtakiwa, alisema hapakuwa na sababu yoyote ya kufanyika kwa utambuzi kutokana na wawili hao kufahamiana kwa muda mrefu na ushahidi huo haukubishaniwa mahakamani.

“Mhanga (mlalamikaji) alieleza jinsi alivyolazimishwa kufanya tendo la ndoa na alipokataa alitishiwa kuuawa kwa kukatwa panga, hivyo ni dhahiri mshtakiwa alitumia nguvu kumbaka,” alisema hakimu.

Kabla ya hukumu, upande wa mashtaka licha ya kusema hauna kumbukumbu za matukio ya nyuma ya mshtakiwa, uliiomba mahakama itoe adhabu kali kwa mshtakiwa kutokana na matukio hayo kukithiri katika jamii.

Katika shtaka la kwanza la kubaka, mahakama ilimhukumu kifungo cha miaka 30 jela; na shtaka la pili la kumwingilia kinyume cha maumbile, mahakama ikamhukumu kifungo cha miaka kama hiyo jela. Adhabu zote zinakwenda pamoja, hivyo mshtakiwa atatumikia kifungo cha miaka 30 jela.

 

Wakati huo huo, Mahakama ya Wilaya ya Siha imemhukumu Mwenyekiti wa Kijiji cha Mitimirefu, Matei Komu, kwenda jela miaka saba au kulipa faini ya Sh milioni mbili baada ya kutiwa hatiani kwa kosa la kujipatia pesa kwa njia ya udanganyifu.

Mwenyekiti huyo alijipatia Sh milioni saba kutoka kwa Bora Masaki kwa kumuuzia miti 100 akidai ni mali ya Kijiji cha Mitimirefu, ilhali akifahamu kuwa miti hiyo ni mali ya Ushirika wa Wakulima wa Lawate.

Shauri hilo la jinai namba 35/2017 lilifunguliwa mahakamani hapo na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) na kuendeshwa na Mwendesha Mashtaka, Suzan Kimaro.

Hukumu hiyo ilitolewa na Hakimu Mfawidhi, Jasmine Athuman.

Mbali na adhabu hiyo ya kifungo cha miaka saba au kulipa faini, Komu ametakiwa pindi atakapomaliza adhabu yake amrejeshee Masaki Sh milioni saba.

Komu alipelekwa katika Gereza Kuu la Mkoa wa Kilimanjaro la Karanga.

By Jamhuri