Wafanyakazi wa Colosseum Hotel wamekamatwa na kuwekwa rumande wakihusishwa na utekwaji wa Mohammed Dewji (Mo) wiki iliyopita.

Miongoni mwao yumo mtaalamu wa mawasiliano ambaye baada ya tukio hilo amekuwa ‘akiwakwepa’ polisi.

Polisi wanatilia shaka hatua ya uongozi wa hoteli hiyo kukaa kimya kwa takriban saa mbili bila kutoa taarifa za kutekwa kwa mfanyabiashara huyo kijana.

Wanaoshikiliwa na Jeshi la Polisi kwa mahojiano ni mfanyakazi wa mapokezi sehemu ya mazoezi, aliyefahamika kwa jina la Prisca; Meneja wa Hoteli hiyo, Abbas na mlinzi mkuu wa hoteli, Swai.

 

Wengine ni Mkurugenzi wa Hoteli ya Colosseum, Shariya; Meneja Mkuu wa Hoteli, Mustapha Daryi na walinzi wanne wa Kampuni ya G1 Security Group waliokuwa zamu siku ya tukio.

Mwingine aliyetiwa mbaroni ni Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano (IT), aliyefahamika kwa jina la Abbas na mkufunzi wa Mohammed anayeitwa Ramadhani.

JAMHURI limeelezwa kuwa Mohammed alikuwa na utaratibu wa kufika hotelini hapo mara tatu kwa siku anapokuwa jijini Dar es Salaam bila kukosa.

“Anapokuja asubuhi huwa anakuja mwenyewe bila dereva, mchana na jioni huwa anakuwa na dereva,” kimesema chanzo chetu.

 

Siku ya tukio Mohammed aliwasili hotelini hapo saa 11 alfajiri na kuegesha gari pembeni mwa gari alilolikuta mbele ya jengo la kufanyia mazoezi. Aliposhuka kabla hajafunga mlango wa gari lake, alivamiwa na watu wawili.

“Watu wawili wakamvutia kwenye gari lao ndipo akaanza kupiga kelele akiwaomba walinzi wasifungue geti.

 

“Wale watu walipoona hivyo wakafyatua risasi na mmoja akaenda kufungua geti wakatoka naye. Lakini hawa watu walikuja na magari mawili, moja liliegeshwa kwenye maegesho yaliyo nje ya hoteli na jingine liliegeshwa ndani, ambalo lilitumika kumteka.

“Mohammed alipovamiwa na watu hao alidondosha funguo za gari, simu na saa, ambavyo viliokotwa na meneja wa usiku (Abbas) aliyekabidhi vitu hivyo Polisi,” kimesema chanzo chetu.

Pamoja na kukamatwa kwa wafanyakazi hao, rafiki wa karibu wa Mohammed anayeelezwa kuwa mteja wa muda mrefu hotelini hapo, Kangaro Sewali, pia amehojiwa.

Sewali anatajwa kuwa mtu wa karibu wa Mohammed na hotelini hapo anaelezwa kama ni ‘nyumbani’ kwake.

 

Kwenye orodha hiyo yumo pia mfanyabiashara, Nillesh Suchack, ambaye amekamatwa kwa ajili ya mahojiano.

Baadhi ya kamera katika hoteli hizo ziliondolewa baada ya kile kinachoelezwa kuwa ni mabadiliko kwenye kitengo cha ulinzi.

 

Mabadiliko hayo yanadaiwa kufanywa punde baada ya kubadilishwa wafanyakazi wa kitengo cha IT. Kamera za mbele ya jengo la mazoezi (gym) na eneo la nje la maegesho ya magari zikiondolewa.

“Nimeshangaa kuona kamera za mbele kwenye jengo la gym na parking (maegesho) za nje zimeondolewa. Hizi kamera ziliwahi kusaidia kulipotokea uhalifu AKN ambao ni jirani. Uongozi ulipobadilisha watu wa IT mambo mengi yakabadilika,” amesema.

Mkuu wa kitengo cha IT wa sasa, Abbas, anatajwa kuwa ni mtu wa karibu wa meneja wa hoteli hiyo.

 

Polisi wamepanua wigo wa uchunguzi wakitaka kujua kama tukio hili ni la kweli au ni ‘sinema’ iliyoandaliwa kwa ustadi mkubwa, hasa kutokana na uamuzi wa kuondolewa kwa kamera katika eneo nyeti kama hilo.

Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Kangi Lugola, anasema Jeshi la Polisi linaendelea na uchunguzi wa kutekwa Mohammed.

“Masuala ya namna hii ni organized crime, upelelezi wake unachukua muda, si wa leo au kesho. Tunaomba tupewe nafasi ili tuweze kumaliza hii kazi na wahusika wote watakamatwa na kuchukuliwa hatua,” amesema Lugola.

Lugola anaamini Mohammed atapatikana mapema kutokana na juhudi zinazofanywa na polisi wanaoshirikiana na vyombo vingine vya ulinzi na usalama.

“Si kwamba ni majini tu tunakolinda, nchi hii inayo mipaka mingi, huko kote tuko makini kuhakikisha mtu huyu anapatikana kama wengine walivyopatikana. Kuna operesheni zinazoendelea,” amesema.

Ametoa mwito kwa wafanyabiashara na wawekezaji kufunga mifumo ya ulinzi (kamera) katika maeneo yao na kujiwekea ulinzi binafsi.

 

Anakiri tukio la kutekwa Mohammed limeishtua serikali, kwani ni la kwanza nchini kumpata mwekezaji na mfanyabiashara mkubwa.

Amesema matukio mengi ya utekaji yanasababishwa na masuala ya kisiasa, kiuchumi, wivu wa kimapenzi, imani za kishirikina na visasi.

Ametoa takwimu akisema mwaka 2016 watu tisa walipotea, lakini watano kati yao walipatika. Mwaka 2017 watu 27 waliripotiwa kupotea, 22 kati yao walipatikana na mwaka huu watu 21 walitekwa, huku 17 kati yao wakipatikana wakiwa hai. Watuhumiwa 10 wamefikishwa mahakamani mwaka huu. Mohammed anadaiwa kutekwa na watu wasiojulikana Oktoba 11.

Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam (RPC), Lazaro Mambosasa, amesema waliomteka ni Wazungu wawili.

 

Mohammed Dewji ni nani?

Mohammed Dewji (Mo) alizaliwa Mei 8, 1975 Kata ya Ipembe, mjini Singida. Ni mtoto wa pili wa mzee Gulam Dewji katika watoto sita wa familia hiyo. Ana dada mmoja, Sabera na wadogo zake; Ali, Hassan, Hussein na Fatema.

Baada ya kufikisha umri wa miaka mitano, alihama na kwenda Arusha kwa ajili ya elimu ya msingi. Alisoma katika Shule ya Msingi Arusha hadi mwaka 1986 alipohitimu.

Mwaka 1987 alihamia Dar es Salaam na alijiunga na Shule ya Kimataifa ya Tanganyika (IST) alikohitimu elimu ya sekondari mwaka 1992. Mwaka 1992 alikwenda nchini Marekani na kujiunga katika Shule ya Saddle Brooke High School. Akiwa hapo ndipo Mo akawa Rais wa wanafunzi wa shule hiyo.

 

Kushika nafasi kama hiyo katika nchi ngeni lilikuwa ni jambo la kujivunia na heshima kubwa kwa familia, pia Watanzania kwa ujumla. Pamoja na kuwa na nafasi ya uongozi akiwa shuleni Marekani, Mo alipigiwa kura ya kuwa kati ya wanafunzi waliofanya vizuri na wenye vipaji (Most Accomplished Student). Upande wa wanawake aliyepigiwa kura mwaka huo alikuwa ni mchezaji maarufu wa tenisi duniani wakati ule, Jeniffer Capriati.

Alipohitimu masomo Saddle Brooke, Mo alijiunga na moja ya vyuo vikuu bora duniani, Georgetown University, jijini Washington D.C, Marekani. Alisomea biashara ya kimataifa na fedha, huku akichukua Theolojia kama somo la ziada.

Akiwa Georgetown, Mohammed alianza kubadilika kimaisha na kubadili mtazamo mzima wa kuangalia mambo ambayo binadamu anayafanya kila siku.

Chuo hicho kinasifika kuwa na elimu bora na kimetoa viongozi na watu waliofanikiwa katika maisha, akiwamo rais wa zamani wa Marekani, Bill Clinton; Mfalme Abdullah wa Jordan; Rais Gloria Arroyo wa Ufilipino na wacheza mpira wa kikapu maarufu nchini Marekani kama Allen Iverson na Patrick Ewing.

 

Alipohitimu mwaka 1998 alirudi nyumbani Tanzania na moja kwa moja akaingia kwenye biashara za baba yake, mzee Gulam na akaanza na nafasi ya Mdhibiti Mkuu wa Fedha katika Kampuni ya Mohammed Enterprises Tanzania Limited (METL).

Jarida la Forbes la Marekani lilimtaja Dewji katika nafasi ya 24 ya matajiri wa Afrika, akiwa na utajiri wa dola bilioni 1.3 za Marekani (Sh trilioni 2.34) unaotokana na biashara kupitia METL Group. Alibadilisha biashara aliyoanzisha baba yake kutoka uuzaji wa bidhaa na kuwa na viwanda.

Alinunua viwanda vya nguo na mafuta vilivyokuwa vinamilikiwa na serikali na kuvifanya viwe na faida zaidi kwa kutumia mtindo wa kisasa wa menejimenti.

METL ina viwanda vya kutengeneza nguo na bidhaa nyingine za matumizi ya binadamu, vikiwamo vyakula, sabuni na vinywaji. Pia ina mapato yanayozidi dola milioni 1.4 za Marekani (Sh trilioni 2.5) kwa mwaka.

Mbali na kuingia kwenye biashara, Mohammed alijiingiza kwenye michezo na kuanza kuifadhili Simba Sports Club ya Dar es Salaam.

 

Huu ukawa mwanzo wa Watanzania kumuona akiingia kwenye ulimwengu wa michezo wa Tanzania na hasa soka.

Mwaka 2000, uchaguzi wa pili wa mfumo wa vyama vingi nchini ulipowadia, akagombea ubunge kupitia CCM katika Jimbo la Singida Mjini.

Katika kura za maoni alimshinda Waziri wa Maji wa wakati huo, Mussa Nkhangaa, kwa kura nyingi lakini Kamati Kuu (CC) ya CCM haikumpitisha kugombea ubunge.

Mohammed alikubali na kuheshimu uamuzi wa chama na kumpigia kampeni mgombea aliyepitishwa na kuhakikisha wanashinda uchaguzi wa mwaka 2000.

Alitekeleza ahadi zake kwa kuwasaidia wananchi wa Singida kwa hali na mali, huku pia akizidi kutoa mikataba minono ya udhamini kwa Simba iliyokuwa zaidi ya Sh milioni 100 kwa mwaka.

Mwaka 2001 Mohammed aliachana na ukapera – akamuoa Saira, ambaye alikuwa rafiki yake tangu wakiwa shuleni, waliyepotezana baada ya Mohammed kwenda masomoni Marekani. Wamejaliwa watoto wawili, Naila na Abbas.

Miaka miwili baada ya ndoa, Mohammed alipanda cheo katika kampuni ya familia na kukabidhiwa rasmi kampuni nzima kama Mkurugenzi Mkuu wa METL.

 

Chini ya uongozi wake kampuni imepanda ngazi nyingi za mafanikio na kukua mara nane ya kiwango alichokikuta kuanzia pale alipoanza kufanya kazi. Amewekeza kwenye sekta mbalimbali za kilimo, fedha, uzalishaji na usambazaji wa bidhaa.

Takwimu zinaonyesha METL inachangia pato la ndani la taifa kwa asilimia mbili na kuajiri watu zaidi ya 20,000 nchini.

Mwaka 2005 Mohammed aliwania ubunge katika Jimbo la Singida Mjini. Aliibuka mshindi katika kura za maoni. Akapitishwa kuwa mgombea.

 

Desemba 29, 2005 aliapishwa kuwa Mbunge wa Singida Mjini.

Ni mwanamichezo aliyeweza kuamsha ari mpya nchini kwa kushirikiana na Rais wa Awamu ya Nne, Jakaya Kikwete na kuwafanya Watanzania kupenda michezo na hasa timu ya taifa ya soka, Taifa Stars. Ili kufanikisha na kuleta maendeleo ya Stars, Kamati Maalumu ya Ushindi iliundwa huku Mo akiteuliwa kuwa mwenyekiti wake.

Katika kipindi chake, Taifa Stars ilishiriki michuano mikubwa barani Afrika ya CHAN iliyofanyika nchini Ivory Coast.

Mwaka 2007 kulikuwa na uchaguzi wa viongozi wa Chama (CCM) na Mo aligombea nafasi ya Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) na akafanikiwa kushinda.

By Jamhuri