Picha ya Waziri MagembeWananchi 3,113 wa Mbarali mkoani Mbeya, waliohamishwa katika vijiji vyao kupisha upanuzi wa Hifadhi ya Taifa ya Ruaha na kupunjwa fidia za maeneo yao, wamesema Serikali imeendelea kuwahadaa kuhusu madai yao.

Mwishoni mwa mwaka jana, Gazeti la JAMHURI liliripoti mgogoro huo ambao umeibua mvutano wa taasisi mbalimbali za Serikali ambazo zimelalamikiwa kuhusika kuwapunja fidia wananchi hao na kiasi kikubwa cha fedha za umma kuwanufaisha watu wachache.

Baada gazeti hili kuandika kwa undani kuhusu mgogoro huo, Wizara ya Maliasili na Utalii, Shirika la Hifadhi za Taifa (TANAPA), Ofisi ya Waziri Mkuu na uongozi wa Mkoa wa Mbeya, kwa pamoja walikubaliana kufanya tathmini nyingine kwa kupima maeneo hayo na kuandaa fidia mpya kwa wananchi hao, lakini licha ya kazi hiyo kumalizika miezi minne sasa, hakuna kinachoendelea.

Wanasema, aliyekuwa Waziri wa Maliasili na Utalii, Lazaro Nyalandu, alipofanya ziara wilayani Mbarali mwaka jana, aliagiza wananchi hao wafanyiwe tathmini upya ya maeneo yao na kulipwa haki zao kulingana na mali walizokuwa nazo, badala ya kuendeleza mgogoro huo.

Mwenyekiti wa kamati ya wahanga hao, Patrick Mnyota, anasema Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Abbas Kandoro, kwa upande wake alimaliza kufanya sehemu yake baada ya kukamilika kwa kazi ya uthamini, na kwamba taarifa yake yote imetumwa Wizara ya Maliasili na Utalii, TANAPA na Ofisi ya Waziri Mkuu.

Mnyota anasema licha ya taarifa hiyo kuwasilishwa kwa mamlaka husika, wameendelea kuzungushwa tena na TANAPA walioagizwa kulipa fidia hizo na wizara, jambo linaloendelea kuchochea mgogoro huo.

Anasema mambo haya ya kuzungushana yameanza mwaka 2007 na baadaye 2008 walipohamishwa katika makazi yao ili kupisha upanuzi wa hifadhi hiyo na kulipwa kati ya Sh 4,000 na Sh 10,000 kwa kila ardhi yenye ukubwa wa ekari moja yenye mazao, majengo na usafiri kwa kilomita moja Sh. 1,000.

Kiasi cha fidia hiyo kimejumuisha gharama za usafiri na posho ya usumbufu wa pango la nyumba kwa miezi 36, kitendo kinachodaiwa na wakazi hao kuwa uongozi wa Mbeya chini ya Kandoro umejinufaisha.

Wanasema Waziri Mkuu aliyemaliza muda wake, Mizengo Pinda, alipofikishiwa malalamiko yao, aliamuru iundwe kamati iliyowashirikisha wakuu wa mikoa ya Mbeya, Njombe na Iringa na kuagiza wananchi hao wakutane na mthamini mkuu wa Serikali.

Machi 12, mwaka jana, Kandoro, akiwa ameambatana na wakuu wa mikoa hiyo, Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, na Mkurugenzi Mkuu wa Hifadhi za Taifa (TANAPA), Allan Kijazi, walikutana na wananchi hao wilayani Mbarali na kusikiliza malalamiko yao.

Baada ya kusikiliza hoja zao, ahadi ilitolewa kwamba fidia hiyo ingefanyika, lakini hadi sasa hakuna ufumbuzi wowote uliopatikana zaidi ya wahusika kutupiana mpira na kuzidi kuwapotezea muda.

Fedha zilizotengwa na TANAPA kwa ajili ya fidia zinazodaiwa kuwanufaisha wajanja wachache walioamua kuwadhulumu wananchi hao waliolipwa fidia ndogo kwa ‘mtutu wa bunduki’, huku wakilazimishwa kuzikagua hundi hizo wakifika katika makazi yao.

Mnyota anasema kwa muda mrefu Kandoro anadai ameandaa ripoti na kuituma Wizara ya Maliasili na Utalii, jambo ambalo halikufanyika kwa wakati, kwani walipofuatilia wizarani walielezwa kuwa haijafikishwa kama mkuu huyo anavyodai.

“Agosti 17, mwaka jana, tuliandika barua kwa Waziri Mkuu na tulipofika ofisini kwake, katibu wake alimpigia simu Kandoro na kuulizia ripoti iliyofanyiwa kazi na wataalamu, akadai kwamba imetumwa wizarani wakati watendaji wa wizara wakikana kuwa hawajaipokea,” anasema Mnyota.

Kutokana na kushindwa kutoa majibu sahihi ya kulipa haki za wananchi hao, Julai 29 na Agosti 3, mwaka jana, Kandoro aliwaeleza kwamba watakuwa na kikao cha pamoja na wataalamu mbalimbali ili kumalizia kazi yao huku akiendelea kuwadanganya kwamba ripoti imeshatumwa Ofisi ya Waziri Mkuu na Wizara ya Maliasili na Utalii.

Hata hivyo, kamati iliyoundwa kwa maagizo ya Waziri Mkuu, iliteua wajumbe Esteria Ndaga, Athuman Mohamed, Mkaguzi wa fedha za ndani kutoka Ofisi ya Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), Mthamini wa Ardhi wa Wilaya ya Mbarali, wataalamu wengine kutoka Wizara ya Maliasili na Utalii, Idara ya Usalama wa Taifa na Takukuru, lakini anasikitika kwamba imeshindwa kukamilisha ufumbuzi wa suala hilo.

Aprili 16 na 17, mwaka jana, aliyekuwa Waziri wa Maliasili na Utalii, Nyalandu, aliagiza kamati hiyo kufanya tathmini upya na kukamilisha kazi ya kuwalipa wananchi hao fidia zao, huku tangazo la Serikali namba 28 likiwa limeagiza wananchi ambao hawakufanyiwa tathmini warudi katika maeneo yao.

Pamoja na agizo hilo la Nyalandu, Mnyota anasema hakuna utekelezaji wowote na kwamba sasa wamejiridhisha kwamba maagizo hayo yaliyotolewa bila utekelezaji ni ulaghai wa waziwazi uliofanywa na watendaji hao wa Serikali.

Anasema Mei 15, mwaka jana, kamati ya wahanga wa uhamisho huo waliopunjwa fidia zao, iliamua kurudi tena kwa Mkuu wa Mkoa wa Mbeya na Ofisa Ardhi wa Mkoa, lakini wakaelezwa na Katibu wake, George Kikosa, kwamba taarifa ya tathmini imepelekwa kwa Waziri Mkuu tangu Mei 5, mwaka jana.

“Ubabaishaji wa Kandoro umeendelea kujitokeza mara kwa mara kwa kuwazungusha wananchi hao huku wakielewa wazi haki zao zimewanufaisha watu wachache wanaodai  Sh bilioni sita zilitumika kulipa fidia hizo,” anasema Mnyota.

Anadai kiasi hicho cha fedha kilitumika kuwalipa wahanga walioambulia kati ya Sh 4,000 na Sh 10,000 kwa kila ardhi yenye ukubwa wa ekari moja yenye mazao, majengo na usafiri kwa kilomita moja Sh. 1,000 na akasema: “Huu ni uhuni mtupu.”

Novemba 7, 2013 Ofisi ya Waziri Mkuu iliwaandikia barua wananchi hao na kuwataka kusubiri wakati ikishughulikia haki zao za madai ya fidia ya ardhi.

“Kamati ya walalamikaji ipeleke maombi yao rasmi kwa Mthamini Mkuu wa Serikali,” inaeleza sehemu ya barua hiyo iliyosainiwa na Buberwa kwa niaba ya Katibu wa Waziri Mkuu, na nakala kupelekwa Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi; Maliasili na Utalii; Katibu Mkuu wa CCM na Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Mbeya.

Walimweleza mthamini huyo kuhakikisha waliopunjwa fidia zao na kulipwa kiasi cha kati ya Sh 4,000 na Sh 10,000 kwamba malipo hayo yangeongezwa na kufikia Sh 600,000 bila kujali ukubwa wa ardhi na majengo kwa kutumia sheria ya mwaka 2015.

Wizara ya Maliasili na Utalii

Kwa upande wake, Waziri wa Maliasili na Utalii, Profesa Jumanne Maghembe, alipoulizwa na JAMHURI kuhusu wahanga hao kutolipwa mapunjo ya fidia zao baada kuondoka kwa hiari yao katika maeneo yao kupisha upanuzi wa hifadhi hiyo, alijibu kwa mkato, “Suala lao linashughukiwa.”

2458 Total Views 2 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!