Serikali imeamua kufuatilia kwa kina wakazi wa Dar es Salaam wanaomiliki viwanja ambavyo kwenye ramani za mipango miji vinaoneshwa kuwa ni maeneo ya wazi.

Maeneo ambayo Serikali inayamulika ni yale yenye hadhi, umaarufu na thamani kubwa yaliyopo Oysterbay, Masaki, Mikocheni, Sinza na sehemu nyingine katika Jiji la Dar es Salaam.

Taarifa kutoka Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi inasema maeneo ya wazi zaidi ya 180 yamevamiwa katika kipindi cha miaka 20 iliyopita.

Kati ya hayo, viwanja 111 ni ndani ya Manispaa ya Kinondoni, wakati Ilala viwanja 50 vimevamiwa; wakati Temeke  ni viwanja 19.

Tayari taarifa hizo zimethibitishwa na Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, William Lukuvi pamoja na Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira, January Makamba, walipozungumza na waandishi wa habari. Kwa idadi hiyo ya viwanja kuvamiwa, Kinondoni inaongoza kwa waliojenga maeneo ya wazi na imebainika wana hati za umiliki.

Ramani ya Jiji la Dar es Salaam ya mwaka 1994 inabainisha maeneo ya wazi, makazi, michezo na viwanda.

Ramani hiyo inaonesha eneo la Masaki, Barabara ya Haile Selassie, katikati ya kiwanja Na. 531 na 504 ni eneo la wazi lililokuwa likitumiwa kwa michezo miaka ya 1990, lakini sasa limejengwa nyumba nne za kifahari na kupewa Na. 1733. Eneo hilo lipo pembeni mwa duka la Marry Brown. 

Kuna nyaraka zinazoonesha kuwa mchoro wa eneo hilo ulichorwa na K. Msago na kusainiwa Juni 4, 1992.

Eneo hilo la wazi limejengwa na mfanyabiashara Mama Ligongo anayetajwa kumiliki nyumba kadhaa jijini Dar es Salaam.

JAMHURI liliwasiliana na Mama Ligongo kuhusu ujenzi katika eneo hilo la wazi, na kumtaka akutane na mwandishi akiwa na nyaraka za umiliki wa eneo hilo.

Hata alipokutana naye kama alivyoahidi, hakuwa na nyaraka.

Badala yake katika mahojiano na JAMHURI, Mama Ligongo anasema mumewe ndiye aliyenunua eneo hilo. Kwa sasa mumewe ni marehemu.

Alipoulizwa tarehe ambayo alilinunuliwa eneo hilo, alijibu: “Sikumbuki, ila nina hati ya umiliki wa eneo hilo ambayo ilitolewa na Wizara ya Ardhi.

“Niko na hati miliki ya eneo hili, kama ni eneo la wazi waulizwe watu wa ardhi, siyo mimi, vitu hivi kuniuliza mimi ni kunionea bure. Na ikumbukwe ya kuwa mume wangu hakuwa mtu wa kwanza kununua eneo hili kwani alinunua kwa mtu- jambo alilolifanya ni kubadili hati miliki.”

Anaongeza: “…Siku hizi hakuna kumuonea mtu, kama watakuja kubomoa watajua maana watanilipa.”

Ofisa Habari wa Manispaa ya Kinondoni, Sebastian Mhohela, anasema kila eneo la wazi lililovamiwa litarudishwa katika hali yake ya awali kama michoro inavyoonesha.

Mhohela anasema kazi ya uvunjaji ilishaanza na ilisimama kwa muda kutokana na Baraza la Ardhi kuvunjwa.

Anasema baada ya kupatikana kwa Baraza jipya, hakuna shaka mchakato utaendelezwa na vikao vya mipango miji na mazingira vinatarajiwa kuanza hivi karibuni.

“Taarifa inaandaliwa kila kata, mtaa kisha inapelekwa Baraza la Madiwani. Mfano mzuri ni Sinza ambako nyumba zimeshawekewa ‘X’ na wananchi wameanza kuvunja wenyewe, ila changamoto kubwa iliyopo ni watu kukimbilia mahakamani kuweka zuio wakati walijenga kinyume cha taratibu,” anasema Mhohela.

Mmoja wa maofisa mipango miji aliyeomba jina lake lihifadhiwe anasema kwa mujibu wa ramani iliyopo, eneo hilo ni la wazi na limejengwa kinyume cha taratibu.

“Kwanza michoro inaonyesha kuwa eneo hilo ni la wazi, pili haiwezekani mchoro wa mwaka 1994 ukaonyesha eneo ni wazi, lakini ukawa na mchoro unaoonyesha kuwa eneo hilo ni makazi miaka miwili nyuma. Pia hata ukitizama namba zake zi tofauti kabisa na hizo zilizopo, wenzake wote ni 500, lakini yeye ni 1000,” anasema.

JAMHURI limezungumza na baadhi ya maofisa wa Wizara ya Ardhi ambao wanasema kuwa eneo hilo liliuzwa na maofisa wenzao, na kwamba halikuwahi kumilikiwa na yeyote.

“Hilo eneo hapo awali lilikuwa sehemu ya watoto ya kuchezea, lilifungwa mabembea, lakini walioliuza tayari walishaondoka Ardhi muda mrefu na waliliuza kwa shilingi milioni tatu tu. Pia hata mnunuzi alijua wazi kuwa eneo hilo ni la wazi, sema pesa ndiyo iliyotembea na kumwandalia mchoro pamoja na hati,” anasema mtoa taarifa.  

Mwezi uliopita, Lukuvi aliongoza ubomoaji uzio eneo la ufukwe wa Coco uliojengwa pembezoni mwa hoteli ya Indian Oceanic.

Lukuvi anasema ujenzi huo haukufuata taratibu na akaagiza Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), kuchunguza waliohusika ili wachukuliwe hatua za kisheria. Waziri huyo wa Ardhi, Nyumba na Makazi amesema serikali kamwe haitishwi na wanaotumia kiburi cha fedha kujenga maeneo yasiyostahili.

2311 Total Views 2 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!