Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi, imelikaribisha Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) kwenye mapambano dhidi ya majambazi na wahalifu wengine.

Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Charles Kitwanga, ameikaribisha JWTZ ili itumie misitu na mapori kwa ajili ya mazoezi yake na wakati huo huo kuwakabili wahalifu waliojificha humo.

Akizungumza na JAMHURI, Kitwanga amesema: “Tumeona JWTZ wanafanya mazoezi yao kila baada ya muda fulani. Ndiyo maana tunaona ni vizuri kama watakuwa kwenye mazoezi, basi wayafanyie katika misitu au mapori ambayo tunadhani yanatumiwa na wahalifu.

“Sisi Polisi uwezo tunao, lakini tunadhani JWTZ kutumia mapori na misitu hiyo kwenye mazoezi yake kutasaidia mambo mawili-moja ni la wao kufanya mazoezi, lakini la pili ni la kusaidia kuwadhibiti wahalifu wanaojificha huko.

“Askari wanapokuwa hawapo vitani kama sasa tunaona ni muhimu watumike kwa njia hiyo kusaidia suala la ulinzi kwa sababu sisi ni Serikali moja. Sijawaomba rasmi, lakini naamini tutaongea, tutaelewana na tutafanya kazi kwa ajili ya Watanzania wote,” amesema Kitwanga.

Anatoa mfano wa maeneo ambayo angependa JWTZ wasaidie kufurusha wahalifu kuwa ni katika misitu mingi iliyopo Bagamoyo na eneo la Ruvu mkoani Pwani.

“Humo ndani hatujui wanaishi nani, lakini kama yumo binadamu anayefanya shughuli isiyo salama, aondolewe. Sijazungumza na Waziri mwenzangu (Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa), lakini nina hakika nikimfikishia jambo hili hata yeye atafurahia maana tutakuwa tunampa premises (maeneo) ya mazoezi,” amesema.

Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Dk. Hussein Mwinyi, hakupatikana kuzungumzia mtazamo na mapendekezo ya Kitwanga, ingawa habari za uhakika ni kwamba Rais John Magufuli, amekuwa akikerwa na wimbi la uhalifu.

Mara kadhaa Rais amenukuliwa akivihimiza vyombo vya ulinzi na usalama kukabiliana na uhalifu ili kuwawezesha Watanzania kutumia muda mrefu katika shughuli za maendeleo badala ya kujihami dhidi ya wahalifu.

Kwa miezi ya karibuni kumeibuka wimbi la majambazi wanaofanya uporaji katika benki na kwa watu wanaosafirisha kiasi kikubwa cha fedha.

Matukio ya aina hiyo yameripotiwa katika benki na mitaa kadhaa ya Dar es Salaam na maeneo jirani na jiji hilo.

Wiki iliyopita, Polisi wa Kanda Maalumu ya Dar es Salaam kwa kushirikiana na wananchi waliwaua watu watatu wanaodhaniwa majambazi baada ya kuvamia benki ya Access iliyopo Mbagala.

Kamanda wa Polisi katika Kanda hiyo, Kamishna, Simon Siro, ameahidi kukabiliana na hatimaye kukomesha vitendo vya ujambazi katika jiji hilo.

Mwaka jana matukio yaliyotawala yalikuwa ya majambazi kuvamia na kuua raia na askari katika vituo vya polisi.

Ushiriki wa JWTZ katika kukabiliana na wahalifu unaweza kuchukuliwa kwa hadhari kubwa kutokana na historia ya utendaji kazi wa chombo hicho.

Mwaka juzi JWTZ waliongoza Operesheni Tokomeza iliyolenga kukomesha ujangili, lakini kukaibuka malalamiko kuwa baadhi ya watuhumiwa waliteswa na hata kupoteza maisha. Hatua hiyo ilimfanya Rais wa wakati huo, Jakaya Kikwete, asimamishe operesheni hiyo ingawa aliahidi awamu ya pili ingerejeshwa.

Operesheni hiyo ilisaidia mno kupunguza vitendo vya ujangili, hasa wa tembo na faru ambao wanatajwa kuwa hatarini kutoweka.

Hivi karibuni majangili walidungua helikopta kwa risasi na kumuua rubani Rodgers Gower (37), raia wa Uingereza. Tukio hilo lilitokea katika Pori la Akiba la Makao, Meatu mkoani Simiyu.

2379 Total Views 2 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!