Wahega walisema kwamba linaweza kutokea usilolitarajia kamwe. Sikutarajia hata siku moja kwamba Mbunge wa kuteuliwa na Rais atajiingiza kwa kishindo katika historia ya Muungano wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kwa kutenda kinachofanana na kuuma mkono unaomlisha, nia yake ikiwa kujiepusha na mgongano wa maslahi.

James Mbatia, Mwenyekiti wa chama cha siasa NCCR-Mageuzi, ambaye ameteuliwa na Rais Jakaya Kikwete kuwa mbunge, alikataa kuteuliwa na Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, kushiriki katika Tume iliyosimikwa kuchunguza viini vya kutofaulu kwa kiasi cha ajabu kwa wanafunzi wa kidato cha nne mwaka jana, na elimu nchini kwa jumla.

Awali ya yote, niseme kwamba mimi ni raia wa Tanzania ambaye si mwanachama wa chama chote chote cha siasa.

 

Ibara ya 26 ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania 1977, kama ilivyorekebishwa (“Katiba ya Muungano”), inamtaka kila mtu kuwa na wajibu wa kufuata na kutii Katiba ya Muungano na Sheria za Jamhuri ya Muungano.


Pia inatamka kwamba kila mtu ana haki, kwa kufuata utaratibu uliowekwa na sheria, kuchukua hatua za kisheria kuhakikisha hifadhi ya Katiba ya Muungano na sheria za nchi.


Miongoni mwa ibara za Katiba hiyo zinazotakiwa kuhifadhiwa ni ibara: 8 (1) (a) na (c) (Serikali na Watu); 63 (2), (3) (a) (b) na (d) (Madaraka ya Bunge); 100 na 101 (Madaraka na Haki za Bunge).

Mbatia alitangaza kwamba kushiriki katika Tume hiyo iliyosimikwa na Serikali, kungegonganisha maslahi kati yake kama Mbunge na utendaji wake katika Serikali ambayo anapaswa kuiwajibisha.


Ibara ya 8 (1) (a) na (c) ya Katiba ya Muungano inatamka kwamba: Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ni nchi inayofuata misingi ya demokrasia na haki ya kijamii, na kwa hiyo, wananchi ndiyo msingi wa mamlaka yote na Serikali itapata madaraka na mamlaka yake yote kutoka kwa wananchi kwa mujibu wa Katiba ya Muungano; na kwamba Serikali itawajibika kwa wananchi.


Ibara ya 63 (2) na (3) nayo inatamka kwamba Bunge litakuwa na madaraka, kwa niaba ya wananchi, kusimamia na kuishauri Serikali ya Jamhuri ya Muungano na vyombo vyake vyote, katika utekelezaji wa majukumu yake kwa mujibu wa Katiba ya Muungano.


Inaongeza kwamba, kwa madhumuni ya utekelezaji wa madaraka yake, Bunge laweza kuuliza waziri yeyote swali lolote kuhusu mambo ya umma katika Jamhuri ya Muungano ambayo yako katika wajibu wake; kujadili utekelezaji wa kila Wizara wakati wa Mkutano wa Bunge wa kila mwaka wa bajeti; kutunga sheria pale ambapo utekelezaji unahitaji kuwapo sheria; n.k.


Ibara za 100 na 101 zinaonesha hekima na busara ya kutokupoteza kinga ya ubunge kinyume na kama Mbatia angejiruhusu kushiriki katika Tume ya Waziri Mkuu.


Ibara ya 100 inaweka bayana kwamba kutakuwa na uhuru wa mawazo, majadiliano na utaratibu katika Bunge, na uhuru huo hautavunjwa wala kuhojiwa na chombo chochote katika Jamhuri ya Muungano, au katika mahakama au mahali pengine nje ya Bunge.


Inaongeza kwamba, bila ya kuathiri Katiba ya Muungano au masharti ya sheria nyingine yoyote inayohusika, mbunge yeyote hatashitakiwa au kufunguliwa shauri la madai mahakamani kutokana na jambo lolote alilolisema au kulifanya ndani ya Bunge au alilolileta Bungeni kwa njia ya maombi, muswada, haja au vinginevyo.

 

Ibara ya 101 inahitimisha kwamba Bunge laweza kutunga sheria kwa ajili ya kuweka masharti ya kuwezesha mahakama na sheria kuhifadhi na kutilia nguvu uhuru wa mawazo, majadiliano na utaratibu wa shughuli katika Bunge ambao kwa mujibu wa ibara ya 100 umedhaminiwa na Katiba ya Muungano.


Onyo ni kwamba mbunge yeyote ambaye nje ya Bunge anashiriki katika Tume hiyo iliyoteuliwa na Serikali kuchunguza matatizo ya elimu nchini, akae chonjo kwamba mawazo, majadiliano, jambo lolote atakalosema au kulifanya nje ya Bunge au aliloleta kwenye Tume hiyo, ombi, hoja yake au vinginevyo hayatakuwa na kinga ya kibunge.

 

Kwa hiyo, wabunge wa namna hiyo wanaweza kushitakiwa au kufunguliwa shauri la madai mahakamani. Wabunge chungeni kinga yenu ya ubunge.

 

Somo jingine ambalo tunapata kwa James Mbatia ni kwamba Katiba Mpya ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania  ikataze wakuu wa mikoa na wilaya, na mawaziri, ambao wote ni watumishi wa Serikali, kuwa wabunge.

 

Ingefaa kila mwananchi akawa na nakala ya Katiba ya Muungano na ya Katiba ya Zanzibar, 1984. Katiba hizo mbili zimeandikwa katika Kiswahili. Zinapatikana katika maduka ya vitabu vya Serikali.


Haya shime, kila chama cha siasa sambazeni nakala za Katiba hizo kwa wananchi. Asiyejua kusoma na kuandika atafsiriwe hadi hapo tume hiyo itakapotoa ufumbuzi.

Novatus Rweyemamu

Wakili Mwandamizi

Simu: 0784 312 623

 

By Jamhuri