Na Thompson Mpanji, Mbeya

BAADHI ya wananchi wa Mtaa wa Gombe, Kata ya Itezi wameelezea kutoridhishwa na uamuzi uliotolewa Januari 15, 2018 katika kesi Na. 204 ya Mwaka 2016 dhidi ya mwekezaji (jina la Kampuni limehifadhiwa) inayohusu mgogoro wa ardhi iliyotolewa na Mahakama ya Ardhi ngazi ya Wilaya, mkoani Mbeya.

Wamemwomba Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Wiliam Lukuvi kuingilia kati mgogoro kwa madai kuwa hawajatendewa haki.

Wananchi hao wamesema wakati wakiendelea kuwa na matumaini na Serikali ya Awamu ya Tano ya Rais, John Magufuli wanaendelea na mchakato  wa kukata rufaa Mahakama ya Kuu kudai haki zao.

Wakizungumza na JAMHURI baadhi ya wawakilishi wa wananchi hao, akiwamo na Nazareth Mwanjisi, wameelezea asili ya mgogoro huo waliodai ulianza Julai, 2016 baada ya mtu aliyejitambulisha kwa jina la mwekezaji kuwaita na kutaka kuwalipa fidia ya mashamba yao, lakini  chakushangaza wakati wakiendelea na mazungumzo figisu zikaanza.

“Wakati tukiendelea na mazungumzo huyo mwekezaji alibadilika na tukakuta ameanza kuweka mawe na tulipomfuata kumuuliza kulikoni alitujibu sisi ni wahuni na kwamba hawezi kutupatia fidia na kwamba eneo hilo analimiliki kisheria kwamba anayo hati miliki,” amesema Christopher Ndolela.

Baadhi ya walalamikaji akiwemo Anastazia Degende na kikongwe Mwinga Mwandawale, wamesema wakati wakiendelea na mvutano  waliamua  kwenda kumuona Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Amos Makalla kufikisha malalamiko yao naye akaunda Tume  ambayo baadaye ilitoa matokeo ya uchunguzi kuwa wanapaswa kulipwa  fidia, lakini haikufanyika hivyo.

Baadaye iliundwa Tume nyingine kutoka Ofisi ya Mkuu wa Wilaya ya Mbeya, William Ntinika na hawakujua ilipoishia. Hatimaye waliitwa mahakamani na kuambiwa kesi iliendeshwe na ilipofika Januari 15, 2018 ikatoka hukumu kuwa mwekezaji ameshinda.

Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Amos Gabriel Makalla alipoulizwa na JAMHURI ameshauri wananchi hao kama hawajaridhika na uamuzi wanapaswa kuendelea na ngazi inayofuata ya Mahakama na si kukimbilia serikalini.

By Jamhuri