Ninaweza kusema kuwa wanachama wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) bado wana imani na Freeman Mbowe, baada ya mkutano mkuu wake kuonyesha imani naye na kumwacha aendelee kushikilia usukani wa kukiongoza kwa kumpa tena nafasi ya kuwa mwenyekiti wake wa taifa.

Huo ni ushindi uliopatikana katika mazingira yenye utata mkubwa. Ni utata unaotokana na nguvu za dola kutaka hilo lisifanikiwe, lakini Mungu ni mkubwa, limefanikiwa, tena kwa kishindo kikuu!

Katika mazingira aliyomo ninashindwa kumpongeza Mbowe yeye kama yeye, ila ninasema ni ushindi wa wananchi wote wa Tanzania. Ninasema hongera Watanzania. Nitaeleza kwa nini ninasema hivyo.

Mara nyingi nimewafananisha viongozi wa Chadema na viongozi wa wananchi walio wengi wa Afrika Kusini enzi za makaburu, kina Mandela na wenzake. 

Kuna watu wenye kasumba ya kutotaka kuwafananisha viongozi hawa wakidai huwezi kumlinganisha Mandela na Mbowe wala Lissu.

Sioni tofauti kati ya viongozi hawa ipo wapi, kwa sababu wote ni wanasiasa na wapinzani wa serikali zilizopo madarakani. Hatuwezi kusema Mandela alikuwa mtume wa Mungu wakati Mbowe na Lissu ni binadamu wa kawaida, hapana, wote ni wanasiasa, tena wa upinzani. 

Kabla hajachaguliwa kuwa rais, Mandela ameendesha harakati zake za kisiasa akiwa mpinzani, tena mpinzani hasa wa serikali ya makaburu hadi kufikia hatua ya kufungwa gerezani. Mandela alinusurika kuuawa mara kadhaa kutokana na upinzani wake kwa serikali.

Hatuwezi kufananisha yaliyomtokea Mandela kila moja na yale yaliyomtokea Mbowe, msingi hapa ni kuwa wote ni wanasiasa wapinzani kwa serikali zao.

Tofauti ni kwamba Mandela alipigania haki ya kutaka watu wote wa nchi yake wawe nayo bila kubaguana kwa rangi kama ilivyokuwa kwa miaka mingi Afrika Kusini. Mbowe naye anataka haki iwepo kwa watu wote bila kubaguana kwa itikadi. Tofauti yao ni hiyo; wakati Mandela akipigana dhidi ya ubaguzi wa rangi, Mbowe yeye anapigania usawa wa kiitikadi.

Wale waliobaguana kwa rangi wana afadhali kidogo, kwa sababu walikuwa na cha kuonyesha, ubaguzi wa rangi.

Wakisema mweusi hapaswi kufanya hivi na vile, inaonekana wazi, maana anayesema hivyo ni mweupe. Ni tofauti na ubaguzi wa kiitikadi, kwa sababu hiyo ni tofauti isiyoonekana waziwazi. Ni tofauti iliyo ndani ya mioyo ya wanaoitamani, hivyo ni vigumu sana kuwapambanua watu kwa tofauti za kiitikadi.

Ndiyo maana, wakati mwingine chama fulani kinaweza kumkaribisha mwanachama kikiamini kuwa ni mwenzao kiitikadi. Lakini baadaye inakuja kubainika kuwa kumbe mtu huyu wala hana itikadi sawa na ya kile chama. Matokeo yake ni migogoro ya mara kwa mara katika vyama. Haya yametokea hata ndani ya Chadema.

Kwa wasioelewa maana halisi ya itikadi na umuhimu wake katika uendeshaji wa chama cha siasa, wanaweza kumuona Mbowe kama mpiga kelele tu pale anapodai usawa wa kiitikadi. Lakini kimsingi chama chochote cha siasa ni itikadi. Bila itikadi hakuna chama, bali ni kikundi tu cha watu ambao wanadhani wana masilahi ya pamoja. Itikadi ndiyo itakayoonyesha dira na mwelekeo wa chama. Itikadi ndiyo inatoa misingi ya chama. Bila mwelekeo mzuri na misingi imara, hamuwezi kuwa na chama cha siasa.

Wenye mapenzi ya kweli na nchi yao ni lazima walione hilo la itikadi sambamba na kuushangilia ushindi wa Mbowe, kwa sababu ni ushindi unaoiweka nchi yetu mahali salama. 

Wapo vibaraka ambao bila shaka kwa malipo wanatumwa kukichafua chama, kitu ambacho kimejitokeza na kuwasuta vibaraka wenyewe!

Marehemu Dk. Jonas Malheiro Savimbi wa UNITA alikuwa hakubaliani na yaliyokuwa yakifanyika nchini mwake, Angola. Ilikuwa ni tofauti ya itikadi, lakini badala ya kuidai kisiasa yeye akaamua kuingia msituni kudai itikadi kwa mtutu wa bunduki. 

Matokeo ya uamuzi huo yaliigharimu sana Angola na watu wake, kwani vita, vifo, uharibifu wa mali na kadhalika ndiyo yalikuwa matokeo ya uamuzi aliochukua Savimbi. 

Moja ya nchi tajiri sana barani Afrika ikawa nchi maskini, licha ya rasilimali nyingi hizo, kutokana tu na kushindwa kutumia muda wake kuleta maendeleo na badala yake kutumia muda huo kupigana vita ya mwenyewe kwa wenyewe!

Kwa hiyo, waliokuwa na upeo waliweza kushangilia mafanikio ya Dk. Savimbi, kwani ilipobainika anachokitaka ni nini, walizungumza naye akakubali kuacha kudai itikadi kwa mtutu wa bunduki ingawa hilo lilikuja kumuangamiza baada ya mabeberu wa nje kuingilia kati na kummalizia!

Ndiyo maana ninasema hata hapa ushindi wa kishindo wa Mbowe ni ushindi wa nchi na wananchi. Tunapaswa tuushangilie kwa pamoja, Wana Chadema na wasiokuwa Wana Chadema, kwa sababu matokeo ya ushindi huo ni amani na faraja kwetu sisi sote. Tuna bahati kwamba Mbowe na chama chake wameamua kupigania usawa wa kiitikadi kwa njia ya kisiasa na si mapigano ya msituni.

Nawashangaa vibaraka wanaojitokeza na kumpinga Mbowe, wakidhani kwa kufanya hivyo wanaufurahisha utawala uliopo madarakani. Vibaraka hao wanahitaji kujifunza kutafakari. Anachokifanya Mbowe ni faida kwa nchi yake na uongozi uliopo madarakani. Kwa hiyo, kumsuguasugua na kumsemasema wakidhani wanafanya kitu cha maana, inawabidi watafakari.

Mafanikio ya mkutano wa Chadema yanahitaji kupigiwa mfano hata na chama tawala. Ni mafanikio ya watu waliojitoa kukifanikisha walichokilenga, watu ambao ni ‘committed in the real sense’,  ndiyo maana tumeweza kuona mtu anahutubia mkutano huo tokea ughaibuni, Tundu Lissu, na wajumbe wakampa umakamu wa mwenyekiti kwa kishindo.

Wapo baadhi ya watu wanaofanya mambo, sijui kwa kutumwa kama njia ya ushushushu. Mtu anaamua kujiunga Chadema na watu wanamheshimu na kumpa haki hiyo wakiamini kuwa itikadi ya chama ndiyo iliyomvuta. Halafu ghafla, wakati itikadi haijabadilika, yeye anageuka na kuamua kuondoka Chadema. Hapo unafahamu mara moja kuwa kumbe kilichokuwa kimemleta Chadema si itikadi, bali jambo jingine ambalo hakuliweka hadharani.

Hiki ni chama chenye kuhitaji watu makini. Ndiyo maana ninauona umuhimu wa kumpongeza Mbowe ambaye licha ya misukosuko bado amesimama imara kutetea kile anachoamini. Ni mtu makini, anakiona na kukitambua alichokilenga, tofauti na wanaopeperushwa na upepo kama vishada!

Katika masuala ya siasa, mimi ni mpenzi wa Madiba, mzee Nelson Mandela. Msimamo wake usioyumba ndio ulimfanya kutoka kifungoni na kuwa rais wa kwanza mweusi kwa heshima ya nchi yake.

Fikiria mtu anajitokeza kuwa rubani wenu, amekwisha kukiondoa chombo na kipo angani, mara anajitoa na kutaka kujirusha chini! Fikiria majaliwa yenu yatakuwaje! Au anaondoa chombo cha majini na mkifika maji marefu anabadilika kwamba yeye ameacha unahodha, anataka ashuke na kujirusha majini kwa vile yeye ni bingwa wa kuogelea! Mtamuelewaje mtu wa hivyo?

Madhara yoyote yanayoweza kutokea si kwamba yatawahusu tu wale waliomo ndani ya chombo ila hata walio nje ya chombo. Mfano, rubani akiamua kuacha kuirusha ndege iliyo angani, haijulikani itakapoanguka itafikia wapi. 

Inaweza kufikia kwenye umati wa watu, na hapo hata ambao hawakuwa kwenye ndege hiyo wataathirika. Ndiyo maana ninasema panahitajika tafakuri kabla ya kuupongeza uamuzi wa watu wanaopeperushwa na upepo kama vishada.

prudencekarugendo@yahoo.com

0784 989 512 / 0654 031 701

191 Total Views 2 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!