Home Makala KESHO YAKO

KESHO YAKO

by Jamhuri

Anza kujiandaa.  Kesho inaanza leo. Panda mbegu za kesho leo. Ukweli ni kwamba kesho njema hujengwa na leo njema. Ikiwa leo njema imekosewa, hakuna kesho njema yenye mafanikio. Rais wa 36 wa Marekani, Lyndon B. Johnson anasema: “Jana si ya kwetu tena na hatuwezi kuirudisha, ila kesho ni yetu ya kushinda au kushindwa.”  

Kama jana ulishindwa katika jambo fulani, usikubali na kesho ushindwe katika jambo hilohilo. Tafuta namna nyingine ya kukabiliana nalo na kushinda.

Jana haiwezi kubadilishwa, lakini kesho inaweza kubadilishwa. Ibadilishe kesho yako kwa kujifunza kupitia yaliyokupata jana. Usipambane na maumivu yako ya jana. Kumbuka: ‘Hauwezi kuirudisha jana’.  Kupambana na jana ni kupoteza uelekeo wako wa maisha.  Jana imepita na maumivu yake yote. 

Historia ya jana ilibaki jana. Hamishia nguvu zako kesho. Fokasi kesho. Methali ya Kiarabu inasema: “Yajayo ni mazuri zaidi kuliko yaliyopita.” Usihuzunike kwa sababu ya historia yako ya jana. Bado una nafasi nzuri ya kufanikiwa. Una nafasi ya kuandika upya historia ya maisha yako.

Rais wa zamani wa Marekani, Abraham Lincoln, anasema: “Namna nzuri ya kubashiri kesho itakavyokuwa ni kuiumba.” Wewe ndiye muumbaji wa maisha yako.  Umba maisha yako vizuri.  Umba kesho yako itakavyokuwa. Anza kuiumba kesho yako leo. Umba leo maisha unayotaka uishi kesho. 

Kumbuka; Ukitaka kuwa mtu mwema kesho, kuwa mtu mwema zaidi leo. Uamuzi wako wa leo unaweza kuiharibu kesho yako au unaweza kuijenga kesho yako. Jenga leo yako vizuri ili kesho yako iwe imara (nzuri).

Kesho inajengwa na msingi wa leo.  Kesho haiwezi kujengwa na msingi wa kesho. Kesho haiwezi kutengenezwa kesho. Mwanaharakati Mahatma Gandhi anasema: “Kesho inategemea tunayofanya leo.” Matunda ya kesho yanapandwa leo. Panda leo unachotaka uvune kesho.

Pambana na mazingira yanayokuzunguka ili uibuke bingwa. Tafakari ushuhuda huu wa maisha ya Nick Vujicic aliyezaliwa Disemba 4, 1984 nchini Australia. Alizaliwa akiwa hana miguu wala mikono. Mwaka 2002 Vujicic alimuoa Kane Mihayara. Vujicic na mke wake wamejaliwa kupata watoto wanne. Akiwa na umri wa miaka 10 alimwambia mama yake mzazi maneno haya: “Mama, nina nia ya kufanikiwa na nitafanikiwa.”

Katika kitabu chake cha kumbukumbu, Nick Vujicic aliwahi kuandika hivi: “Kesho inang’aa kuliko jana.” Vujicic amefanikiwa sana. Leo hii dunia nzima inasoma vitabu vya hamasa vilivyoandikwa naye. Nick Vujicic anafanya mikutano ya kutoa hamasa kwa watu kujituma kufanya kazi. Vujicic ni miongoni mwa mabilionea duniani.

Kesho yako inan’gaa.  Kesho yako inakuja, tena kesho yako ni ya matumaini na mafanikio makubwa. Ingoje kwa furaha. Mwandishi Henrieta C. Mears anasema: “Mungu anatuacha tushindwe katika jambo ambalo si la msingi ili tuweze kufanikiwa katika jambo ambalo ni la msingi.”

Kuna nyakati fulani, mtu anahisi kuwa hawezi kuona njia kwa urahisi. Anawahi kuhitimisha kwa kusema: “Hapa siwezi.” Kumbuka: Pale unaposema, hapa nimefika mwisho, Mungu anasema: “Huu ni mwanzo mpya.”  Mwandishi na mshairi wa Marekani, Albert Laighton, anatutia moyo kwa ujumbe huu: “Pale mwanadamu anapoona majani yamekauka, Mungu anaona maua mazuri yamechanua.”

Ambatana na watu ambao wako tayari kukuona ukitimiza ndoto yako.  Watu ambao wanailinda kesho yako. Usiandamane na watu ambao hawana mtazamo chanya juu ya maisha. Ukiandamana na watu waliofanikiwa,  kesho yako itakuwa ya mafanikio. 

Mwandishi Mark Ambrose anasema: “Nionyeshe marafiki zako nami nitakuonyesha wakati wako ujao.”  

Mchungaji  Joel  Osteen  anasema: “Unahitaji kujichanganya na watu ambao wanakuhamasisha, watu ambao wanakupa changamoto ya kupanda juu zaidi, watu ambao wanakufanya uwe mzuri zaidi. Usipoteze muda wako wa thamani na watu ambao hawaongezi chochote katika kukua kwako.”

Pambana leo ili kesho ikuheshimu. Norman Causin anasema: “Kifo si hasara kubwa kuliko zote kwenye maisha. Hasara kubwa kuliko zote ni kile kinachokufa ndani yako wakati bado unaishi.”  Jiulize: ‘Ni  kitu gani kimekufa ndani yako?’ Je, ndoto ya maisha yako imekufa au bado iko hai?  Kuna  watu wengi ambao wameruhusu  mambo makubwa yaliyo ndani yao yafe wakiwa bado hai. 

Wengi wamebaki kulalamika. Wanalalamikia mazingira waliyokulia.  Wanazilalamikia familia zao. Wanailalamikia serikali yao. Acha kulalamika. Bado hujachelewa kufanikiwa. Chapa kazi. Usikubali kipaji chako kife ungali bado unaishi. Usikubali maono yako yafe ungali bado unaishi. 

Rafiki yangu Emmy Paul alinitumia ujumbe kwenye simu yangu ya mkononi. Ujumbe wake ulikuwa unasomeka hivi: “Usiangalie jana kwa hasira wala kesho kwa woga, itazame leo kwa hekima na busara huku ukijipanga kusonga mbele kwa kumtanguliza Mungu kwa kila jambo. Usiogope maneno ya wanaokusema vibaya, maana maneno ni HERUFI tu zilizounganishwa na kupewa sauti. Lawama na maelezo mengi ni mali ya walioshindwa, lakini walioshinda wana maneno mawili mtu: “MALENGO na JITIHADA.” Maneno haya yalinibariki na kunifariji.  Naomba na wewe yakufariji na kukubariki.A

You may also like