Mbunge jangili

Wakati wabunge kadhaa wakijiandaa kukwamisha Bajeti ya Wizara ya Maliasiali na Utalii, imebainika kuwa miongoni mwao ni watuhumiwa wakuu wa ujangili.

Wabunge hao wameunda umoja usio rasmi, kupinga kutekelezwa kwa Operesheni Taifisha Mifugo, iliyotangazwa na Serikali kupitia Waziri wa Maliasili na Utalii, Profesa Jumanne Maghembe, na kutiwa nguvu na Makamu wa Rais, Samia Suluhu Hassan.

Operesheni hiyo imepangwa kutekelezwa Juni 15, mwaka huu katika mapori yote yaliyovamiwa na mifugo.

Miongoni mwa wanaopinga kutekelezwa kwa Operesheni hiyo ni Mbunge wa Meatu, Salum Khamis Salum (CCM), ambaye anatajwa kwenye orodha ya watuhumiwa wa ujangili.

Salum, kama walivyo wabunge wengine, wanapinga kuondolewa kwa mifugo, hasa ng’ombe katika Pori la Akiba Maswa, ambalo linaelekea kufa kutokana na kulemewa na maelfu ya mifugo.

Lakini uchunguzi wa JAMHURI umebaini kuwa uingizaji mifugo katika Mapori ya Hifadhi, pamoja na kusaka malisho, unalenga zaidi kuwawezesha majangili kuua wanyamapori wakiwamo tembo.

Kumbukumbu zinaonesha kuwa Mbunge Salum kwa nyakati tofauti, yeye na baadhi ya watu alio na nasaba nao, wamekuwa wakitajwa kwenye matukio ya ujangili.

Mwaka 2009 gari la kampuni yake ya Jambo, aina ya Toyota Land Cruiser lilikamatwa katika Pori la Akiba Maswa likiwa na idadi kubwa ya wanyamapori waliouawa kinyume cha sheria.

Ilibainika kuwa vibali vya uwindaji havikuwaruhusu kuwinda katika pori hilo. Silaha zilizotumika kuua wanyama hao ni tofauti na zilizoandikishwa kwenye vibali, na pia idadi ya wanyama ilipindukia ile iliyohalalishwa kisheria. Ofisa aliyewakamata alikuwa Honest John.

Waliokamatwa kwenye gari la mbunge huyo kwa ujangili ni John Makuru, Musa Maziku, Seif Lyale, Sita Isong’ombe, Ramadhan Ali na Godfray Milyango. Walifunguliwa kesi ya ujangili Na. EC.11/2009 katika Mahakama ya Meatu. Walipewa adhabu ya faini.

Miaka mitatu baadaye, pembe za tembo zilikamatwa katika basi, mali ya kampuni ya Jambo Bus Transport; inayomilikiwa na Mbunge Salum. Pembe hizo zilikamatwa karibu na Kijiji cha SakaSaka, Meatu mkoani Shinyanga.

Watuhumiwa wawili – Jackson Bambebuye na Matiku Nsenga, walifunguliwa kesi ya ujangili Na. EC.17/2012 katika Mahakama ya Meatu.

Aidha, mwaka 2013 watu wanaotajwa kuwa na uhusiano wa kinasaba na Salum walikamatwa katika Hifadhi ya Jamii za Wanyamapori (WMA) ya Makao, na kushitakiwa kwa makosa saba yakiwamo ya ujangili.

Washitakiwa hao ni Fahad Said, Salum Amary, Seif Ally, Zaid Said na Mohamed Hilal – wote wakazi wa mjini Shinyanga.

Walishitakiwa kwa makosa saba yakiwamo ya kuwinda kinyume cha sheria ndani ya WMA, kuingia kinyume cha sheria ndani ya WMA, kuingia na silaha ndani ya WMA kinyume cha sheria, kuua wanyamapori ambao hawakuidhinishwa kuuawa, kutumia mbinu zisizoruhusiwa katika kuua wanyama, kukamatwa wakiwa na nyara za Serikali kinyume cha sheria na kushindwa/kupuuza kurekodi wanyama waliowaua kwenye leseni ya uwindaji.

Mtandao wa ujangili umekuwa ukiwahusisha baadhi ya viongozi wakubwa serikalini na katika vyombo vya usalama.

Mbunge huyo amekuwa akilifanya suala hili kuwa siri kubwa na wananchi wenye uzalendo wa hali ya juu, walilifikisha kwa gazeti la JAMHURI, wakiomba lichunguzwe kwa maelezo kuwa mbunge huyu bado anaendelea na mchezo wa kuua wanyamapori.

Gazeti la JAMHURI limefanya juhudi kwa zaidi ya mwezi sasa kuwasiliana na Mbunge Salum, lakini pamoja na kumpelekea maswali, amekaa kimya na wakati mwingine anawakimbia waandishi wa gazeti hili kila akikutana nao.

Mwaka 2012, bunduki tatu za aliyekuwa Mbunge wa Tunduru Kusini, Mtutura Mtutura (CCM), zilikamatwa kwa matukio ya ujangili katika Pori la Selous – Niassa, lililopo Tunduru, mpakani kwa Tanzania na Msumbiji.

Silaha hizo zilikamatwa zikiwa na msaidizi wa mbunge huyo aliyetajwa kwa jina moja la Nakale, ambaye ni mkazi wa Kijiji cha Chiungo, Tarafa ya Namasakata wilayani Tunduru. Mahakama ya Wilaya ya Tunduru ilimhukumu kifungo cha nje cha miaka miwili.

Kukamatwa kwake kulitokana na Operseheni Malihai iliyoendeshwa na aliyekuwa Kamishna Msaidizi Mwandamizi (SACP) wa Jeshi la Polisi, Simon Sirro, na Kamanda wa Kikosi dhidi ya Ujangili wa Wizara ya Maliasili na Utalii, Venance Tossi. Kwa sasa Siro ni Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam.

Katika ushahidi wake mahakamani, Chiungo alikiri kuwa bunduki hizo ni mali ya Mtutura.

Aliyekuwa Waziri wa Maliasili na Utalii, Lazaro Nyalandu, ni miongoni mwa watuhumiwa wa ujangili. Anatajwa kuwa mmiliki wa gari namba T 505 BKM, mwenye utambulisho wa mlipa kodi (TIN: 105-059-701), ambalo lilikamatwa na nyara za Serikali.

Gari hilo lilikamatwa na baadaye Ofisa Mtendaji wa Kijiji cha Mwanyonye mkoani Singida, Rehema Manji, alifungua mashitaka polisi akilalamika kutishiwa kwa bastola baada ya kulikamata gari hilo ambalo dereva wake aliamua kuvunja kizuizi na kukimbia baada ya kukamatwa akiwa na nyara.

Siri kubwa bado zimegubika orodha ya vigogo waliotajwa katika orodha ya majangili kabla na wakati wa Operesheni Tokomeza. Aliyekuwa Rais wa wakati huo, Jakaya Kikwete, aliwahi kulitangazia Taifa kwamba ana orodha ya majangili 40 ambao miongoni mwao inasemekana kuna viongozi wenye majina makubwa. Hadi anaondoka madarakani hakuwahi kuwataja au kuamuru kukamatwa kwa ‘majangili’ hao.

 

Umegaji maeneo ya hifadhi

Mbunge wa Viti Maalumu, Gimbi Masaba (Chadema), hivi karibuni bungeni alitaka Serikali itenge Pori la Akiba Maswa kwa ajili ya wafugaji.

Pori hilo linapakana na Hifadhi ya Taifa ya Serengeti kwa upande wa kusini na muhimu mno katika ikolojia ya hifadhi hiyo. Pori hilo limepunguzwa mara tano kwa nyakati tofauti ili kuwawezesha wafugaji kupata eneo la malisho.

Waziri wa Maliasili na Utalii, Profesa Maghembe, akimjibu Masaba, alisema Serikali haikusudii kutekeleza mapendekezo ya mbunge huyo akisema kufanya hivyo ni kuua uhifadhi nchini.

Wanasiasa, wafanyabiashara na viongozi wengine wenye ukwasi, hununua ng’ombe dhaifu na kisha kutumia malisho ndani ya hifadhi ili kuwanenepesha kabla ya kuwapeleka minadani. Hatua hiyo imesababisha kuwapo kwa shinikizo kubwa la kutaka maeneo ya hifadhi yamegwe.