Mmiliki wa kampuni ya Educational Books Publishers ya jijini Dar es Salaam, anadaiwa kumdhulumu mwandishi mahiri na mkongwe wa vitabu nchini, Mzee Yusuf Halimoja. Taarifa zilizolifikia gazeti hili zinaeleza kwamba mwaka 2010 mchapishaji huyo wa vitabu na Mzee Halimoja walikubaliana kwamba mwandishi huyo aandike vitabu vya kiada vya masomo ya uraia na historia vya darasa la saba.

Habari zinasema baada ya makubaliano hayo Mzee Halimoja alimtaka mchapishaji huyo wawekeane mkataba ambao ungetaja angelipwa lini kiasi gani cha fedha kwa kazi hiyo.

 

Inaelezwa kuwa mchapishaji huyo alimwahidi Mzee Halimoja kuwa wangewekeana mkataba mara baada ya vitabu vyake kuidhinishwa na Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi, na kwamba angemtangulizia malipo ya Sh milioni 50,000.

 

Halimoja amesema vitabu vyake vyote viliidhinishwa na wizara hiyo Januari 15, 2011 lakini mchapishaji huyo akavichapisha na kuanza kuviuza bila kumtaarifu.

 

Kufuatia hali hiyo, Halimoja alipeleka shauri hilo katika kituo cha Sheria na Haki za Binadamu akidai alipwe na mchapishaji huyo kiasi cha Sh milioni 500. Kituo hicho kikawasiliana na mchapishaji huyo. Agosti 4, 2011 kikafanyika kikao cha kutafuta maelewano.

 

Kwa mujibu wa habari hizo, mchapishaji huyo alikiri kuchapisha vitabu vya Mzee Halimoja bila kuwekeana naye mkataba na kwamba alikuwa ameahidi  kumtangulizia malipo ya Sh milioni 50.

 

Aidha, mchapishaji huyo alimtaka Mzee Halimoja asaini mkataba ambao ungeleta picha kwamba waliwekeana mkataba kabla hajachapisha vitabu vya Mzee Halimoja.

 

Inadaiwa kwamba Mzee Halimoja alikataa kupokea Sh milioni moja ili asaini mkataba feki uliokuwa umeandaliwa na mchapishaji huyo.

 

Inaelezwa kuwa wakati fulani mchapishaji huyo alimtaka wakili wa Mzee Halimoja aende ofisini  kwake peke yake wakazungumzie suala hilo lakini wakili akakataa akisema hawezi kwenda bila mteja wake.

 

Mchapishaji huyo, Mohamed alipohojiwa na JAMHURI kuhusu malalamiko hayo alikiri kuchapisha vitabu hivyo bila kuwekeana mkataba. Alitaka mwandishi wa habari ampeleke Mzee Halimoja wakawekeane mkataba wa kuchapisha vitabu alivyokwisha kuvichapisha.

 

Hata hivyo, Mzee Halimoja alipinga hoja hiyo akisema hawezi kwenda kuwekeana mkataba bila wakili wake anayeshughulikia shauri hilo.

 

Kuna taarifa za kuaminika kwamba mawakili wa Mzee Halimoja wamejipanga kumfungulia mchapishaji huyo mashtaka mawili mahakamani. Kwanza shitaka la jinai la kuiba kazi za Mzee Halimoja. Pili shitaka la madai ya kuchapisha na kuuza vitabu vya Mzee Halimoja miaka mitatu bila kumpa chochote.

 

By Jamhuri