Mpendwa msomaji, leo kwa mara ya kwanza nadhani katika safu hii kupitia gazeti JAMHURI, nalazimika kuandika masuala yanayohusiana na kinywaji. Nimelazimika kuandika suala hili, baada ya kuona kadhia ya kodi inayoendelea hapa nchini. Serikali imekoma kufikiri na sasa imeamua kutengeneza kitanzi cha kunyonga biashara hapa nchini.

Mwishoni mwa wiki nimesoma orodha ya miswada sita inayopelekwa bungeni, sikuona ule ulioahidiwa wa kusitisha tozo ya simu ya Sh 1,000 kwa kila simu kila mwezi. Wakati nikipata mshituko huo, nikakuta Serikali imeanzisha kodi ya zuio. Hii haijapigiwa kelele, lakini wafanyabiashara wakiifahamu vyema nasubiri kuona maandamano.

 

Sitanii, kodi hii ni ya ajabu. Kama kawaida wabunge wetu wakiwa wamesinzia imepitishwa kwa kuvangwa. Nao bila ajizi wakapiga kura za ndiyoooooooooo. Leo Rwanda tayari wametangaza kuanzia Septemba Mosi hawatapitisha mizigo yao nchini. Serikali yetu imejifanya kuwapuuza, lakini tutakiona cha moto.

Hii kodi ya zuio ni DECI nyingine. Ukiuza bidhaa yoyote kwa mtu yeyote au kampuni yoyote kwa sasa, kabla ya kukupatia malipo yako anakata asilimia 5 anaipeleka TRA kila mwezi. Mimi nilifikiri ni mchezo, ila mteja mmoja aliyeputa tangazo mwezi huu tukampelekea ‘invoice’ wakati wa kututulipa amekata asilimia tano. Hii ndio kodi ya zuio.

 

Wanyarwanda wamesema, kwa sasa wasafirishaji wameongeza bei ya kusafirisha mizigo kwa maelezo kuwa fedha wanazolipwa zinakatwa tena asilimia 5 bila kujali kuwa ni mtaji au faida. Kwa kawaida sheria za fedha zinasema mtaji haukatwi kodi. Ukikata mtaji kodi maana yake ni kwamba unataka kuua biashara. Hiki kinatokea hapa kwetu.

 

Maana yake ni nini? Kwamba nimetumia Sh milioni 3.65 kuchapa gazeti kwa wiki, ndani ya gazeti nimeweka tangazo lenye thamani ya Sh milioni 3.0, wakati wa kulipwa nikikatwa asilimia 5 maana yake ni kuwa nitakatwa Sh 150,000 kwenye mtaji kila wiki. Hii ina maana kuwa hii Sh milioni 3.0 bado haikuwa faida, bali ni sehemu ya mtaji nilioutumbukiza kuchapa gazeti, nikiongeza mauzo ya nakala moja moja ndipo narejesha mtaji wa milioni 3.65 nilizoweka, hivyo kwa kunikata kodi kwenye mtaji Serikali inazidi kudidimiza mtaji wangu.

 

Hii maana yake ni kwamba nikiendelea kupata tangazo la Sh milioni 3.0 kila wiki, Serikali ikaendelea kukata asilimia 5 kila wateja wanaponilipa, ina maana kila mwezi kwenye mtaji wangu huu Serikali itakuwa inakata Sh 600,000 kila mwezi, na baada ya miezi mitano Serikali itakuwa tayari imechukua milioni 3.0 zote, nami nafunga biashara rasmi.

 

Sitanii, inawezekana washauri wa Serikali hawajafikiri sawa sawa katika hili. Duniani kote mtaji hautozwi kodi. Sina uhakika wabunge wetu wana uelewa kiasi gani, lakini hiki tunachofanya itakuwa kama kosa alilofanya Zakia Meghji alipoteuliwa kuwa Waziri wa Fedha. Bila kufahamu mama huyu alipandisha kodi za mafuta ajabu, mwisho wa siku zikamgeuka.

 

Alipandisha bei za usajili wa magari, ushuru wa mafuta na kila kitu akidhani Serikali itakusanya mabilioni, kumbe akajikuta ameua uchumi. Na hakika tangu mwaka 2006/2007 baada ya ile bajeti ya Meghji uchumi haujawahi kutulia. Ilifika mahala hata Serikali mambo yakaitokea puani hadi ikalazimika kushusha bei za usajili wa magari. Inavyoelekea hatukujifunza.

 

Sitanii, kitakachotokea hapa ni wafanyabiashara kuongeza bei za bidhaa na huduma zao, na anayelipia ni mwananchi, ambaye ni mpigakura. Hivyo maisha kwa kila Mtanzania yatazidi kuwa magumu. Watanzania watakamuliwa hadi senti ya mwisho, na wakitoka hapo ukawambia “KIDUMU KILE CHENYEWE…” Usishangae wakikujibu “Pawaaaaaaaaaa”.

 

Nasema haya tunayataka wenyewe. Inakuwaje kuna fedha ziko nje nje, lakini tunaziachia? Kwa mfano hivi karibuni nilikuwa Bujumbura. Katika hoteli niliyofikia nikaona watu wanakunywa bia ya Serengeti. Nilipouliza inapatikana wapi, wakaniambia nisiseme kwa sauti maana inaingizwa Burundi kimagendo. Wakaniambia Serengeti inauzwa kama bangi nchini humo.

 

Kwa Warundi, kinywaji ni jadi. Burudani yao namba moja ni pombe na ya pili ni hiyo nyingine. Kwa Burundi anayekunywa Serengeti anaheshimika kama mtu anayekunywa Heineken hapa kwetu. Nilipouliza kwa nini wasifuate taratibu wakaingiza bia hizo kihalali, wakasema wenye kiwanda cha Serengeti wamezubaa tu.

 

Sitanii, siku chache zilizopita nikiwa kwenye ndege nakwenda Mwanza, nikakaa kiti kimoja na mmoja wa Wakurugenzi wa Serengeti. Nikamwambia habari hiyo. Akanipa maelezo marefu na ya kusikitisha. Akaniambia wameomba mara nyingi kupeleka Serengeti Uganda, Rwanda na Burundi, lakini Serikali inawanyima kibali. Akasema hata Uganda wanaomba wauziwe, ila Serikali yetu inakataa.

 

Nikamwambia nitaifanyia kazi. Kumbe naye ndio wale wale. Kwenye ndege alikuwa anafurahisha genge. Tuliporejea hapa Dar es Salaam ikawa kila nikimpigia simu hapokei. Nikamuuliza kwa sms kuwa kwani vipi mbona ananikaushia? Akasema yeye si msemaji wa Serengeti akanitumia namba ya msemaji. Msemaji nikampigia zaidi ya mara 10 hapokei.

 

Ulivyopita mwezi na zaidi nikamtumia ujumbe mfupi mkurugenzi wa awali. Nikamwambia wakati mnailalamikia Serikali nanyi hamfai. Taarifa hii ambayo ingewafaa kibiashara kwa wao wanakuwa warasimu kuitoa? Nadhani baada ya ujumbe huo akampigia mwenye jukumu la kusema. Huyu naye ndipo akanipigia na kusema hajawahi kuona simu yangu.

 

Nikamwambia sasa umeiona nipe hizo habari, akasema anasafiri nje ya nchi akirejea angenitafuta Jumanne ya wiki inayofuata. Sasa ni wiki ya tatu. Nimeanza kuapta wasiwasi kuwa hata malalamiko yao ni ya uongo. Huenda Serengeti wenyewe hawajawahi kufanya lolote, wanasubiri Serikali ndio iwatafutie masoko. Kwa urasimu niliouona, hakika unaweza kuhalalisha wanachotendewa na Serikali.

 

Sitanii, pamoja na urasimu wa Serengeti, Serikali kupitia Mamlaka ya Mapato Tanzania nilitarajia ingeiona fursa hii. Ingeweza kuchukua jukumu na hatua za msingi kuwezesha bidhaa za Tanzania kupata soko nje ya nchi hasa kwa kushirikiana na Wizara ya Viwanda na Biashara na hapa tungeingiza fedha za kigeni, mapato yangekuwa makubwa tungesahau kodi za simu na hizi za zuio ambazo ni za manyanyaso.

 

Wakati nikipigwa butwaa na hili la Serengeti, nikapata fursa ya kukutana na wakurugenzi wa kiwanda cha Konyagi; Tanzania Distillers Limited. Hawa wanaeleza kilio cha wazi. Kwanza kabla sijazungumzia kilio, nieleze mafanikio. Kwa sasa kiwanda hicho kinauza Konyagi katika nchi za Kenya, Uganda, South Sudan, Rwanda na Marekani. Mazungumzo ya kuuza Konyagi Ulaya yanaendelea.

 

Kutokana na biashara hiyo, kodi mbalimbali zinazolipwa na kiwanda cha Konyagi zinafikia wastani wa Sh bilioni 7.0 kwa mwezi. Kiasi hiki cha bilioni saba ni karibu bajeti ya baadhi ya wizara. Hii ina maana kuwa kama nchi ingepata viwanda 100 vyenye uwezo wa kulipa bilioni saba kwa mwezi, nchi hii ingeweza kupata wastani wa Sh bilioni 700. Hapa tungeishi kwenye nchi ya maziwa na asali.

 

Konyagi ni mmoja kati ya walipa kodi 11 wazuri Tanzania. Hii inathibitisha umuhimu wa viwanda katika kujenga uchumi. Ikumbukwe wazalendo hawa akina David Mgwassa, wamekifufua kiwanda hiki kutoka kwenye mazingira ya kupewa ruzuku sasa kinalipa kodi ya bilioni saba kwa mwezi. Kwa kila hali wanahitaji pongezi. Hawa ndio wazalendo wa kweli.

 

Sitanii, wakati Watanzania hawa wakifanya kazi ya kizalendo, Serikali imewaacha wanaogelea kwenye bwawa la mamba. Bodi ya wazalishaji Kenya ijulikanayo kama NACADA kwa muda mrefu sasa inaitangaza Konyagi kama Chang’aa (gongo). Konyagi ilianza kuingizwa nchini Kenya ndani ya chupa za mililita 200 ikapendwa kama ubwabwa, wakaupiga marufuku ujazo huo.

 

Kwa mbinu wakijua kuwa lazima watawaumiza Konyagi, wakasema lazima Konyagi kuuzwa nchini humo iwe na ujazo wa mililita 205. Kiwanda cha Konyagi kikatii maelekezo haya yaliyotolewa na Shirika la Ubora wa Viwango nchini Kenya (KEBS). Mara tu Konyagi walipoanza kuingiza Kenya Konyagi ndani ya ujazo huo wa mililita 205 wakapewa maelekezo mapya kuwa zinahitajika ziingizwe za mililita 250.

 

Hii maana yake nini? Maana yake wanajua kuwa Konyagi wamekwishaingia hasara ya kutengeneza chupa. Wanajua kuwa hizo chupa hazitakuwa na mtumizi za ujazo wa mililita 205 zikipigwa marufuku. Lakini ajabu, Wakenya wenyewe wanaendelea kuuza vileo vyao hapa nchini kwetu kwa ujazo wa mililita 205. Vileo hivi sio siri, ni pamoja na Sminoff Vodicka, Richot, Gilbreys gin, Bond 7 na Gordon’s.

 

Duniani kote vile ndio chanzo kikubwa cha mapato. Nchi kama Scotland wananchi wake wanaishi maisha ya raha kwa kuuza wine, whisky na gin. Hizi zinawaingizia kodi nyingi ajabu. Ndio maana unaweze kuona Konyagi pamoja na mizengwe yote hiyo wanayopigwa, bado wanaweza kulipa mapato ya wastani wa Sh bilioni 7.0 kila mwezi.

 

Sitanii, hapa kinachostahili ni Serikali kuingilia kati. Itifaki ya Afrika Mashariki inasema bidhaa yoyote ikiishathibitishwa na moja ya Shirika la Viwango kutoka upande moja, basi upande mwingine au nchi yeyote mwanachama ndani ya Jumuiya ya Afrika Mashariki haipaswi kuikagua tena. Kwa Kenya, wanaipuuza TBS yetu iliyopitisha ubora wa Konya inakiuka itifaki.

 

Kinachonisikitisha si hicho tu, ni kuona wao wanauza kwetu vileo vyenye ujazo wanaokataa sisi tusiuze kwao, na bado Serikali yetu haitoi tamko lolote. Konyagi wamewasilisha malalamiko haya katika Bunge la Afrika Mashariki, na wameshinda kesi, lakini hadi sasa utekelezaji ni sifuri. Konyagi inapendwa Kenya kama ubwabwa, na wakubwa wale wamezuia viroba.

 

Hoja ya kuzuia viroba ni kukataa wanywaji wadogo wadogo wasiikimbilie Konyagi na kususa vinywaji vinavyouzwa kwa bei kubwa ndani ya chupa nchini humo. Mimi nasema kwa kodi wanazolipa Konyagi, si busara kuruhusu Wakenya wakaendelea kutuburuza sokoni. Serikali yetu iingilie kati. Ikiwa Wakenya hawataki, basi na sisi tuzuie vinywaji vyao kuingia nchini mwetu.

 

Sitanii, Serikali yetu ikipigania viwanda kama Konyagi na Serengeti, fedha za kigeni zitakuja nyingi na haitakuwa na haja ya kufikiria kuanzisha kodi ya simu au kodi ya zuio itakayoishia kutafuna mitaji ya Watanzania na mwisho kuua kampuni za wazawa. Katika hili nasema Serikali ifikirie na kuchukua hatua sitahiki. Isimame kidete kusema unyanyasaji wa Wakenya hapana. Ila hata Seregeti wajirudi.

 

1728 Total Views 2 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!