mchechuShirika la Nyumba la Taifa (NHC) chini ya Mkurugenzi Mkuu, Nehemia Mchechu limefanikiwa kubadili sura ya jiji la Dar es Salaam kwa kujenga nyumba bora za makazi na biashara.

Wakati wananchi walio wengi wamekuwa wakiishi mbali na Jiji la Dar es Salaam, huku wengi wakitumia gharama kubwa za usafiri kutoka nje ya mji kuingi kila siku, Mpango wa Ujenzi wa nyumba katika maeneo kama Morocco, Kawe, Mchikichini, Victoria na mengine tayari umeanza kupunguza gharama za maishi kwa baadhi ya wananchi.

Miradi ya nyumba za makazi na biashara zinazojengwa katika makutano ya taa za Morocco katika barabara za Ali Hassan Mwinyi na Kawawa, unaojulikana kama Morocco Squre katika Wilaya ya Kinondoni, mbali na kuwapunguzia gharama za usafiri wananchi watakaopata fursa ya kuishi katika nyumba hizo, kwa jinsi zinavyojengwa zikikamilika zitakuwa kivutio cha utalii jijini Dar es Salaam.

Miradi ya Morocco Square Kinondoni na Seven Eleven (711) Kawe, italiweka jiji la Dar es Salaam katika mandhari inayovutia kwa wageni na Watanzania kwa ujumla na kulifanya Jiji la Dar es Salaam kuwa la kisasa likilinganishwa na majiji mengine duniani.

Kutokana na Serikali kutambua kuwa makazi bora ni jambo muhimu kwa maendeleo ya taifa na kuifanya sekta ya nyumba kuwa endelevu na yenye tija kwa wananchi na uchumi, ndiyo maana kwa ubunifu na jitihada zinazochukuliwa na NHC chini ya Mchechu zimeliinua shirika hilo ambalo linalojiendesha kwa tija.

NHC wametumia vyema Sheria ya Mikopo ya Nyumba (The Mortgage Financing Special Provision Act) ya mwaka 2008 iliyoanzishwa kwa lengo kuwezesha wadau wa sekta ya nyumba kushiriki kikamilifu katika kukuza sekta hii muhimu.

Tangu mwaka 2008 benki 19 kati ya 50 zilizopo nchini zimeanza kujihusisha na utoaji mikopo ya nyumba kwa Watanzania. Benki 16 kati ya hizo zimesaini makubaliano na NHC kutoa mikopo kwa wananchi wanaonunua nyumba zinazojengwa na Shirika hilo.

 

Mradi wa Kawe

Novemba 26, 2015 Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) lilizindua rasmi mauzo ya nyumba katika mradi mpya wa Seven Eleven (711) eneo la Kawe jijini Dar es Salaam.

Mradi huo mkubwa ulianza rasmi Januari, 2015 na unatarajiwa kukamilika ifikapo Desemba, 2018 ikiwa ni miezi 48 tangu kuanza kwa ujenzi, huku ukiwa na ukubwa wa mita za mraba 111,842.90.

Mradi huo ambao ni sehemu ya mji mpya wa kisasa (Satellite City), unabadilisha mandhari ya jiji la Dar es Salaam unarajiwa kugharimu kiasi cha zaidi Sh 187,927,105,500.

NHC inasema mradi huo upo katika eneo tulivu la Kawe ambalo liko mita chache kutoka fukwe za bahari ya Hindi pia karibu karibu na maeneo muhimu kama Mbezi Beach, Masaki, Oysterbay, Morocco na Mikocheni ukiwa na jumla ya nyumba 422 za kuuzwa zilizoko kwenye majengo nane tofauti yenye ghorofa 18 kila moja. Nyumba hizo zina huduma zote muhimu za kijamii ikiwemo maduka makubwa kwa ajili ya wakazi wa nyumba hizo na maeneo jirani.

Kwa mujibu wa taarifa ya NHC, mradi wa Seven Eleven Kawe una nyumba za aina nne; nyumba ya kwanza itakuwa na vyumba viwili vya kawaida ikiwa na jumla ya nyumba 24, nyumba ya pili itakuwa na vyumba vitatu vya kawaida ikiwa na idadi ya nyumba 254.

Aina ya tatu ya nyumba ni ile yenye vyumba vitatu dungu ikiwa na idadi ya nyumba 128 na nyumba ya nne itakuwa na vyumba vinne vya kifahari ikiwa na jumla ya nyumba 16 na hivyo kufanya jumla ya nyumba zote kuwa 422.

Katika mradi huo vyumba vyote vimejitosheleza kwa kuwa na maliwato (en suit), sebule iliyoungana na eneo la kulia chakula, maliwato ya wageni na jiko kubwa la kisasa huku zikiwa na ukubwa wa aina tofauti kutokana na idadi ya vyumba vyake. Ukubwa wake ni mita za mraba 128, 132, 151, 182 na 244.

“Pamoja na hayo mradi huo utakuwa na eneo kubwa la ziada la maegesho ya magari, eneo la michezo ya watoto, viwanja vya michezo mbalimbali kama mpira wa kikapu, tennis, riadha, baiskeli na michezo mingine na eneo maalumu la kukusanyia taka,” imeeleza sehemu ya taarifa ya hiyo ya NHC.

Shirika hilo linasema bei za nyumba katika mradi huo zitaanzia Sh 346,376,625 bila VAT na hivyo litafanya punguzo kwa wateja wake wa mwanzoni (Early Bird) ambao watakaolipa katika muda maalumu huku nyumba 106 ndizo zitakazowekwa sokoni kwa sasa. Nyumba hizi zimelenga watu wenye kipato cha kati na cha juu.

Uzinduzi wa mauzo ya nyumba hizo unaelezwa kuwa mfululizo wa uzinduzi wa miradi ya NHC unaolenga kutimiza malengo ya mkakati wa shirika hilo wa miaka kumi 2015/16 hadi 2024/25.

 

Mradi wa Morocco square

Mkurugenzi Mkuu wa NHC, Mchechu wakati anamkaribisha Rais wa Awamu ya Nne, Dk. Jakaya Mrisho Kikwete kuweka jiwe la msingi kwenye jengo la biashara na makazi la shirika hilo Morocco square jijini Dar es Salaam Oktoba 7, mwaka jana, alisema miradi ya ujenzi wa nyumba unaofanywa na shirika hilo  umewapatia wananchi makazi bora, kupendezesha mandhari za miji yetu, kuongeza wigo wa kodi ya majengo na kodi ya ardhi, kuondoa makazi hafifu katika maeneo husika na kutoa ajira za moja kwa moja kwa wananchi.

Anasema mradi wa Morocco square ulianza Juni 2014 na unatarajiwa kukamilika mwanzoni mwa mwaka 2017 ukiwa mradi mkubwa unaotekelezwa na Mkandarasi ambaye ni Kampuni ya Kitanzania ya Estim Construction Ltd ya Dar es Salaam. Mkandarasi ni Daraja la Kwanza aliyepatikana kwa kushindanishwa kimataifa.

Hadi kukamilika ujenzi wa majengo yote manne ya mradi huu utagharimu kiasi cha shilingi billion 150 ambazo ni mkopo kutoka Benki ya CRDB PLC.

“Mradi huu ambao ni mkubwa kuliko yote Afrika Mashariki una mita za mraba 110,000 zilizo katika msingi mmoja. Kati ya mita hizo, 47,793 ni kwa ajili ya ofisi, 24,924 ni kwa ajili ya makazi na mita za mraba 28, 827 ni kwa ajili ya biashara wakati kumbi za mikutano, maduka makubwa, sehemu za kuchezea watoto na maduka ya vyakula na hoteli ikiwa na ukubwa wa mita za mraba 8,456.

Mradi huu una  uwezo wa kubeba watu 6,000 na kutoa ajira ya zipatazo 24,750 kwa majengo manne tofauti, ikiwemo ghorofa 22 kwa ajili ya nyumba 100 za makazi zenye vyumba vitatu na vinne, ghorofa 20 na 17 kwa ajili ya ofisi na maduka makubwa na  ghorofa 13 kwa ajili ya Hoteli yenye vyumba vya kulala 81,” anaeleza Mkurugenzi huyo.

Mradi huu pia una eneo maalumu la kutua helkopta na eneo kubwa kwa ajili ya maegesho ya magari na baada ya kukamilika kwake utaifanya nchi yetu kuwa na majengo yanayofanana na miji mingine mashuhuri duniani kama Dubai na Manhattan na kuwa kivutio kikubwa kwa wageni mbalimbali kutoka nje ya nchi.

kutokana na eneo hili kuwa na ardhi yenye thamani kubwa, anasema tayari wamejitokeza wanunuzi wa baadhi ya ofisi huku Soko la Hisa la Dar es Salaam wakiwa wamenunua mita za mraba 900 za sehemu ya ofisi katika jengo hilo ili kupanua huduma zake.

Pamoja na umuhimu wa Soko la Hisa katika ukuaji wa uchumi wa Taifa anasema jengo la ofisi walizonunua litaitwa “Exchange Tower” na hivyo kuipa heshima nchi yetu.

Anasema Mashirika mengine makubwa ya kitaifa na kimataifa yamekwishawasilisha maombi ya kununua ofisi katika mradi huo ikiwemo Kampuni ya Delloitte.

Mradi wa Morocco square umelenga watu wa kipato cha kati na juu tu tofauti na miradi mingine inayolenga wananchi wa kada ya chini. Hata hivyo, ubunifu wa mradi huo unakwenda sambamba na upatikanaji wa mahitaji muhimu sehemu moja na hivyo kuwarahisishia wananchi wengi kufika katika majengo hayo kwa urahisi.

Jengo la Morocco Square lipo karibu na kitovu cha Jiji la Dar es Salaam likiwa limezungukwa na ofisi na makazi, hivyo kufikika kwa urahisi na wakazi wote wa jiji hususani wa maeneo ya Mikocheni, Oysterbay, Masaki, katikati ya Jiji, Kinondoni, Kawe na Mlimani City.

“Nichukue fursa hii kuwahamasisha wananchi wanaohitaji sehemu kwa ajili ya ofisi, biashara na nyumba za kuishi wajitokeze kwa wingi kununua na hivyo kuwa wamiliki wa nyumba hizo ili kukuza uchumi na ustawi wa maisha yao,” anasema.

 

Wazungumzia miradi ya NHC

Maendeleo ya Miradi-87Wakazi mbalimbali wa Jiji la Dar es Salaam wamempongeza Mkurugenzi Mkuu wa NHC, Nehemia Mchechu kwa jitihada zake za kuliboresha shirika hilo na kulifanya lijiendeshe kwa faida tofauti na lilivyokuwa awali kwa kutegemea wapangaji pekee ambao wengi wao walikuwa hawalipi kodi za pango kwa wakati.

Sophia Julius (32), mkazi wa Kijitonyama jijini Dar es Salaam amelieleza JAMHURI, kwamba jitihada zinazofanywa na uongozi wa shirika hilo kwa kuibua na kujenga miradi mbalimbali ya nyumba nchini kwa ajili ya makazi, ofisi, maduka na huduma nyingine za kijamii nchini zinapaswa kuigwa na taasisi nyingine kuwaletea Watanzania maendeleo ya kweli yanayoonekana.

“Mchechu ni kiongozi wa mfano ambao unapaswa kuigwa na wengine kama wana nia ya kweli ya kumsaidia kazi Rais John Pombe Magufuli kwani hata kazi zake zinaonekana wazi wazi bila kuwa na wingi wa maneno yaliyokosa vitendo,” anasema Sophia.

Salum Juma (42), mkazi Kimara Baruti, anasema NHC kwa sasa imekuwa na ubunifu mkubwa wenye lengo la kuboresha mandhari ya Jiji la Dar es Salaam na miji mingine nchini kuwapatia wananchi makazi bora.

Juma anasema licha ya jitihada nzuri zinazofanywa na uongozi wa shirika hilo, serikali inapaswa kuondoa changamoto zote zinazojitokeza kwa wananchi wa kipato kidogo waweze kumudu gharama za ununuzi wa nyumba ikiwemo kupunguzwa kwa riba na masharti magumu yanayotolewa na benki zinazotoa mikopo ya nyumba.

Anasema shirika hilo pamoja na jitihada zake kuwapatia wananchi makazi bora, lengo linapaswa kuwanufaisha wananchi wa kipato cha chini kama lilivyokuwa lilipoanzishwa.

“Hawa NHC wanafanya kazi nzuri sana na kubwa. Mchechu anastahili pongezi kubwa sana na miradi hii itakapokamilika kwa wakati mandhari ya jiji itavutia sana,” anasema Juma.

Godson Geofrey (31), mkazi wa Kawe, anasema Shirika hilo limefanya kazi nzuri chini ya uongozi Mchechu, lakini kama hakutakuwa na umakini watajikuta wanauza kila kitu na wao kukosa dhamana yoyote kama umiliki wa ardhi.

Anasema ubunifu wa miradi unaoendelea kufanywa na shirika hilo unapaswa kuungwa mkono na kila mmoja na pia taasisi nyingine zinapaswa kujifunza kutoka NHC, zijiendeshe kwa tija badala ya kutegemea serikali pekee kwa kila kitu.

Hivi karibuni, Mchechu ameliambia JAMHURI kuwa alilazimika kuanza na ujenzi wa nyumba za watu wa kipato cha kati na juu kwa nia ya kukusanya mtaji utakaomsaidia kujenga nyumba za watu wa kipato cha chini.

 Mchechu alisema mikopo ya benki ina riba kubwa, hivyo NHC ikikopa benki kujenga nyumba za wananchi wa kipato cha chini, itajikuta nyumba hizo zinakua bei ghari wanashindwa kuzimudu, ndiyo maana akaamua kuanza na za kipato cha kati na cha juu kisha kuanzia mwakani aanze kujenga nyumba za kipato cha chini baada ya kukusanya fedha.

By Jamhuri