KWA muda wa miezi kadha sasa habari kutoka Marekani zimekuwa zikitawaliwa na kinyang’anyiro cha urais. Wagombea wanaowania tiketi za chama wamekuwa wakipambana na kulumbana huku mashabiki wao wakitiana ngumi na kushikana mashati.

Mgombea mmoja anasema “Ukinichafulia mkutano wangu nami n’tamwaga mboga katika mkutano wako.” Alimradi watazamaji wengi wamekuwa wakichukulia mchakato mzima kama burudani ya aina yake.    

Kinachofanyika kwa sasa ni uchaguzi wa awali (primaries) kuelekea uchaguzi wa urais nchini Marekani Novemba 8, 2016. Wao hufanya uchaguzi wa Rais kila baada ya miaka minne. Katiba yao imeweka kikomo cha mihula miwili, hivyo Rais Barack Obama analazimika kung’atuka na kumpisha mwingine atakayechaguliwa.

Hivyo, huu uchaguzi wa awali ni mchakato wa kumteua mgombea urais kutoka kila chama. Vyama vikuu vinavyojulikana zaidi ni Democrat na Republican. Utaratibu wao wa kuteua wagombea na hata wa kumchagua rais ni tofauti na wa hapa Tanzania. Kwa kweli si wote wanaoelewa utaratibu huu. Sitashangaa hata Wamarekani wenyewe wasipoelewa.

Wao wanadai kuwa wanaongoza dunia katika demokrasi. Lakini cha ajabu ni kuwa mgombea wa chama hateuliwi na wanachama, na Rais hachaguliwi na wananchi moja kwa moja kama tufanyavyo sisi hapa kwetu. Ndio maana wanapofanya uchaguzi basi ubalozi wao hapa jijini huwaita waandishi wa habari kuwaelimisha na wengine hupewa fursa ya kwenda Marekani waandike makala za kuusifu mfumo wao.

Huko Marekani wananchi watawachagua watu watakaomchagua Rais kwa niaba yao. Watachagua kikundi cha wapiga kura (electoral college) ambao ndio watakaopiga kura ya kumchagua Rais.      

Hivi sasa kinachofanyika ni mchakato wa kuwateua wagombea urais ulioanza Februari, Mosi na utakaomalizika Juni 14, mwaka huu. Uteuzi huu unahusu majimbo 50 nchini kote. Watu watapiga kura kuwachagua wajumbe watakaohudhuria mkutano mkuu wa chama (nominating convention) ambao ndio utamchagua mgombea wa urais atakayepeperusha bendera ya chama. Katika hatua hii ya kichama hata Wamarekani walio ughaibuni nao wanashirikishwa

Kwa mfano, Chama cha Republican kitawachagua wajumbe 2,472 watakaohudhuria mkutano mkuu (convention) ambako mgombea urais wa chama atateuliwa. Chama hiki kilianza na wanachama 17 waliotangaza nia ya kugombea tangu Machi, mwaka jana.

Hii ni idadi kubwa ya watia nia ambao haijapata kutokea huko. Wengi wao ni watu wenye nyadhifa wakiwa magavana wa mikoa au maseneta (wabunge). Ila mmoja ni tofauti. Huyu ni Donald Trump ambaye si gavana wala seneta bali ni bilionea kutoka New York ambaye amewekeza hata katika mashariki ya kati. Hiyo ndio sifa yake ambayo imewavutia Wamarekani wengi.

Trump si mwanasiasa kama wagombea wengine. Yeye ni bilionea anayefanya biashara ya kujenga na kuuza majengo, pamoja na kuendesha mahoteli na vituo vya kamari (casino). Anadai kuwa kwa vile amefanikiwa kutajirika basi akiwa Rais atahakikisha wananchi nao wanatajirika. Lakini kisichosemwa ni kuwa kampuni zake zimewahi kufilisika mara nne. Huo si mfano mzuri wa kuigwa!

Wengi wanamuona kama ndumila kuwili, kwa vile aliwahi kujiunga na Democrat. Aliwahi hata kumuwezesha kifedha Hillary Clinton katika kampeni zake mnamo 2008.

Trump pia amewahi kuwaunga mkono wanawake waliokuwa wakidai haki ya kutoa mimba. Sasa anapinga jambo hilo na hata kuishambulia Serikali kwa kuziwezesha asasi za uzazi wa mpango (family planning).

Mwaka 2000 alikuwa akiunga mkono mfumo wa bima ya matibabu kwa wananchi wote ukisimamiwa na serikali. Leo anadai eti huko ni kuingilia uhuru wa raia kujichagulia bima. Yaani anataka makampuni ya bima yaruhusiwe kushindana katika soko huria na kila mmoja ajiamulie kujiunga au kutojiunga bila ya kuingiliwa na Serikali.

Trump amekuwa akichochea chuki na ubaguzi wa kidini dhidi ya Waislamu wanaoishi Marekani kwa kuwaita “wakuja wasio na haki ya kuishi nchini.” Anasahau kuwa Waislamu walianza kuingia Marekani kabla ya babu yake kuhamia huko kutoka Ujerumani. Halafu anasema akiwa Rais Waislamu hawataruhusiwa kuingia Marekani.

Anazishambulia pia China, Mexico na Japan kwa kuzilaumu kampuni zinazowekeza huko badala ya kuwekeza nyumbani. Hawa anawaita wasaliti waliokosa uzalendo. Anasahau kuwa kufanya biashara na nchi hizo na kuwekeza huko ni mwendelezo wa sera ya utandawazi, sera ya kibeberu ambayo ina manufaa kwa mabepari wa kimataifa.

Trump anasema akiwa Rais atawaua watuhumiwa wa ugaidi bila ya kuwafikisha mahakamani. Anasema ataua hata familia zao. Huyu ndiye Rais mtarajiwa wa Marekani na sera zake za kifashisti.

Mpinzani mkuu wa Trump katika chama cha Republican ni Seneta Ted Cruz. Huyu huwa anaelezwa kuwa ni mwenye siasa za wastani. Kinachosahauliwa ni kuwa Cruz naye anaunga mkono mashambulizi zaidi katika mashariki ya kati, pamoja na upunguzaji wa kodi kwa matajiri.

Kwa upande wa Democrat mgombea Seneta, Bernie Sanders amewavutia watu wengi, hasa vijana, kutokana na sera yake anayoiita “usoshalisti wa kidemocrasia”.

Yeye anazungumzia “mapinduzi ya kisiasa” lakini tukiangalia zaidi tunaona kuwa msimamo kama huo hauwezi kukubaliwa asilani na Chama cha Democrat, ambacho siku zote kimekuwa kikitumikia maslahi ya kibepari kikishrikiana na Republican, kwa muda wa miaka 150.

Ni kweli vyama hivyo vinatofautiana, lakini si kimsingi.  Democrat ni cha mrengo wa kulia na Republican ni cha mrengo wa kulia zaidi. Ndio maana hata Sanders akishinda urais itamuwia vigumu kutekeleza ahadi zake. Ni sawa na Rais Obama ambaye kabla ya kuchaguliwa aliahidi kufunga gereza la Guantanamo, lakini jitihada zake zimegonga ukuta.

Hivi sasa tunaambiwa Obama anashindwa kutekeleza ahadi zake kwa sababu bunge (Congress) linatawaliwa na chama cha Republican. Lakini ukweli ni kuwa mwaka 2009 na 2010 bunge lilikuwa na wingi wa Democratic, kina Sanders na wenzake pamoja na Rais wao katika Ikulu ya White House. Hata hivyo, hakuna hatua walizochukua tofauti na Republican. Wakati huo uvamizi wa kijeshi katika mashariki ya kati uliongezeka.

Kuhusu gharama za kampeni, michango mingi ya Hillary ni kutoka makampuni makubwa wakati Sanders anategemea wachangiaji wadogo. Wakati mmoja Hillary alikuwa amekusanya dola milioni 29.4 na Sandera dola milioni 26.2. Fedha za Hillary zilitoka kwa wachangiaji matajiri wachache waliotoa kima kikubwa, wakati Sanders alisaidiwa na watu wengi waliotoa kima cha chini. Hawa ni “walalahoi” 650,000 waliochanga wastani wa dola 30 kila mmoja.

Sanders pia amechangiwa na vyama vya wafanyakazi na vijana wengi wamejitolea kumsaidia katika kampeni zake.  Ndio maana Sanders huwa anajisifu kuwa yeye anawasemea watu wadogo na kumshambulia Hillary kuwa anawakilisha maslahi ya makampuni makubwa.

Yeye anadai kuwa huwa anazungumza na wananchi wengi ambao hulalamika kuwa uchumi wa Marekani umepogoka. Ndio maana unakuta Marekani ambayo ni nchi tajiri pekee duniani isiyokuwa na mfumo wa matibabu bure kwa wote. Sanders anasema hii ni aibu na chini ya utawala wake ataondoa aibu hii ya kuwaachia watu wakifa kwa sababu hawana pesa za kulipia matibabu.

Wakati huo huo, Sanders anakusudia kuongeza mshahara kima cha chini kianzie dola 15 kwa saa. Ameahidi pia elimu bure mpaka ngazi ya chuo kikuu.

Lakini ni Sanders huyu huyu ambaye akiwa katika bunge aliunga mkono mashambulizi ya kijeshi nchini Iraq na Afghanistan.  Katika miaka yake yote alipokuwa mbunge amekuwa akiunga mkono mashambulizi ya Marekani katika nchi kama Somalia, Haiti, Bosnia, Liberia, Zaire, Albania, Sudan, Yugoslavia, Yemen na kadhalika. Hivi karibuni aliitaka serikali ikamate mali zote za Urusi na akaishauri Saudi Arabia iendeleze vita katika nchi za Kiarabu.

Mnamo 2006 alipiga kura kuunga mkono azimio dhidi ya Iran. Pia aliunga mkono uvamizi wa Israel nchini Lebanon. Akaunga mkono kuuwekea vikwazo utawala wa Palestina kwa sababu tu wananchi wake walichagua chama cha Hamas katika uchaguzi wa kidemokrasia. Mwaka 2014, akaunga mkono uvamizi na mauaji ya Israel huko Gaza. Akaunga mkono mpango wa Obama wa kuua raia wa Syria na Iraq kwa kutumia ndege zisizo na rubani. Alipoulizwa akasema akiwa Rais atajaribu asiue raia wengi!

Kuhusu huu uchaguzi, ni vizuri tukaelewa kuwa hakuna mgombea wa urais yeyote wa Marekani anayetarajia kuchaguliwa au aliyechaguliwa, ambaye anaweza kuthubutu kuikosoa Israel. Wana asasi ya kizayuni iitwayo AIPAC ambayo ndio inahakikisha kuwa kila Rais au Rais mtarajiwa anatangaza utii wake kwa Israel.

Ndio maana kabla ya Obama kuchaguliwa kwa muhula wa pili aliiangukia AIPAC. Na ndivyo kina Trump, Hillary na Sanders nao wanatarajiwa kuiangukia AIPAC waruhusiwe kugombea urais.

By Jamhuri