1-mhandisi mkazi(kulia)Dejene na MagufuliKAMATA KAMATA NA MAUAJI HOLELA KISANGIRO

Mwaka jana, Hashim Shaibu Mgwandila, aliteuliwa kuwa Mkuu wa Wilaya ya Ngorongoro na kuahidi kuwasaka wahamiaji haramu popote walipo ndani ya Wilaya ya Ngorongoro.

Alianzisha operesheni ya kuwasaka katika Tarafa ya Loliondo tu na kuacha Tarafa ya Sale. Wakati wa msako huo wahamiaji walimtishia kumpeleka mahakamani. Kwa woga, aliamua kutafuta suluhu ili yaishe. Hatuoni tena juhudi za kuwakamata, kuwashitaki na kuwarejesha makwao wahamiaji hawa haramu.

Sasa wahamiaji wanatembea wakiwa na silaha za kivita mchana kweupe maeneo ya Naan na Burku wakipiga watu risasi ovyo na kuwazuia Watanzania kuingia na kupita kwenye maeneo waliyojitwalia kwa nguvu ya Burku na Horane. Maeneo hayo sasa ni kambi za majangili na maficho ya wahalifu wa kila aina.

Kwa kadhia hizi kila mwaka ni lazima mapigano na mauaji ya wananchi wasiokuwa na hatia yatokee. Februari 21, mwaka huu wananchi watatu wa Kijiji cha Kisangiro ambao ni Timoth Thomas, Ndibedi Mgwero na Kasiserya Yusuph- waliuliwa kwenye boma lao kwa risasi saa tatu usiku. Waliofanya mauaji hayo ni Wamasai wa ukoo wa Loita kutoka Kenya.

Hadi tunakuandikia waraka huu wa wazi kwako Mheshimiwa Rais Magufuli, polisi hawajakamata na kumhoji mtu yeyote ingawa viongozi wa wauaji wana kunywa na kula nao baa ya Maleko, Loliondo. Hii inaendelea kuzidisha hofu kwa wananchi wa Kijiji cha Kisangiro.

Kamati ya Ulinzi na Usalama ilipofika eneo la mauaji waliokota maganda 32 ya risasi na waliwazuia waandishi wa habari kupiga maiti picha. Badala yake walimkamata kwa uonevu Mwenyekiti wa Kijiji cha Kisangiro, Ndugu Zakayo Manaya na kumweka mahabusu kwa siku 17 bila dhamana wala kumpeleka mahakamani. Waliwazuia ndugu zake kumuona. Walipompeleka mahakamani, polisi walipinga dhamana na akapelekwa Magereza kwa siku 14 kwa msingi wa kumkomoa ili aache kutetea ardhi ya wananchi wake.

Mheshimiwa Rais Magufuli, huu ni uonevu wa hali ya juu na hii inasababisha wananchi waichukie Serikali yao. Polisi wanashirikiana na wavamizi wa ardhi yetu kujenga mtandao hatari kwa usalama wa nchi yetu kwani hata uwape taarifa za namna gani zinazowahusu wahamiaji hawa, hawachukui hatua na wakichukua hatua makosa hugeuzwa upande wa Watanzania. Huu ni ukoloni katika eneo la Loliondo.

 

AINA YA MIGOGORO YA ARDHI NA VYANZO VYAKE NGORONGORO

Mheshimiwa Rais, Wilaya ya Ngorongoro kuna aina nyingi za migogoro ya ardhi. Kuna mgogoro wa ardhi kati ya Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro (NCAA) na wananchi wa Tarafa ya Ngorongoro wanaodai kuruhusiwa kulima kilimo cha kujikimu; kuna mgogoro kati ya wananchi, Hifadhi ya Taifa ya Serengeti (SENAPA) na kampuni za wawekezaji wa utalii; na wahamiaji haramu Tarafa ya Loliondo -hasa vijiji vya Ololosokwan, Oloipir, Soit sambu, Enguserosambu; kuna mgogoro kati ya wananchi na wahamiaji haramu kutoka Kenya tarafa ya Sale hasa vijiji vya Kisangiro, Oldonyosambu, Tinaga, Yasimdito, Digodigo, Sale, Pinyinyi, Mageri, Magaiduru na kuna migogoro ya ardhi kati ya kijiji na kijiji.

Mheshimiwa Rais Magufuli, chanzo cha tatizo ndiyo tatizo lenyewe. Vyanzo vya migogoro ya ardhi ni vingi kutegemeana na aina ya mgogoro, lakini vyanzo vinavyojulikana ni ongezeko la idadi ya watu wakati ardhi ni ile ile; wingi wa utajiri wa rasilimali za asili uliopo Ngorongoro unaomezewa mate na waroho wa utajiri wa chapuchapu; mtandao mpana wa ufisadi na rushwa kubwa ulioandaliwa na wahamiaji haramu kwa wakubwa wenye dhamana na mamlaka za uongozi Loliondo; NGOs, polisi kujigeuza- maofisa Ardhi, Mifugo, Misitu, Wanyamapori, Uhamiaji, Mahakama, n.k. Polisi Loliondo ni kila kitu, viongozi wa wilaya kufanya kazi kwa mazoea na kujigeuza miungu-watu n.k.

Viongozi wenye mamlaka wanapohamishwa Loliondo na kuletwa wengine; miongoni mwa makabidhiano ni makabidhiano ya wahamiaji haramu waliovamia Kijiji cha Kisangiro kwamba hapo ndipo penye fedha za bure za kuchukua kiulaini. Hapo ndipo lilipo shamba la bibi! Ofisa Uhamiaji mmoja ambaye sasa kahamishiwa Arusha, alipokea fedha nyingi sana kutoka kwa wahamiaji hawa Wakenya.

Wananchi, madiwani na mbunge wanakiri kwamba mapigano ya sasa chanzo chake ni wahamiaji haramu kuvamia ardhi ya Kijiji cha Kisangiro kinyume cha sheria, lakini cha kushangaza mteule wako- Mkuu wa Wilaya na Jeshi la Polisi wanapinga ukweli huu. Wananchi wanajiuliza nia na malengo ya taarifa za intelejensia ya polisi wetu kupinga na kupotosha ukweli bila kueleza chanzo chao cha mauaji.

 

UANZISHWAJI HOLELA WA VITONGOJI, VIJIJI NA KATA NGORONGORO

Mheshimiwa Rais Magufuli, tangu Wilaya ya Ngorongoro ianzishwe mwaka 1979 yenye wakazi 174,328 na sasa kata 28 ugawaji na uanzishwaji wa vitongoji, vijiji na kata huanzishwa bila kufuata taratibu na sheria za Serikali za Mitaa. Wananchi katika vijijiji vinavyogawanywa au kuanzishwa hawashirikishwi; hakuna majadiliano huru ya ugawaji na uanzishwaji wa vitongoji, vijiji na kata mpya (public hiring meeting). Badala yake huanzishwa kwa siri kukidhi matakwa ya kabila la Wamaasai ili wawe na kata nyingi na kiuamuzi kukidhi haja ya kuwalinda wahamiaji, NGOs na kampuni za kitalii, lakini kiuhalisia siyo halali na hii kuiongezea Serikali gharama za uendeshaji. Mfano ni uanzishaji wa vijiji vya Mundorosi, Naan, Olopir, Masusu Maloni n.k. Kwa kuwa TAMISEMI sasa ipo chini ya ofisi yako, Mheshimiwa Rais tafadhali chukua hatua stahiki.

 

ASASI ZA KIRAIA LOLIONDO

Mheshimiwa Rais, sehemu ndogo ya Loliondo pekee kuna asasi za kiraia 31 zilizoanzishwa na Watanzania pamoja na wahamiaji haramu ndani ya kampuni za uwindaji wa kitalii kupitia Wildlife Management Authority (WMA) kwa mgongo wa kuwatetea wafugaji, yanayofadhiliwa na kampuni za uwekezaji wa nchi za Magharibi kwa lengo la kuwatetea wahamiaji na kampuni zao za uwindaji kutoka Kenya zenye vinasaba na Wazungu na kumpiga vita Mwarabu wa Ortello Business Company Limited (OBC).

Kila kampuni ya uwekezaji wa kitalii Loliondo ina azaki yake binafsi kwa msingi wa kuitetea na kupinga mipango ya maendeleo ya Serikali [azaki hizi ziliwahi kupinga ujenzi wa barabara ya lami ya Mto wa Mbu-Makutano wakati Maasai Mara kuna lami.

Walipinga kugawanywa kwa Pori Tengefu la Loliondo, walindai Babu wa Samunge (Ambilike Mwaisapile) yupo Kusini mwa Kenya; walidai Olduvai Gorge ipo Kenya; wanadai Mlima Kilimanjaro upo Kenya; wanataka mpaka wa Bologonja ufunguliwe nk.]

NGOs hizi ndizo zenye uamuzi wakati wa uchaguzi mbalimbali kwa kuwachagulia wananchi viongozi. Pia ndizo huwatafutia wahamiaji haramu ardhi, huandaa, hufadhili na hugharimia mapigano ya makabila. Hivyo, Mheshimiwa Rais Magufuli hili ni jipu lililoiva miaka mingi iliyopita. Tunakuomba ulitumbue. Ili kulinda na kuhifadhi Pori Tengefu la Loliondo, tekeleza mpango wa kugawa kilometa za mraba 4,500 kwa vijiji. Na Idara ya Wanyamapori wamiliki kilometa za mraba 1,500 kwa manufaa ya mazalia ya wanyamapori, ushoroba na vyanzo vya maji.

 

MADHARA YA WAHAMIAJI HARAMU TOKA KENYA

Kimsingi madhara yanayosababishwa na wahamiaji haramu kwa ngazi ya kijiji chetu, kata, wilaya na hata Taifa ni makubwa mno. Wageni hawa wamevamia kwa nguvu ardhi ya Kijiji cha Kisangiro kinyume cha uamuzi wa Serikali uliotolewa na Waziri wa Ardhi, Nyumba ya Maendeleo ya Makazi, Profesa Tibaijuka mnano Machi 23, 2013.

*Kutwaa kwa nguvu mashamba ya wananchi wa Kijiji cha Kisangiro na kuyalima wao na mazao kuuzwa Kenya.

*Kuendesha mauaji ya kikatili kwa Watanzania katika Kijiji cha Kisangiro bila wauaji kukamatwa na kufikishwa kwenye vyombo vya sheria- kisa rushwa.

*Kusababisha athari za kiulinzi na kiusalama hivyo kusababisha kijiji hadi wilaya isitawalike.

*Viongozi wetu wa Serikali ya Kijiji kukamatwa ovyo, kuteswa na Jeshi la Polisi kuwabambikiwa kesi ili kuwatisha ili wasitetee ardhi halali ya wananchi wa kijiji chetu.

*Kuchomwa moto makazi, mazao na mali mbalimbali za wananchi na kuwasababishia mateso makubwa.

*Kwa sababu ya uhaba wa ardhi nchini Kenya na kwa sababu wanajua umuhimu wa ardhi, wahamiaji hawa kwa kutumia rushwa na ufisadi wamemilikishwa ardhi kubwa maeneo mengi ya tarafa za Loliondo na Sale huku wakijua ni kinyume cha sheria mgeni kumiliki ardhi.

Pia wanaharibu mazingira kwenye Pori Tengefu Loliondo kwa kuendesha shughuli za kilimo.

*Kimkakati na maelekezo maalumu kutoka nchini kwao, sasa wanaingiza makundi makubwa ya mifugo ndani ya SENAPA ili wanyama na watalii wahamie Maasai Mara; na Tanzania tukose mapato ya utalii.

*Makundi makubwa ya mifugo ya hawa wahamiaji haramu hulishwa nyasi na maji ya Tanzania na kutusababishia jangwa, hutuletea magonjwa ya mifugo, lakini wanaofaidi kodi na mazao ya mifugo hiyo ni Kenya maana huuzwa kwenye minada yao na halmashauri kutoingiza mapato yoyote.

*Huendesha uwindaji haramu wa wanyamapori, hasa tembo katika SENAPA na Pori Tengefu la Loliondo, upasuaji na usafirishaji haramu wa magogo na mbao kutoka misitu yetu ya hifadhi.

*Wahamiaji hawa pia hufaidi huduma mbalimbali za kijamii kama matibabu, maji, barabara, majosho n.k; hivyo kusababisha athari za kiuchumi.

Wahamiaji hawa kwa kushirikiana na asasi za kiraia wamejiingiza  kwenye nafasi mbalimbali za uongozi wa Halmashauri ili kufanikisha malengo yao pia asasi za kiraia zinaendesha siasa za majitaka kwa kuwachagulia wananchi wenyeviti wa vijiji na vitongoji, madiwani na hata mbunge [lakini safari hii mbunge wao alishindwa] ili kufanikisha malengo yao.

 

MAPENDEKEZO NA USHAURI

Mheshimiwa Rais Magufuli, ili kuipatia suluhu ya kudumu migogoro ya ardhi katika Wilaya ya Ngorongoro baina ya jamii za Wasonjo na Wamaasai ambayo imesababisha hasara kubwa ya mali na kugharimu maisha ya watu wengi na kurudisha nyuma kasi ya maendeleo; tunapendekeza yafuatayo yafanyike:

1: Mipaka ya asili ya Vijiji, Kata na Tarafa ya Sale na Loliondo iheshimiwe. Iwekewe (alama) beacons na vijiji vipewe hati miliki. Kwa kuwa mgogoro huu ulishamalizika kwa pande zote kuridhia uamuzi wa Serikali, tunaomba Serikali yetu Tukufu iweke beacons kwenye mipaka iliyokubaliwa; na iwachukulie hatua za kisheria wote wanachochea na kupalilia kuzuka upya kwa migogoro ya ardhi iliyokwishasuluhishwa.

2: Serikali idhibiti tabia ya wahamiaji haramu kuhama na mipaka ya nchi waliyotoka na kuiunganisha na vijiji au kata walizokaribishwa kwa kulinda mipaka ya nchi yetu na kuwadhibiti wahamiaji haramu kutoka Kenya ambao kwa sehemu kubwa ndiyo chanzo kikuu cha migogoro isiyoisha ya ardhi wilayani Ngorongoro na wanahatarisha usalama na amani ya nchi yetu.

3: Serikali iunde tume huru ya wataalamu na shirikishi kuchunguza ukweli na kubaini vyanzo vya kujirudia rudia kwa migogoro ya ardhi kwa nia ya kupata ufumbuzi wa haki na wa kudumu.

4: Serikali ianzishe operesheni za mara kwa mara za kijeshi  zikiongozwa na Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) kwa kushirikiana na Uhamiaji; na si Jeshi la Polisi ili kudhibiti kujirudia rudia kwa migogoro ya ardhi Kijiji cha Kisangiro.

5: Watendaji wote wa Serikali wasio waaminifu, wala rushwa, wachochezi na wasiojali maslahi ya wananchi wao wala sheria na kanuni za uongozi bora wachukuliwe hatua za kinidhamu na kisheria. Ni vema polisi wote wa vituo vya Loliondo, Ololosogwan/Oloipir, Samunge na Jema wakatumbuliwa! Pia taasisi za umma kama TAKUKURU, Usalama wa Taifa, Uhamiaji, Ardhi, Mkurugenzi wa Halmashauri wachunguzwe kwani hazitimizi majukumu yao ipasavyo.

6: Serikali ichunguze mienendo na kazi za NGOs zilizojazana Loliondo kwa kisingizio cha kuwatetea wafugaji maskini na kujiridhisha na shughuli zao maana asasi hizi zipo nyuma ya migogoro ya ardhi wilayani Ngorongoro.

7: Tunapendekeza Ngorongoro iongozwe na Mkuu wa Wilaya mwanajeshi mwenye cheo cha kuanzia Kanali. Tunaamini wanajeshi ni waaminifu, wazalendo na ndiyo pekee wenye uwezo wa kukataa rushwa, ufisadi na kupambana na wahamiaji haramu.

8: Wilaya hii ni kubwa  mno. Tunashauri iwe na majimbo mawili ya uchaguzi au ziundwe halmashauri mbili. Pia uanzishwe mkoa  maalumu wa kipolisi ili kudhibiti uhalifu na uhujumu uchumi unaofanywa kwa makusudi na baadhi ya makundi kwa maslahi yao binafsi.

9: Mheshimiwa Rais, wilaya hii ina matatizo mengi sana, haina majengo ya mahakama, hospitali ya wilaya, maji safi na salama, miundombinu ya barabara na unakumbuka ulipokuja  kunywa kikombe cha Babu wa Samunge ulituahidi ka-barabara ka-lami kutoka Kigongoni-Selela-Engaruka-Ngarasero-Digodigo-Loliondo-Mugumu-Makao-Nata ya wastani wa kilometa 450.

Mheshimiwa Rais, kwa asili, Serikali ya Loliondo hufanya kazi kwa mazoea. Haina utamaduni wa kutekeleza uamuzi wala maagizo ya Serikali ngazi za juu bila ufuatiliaji. Mfano ni kushindwa kutekeleza kwa makusudi uamuzi wa Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi uliotolewa Machi 23, 2013. Hapana budi hatua za kinidhamu zichukuliwe dhidi ya wahusika wote.

Mwisho, tunakushukuru tena na tuna imani nafasi ya urais uliyonayo imepata mtu sahihi. Tunajua una dhima nyingi za kitaifa na kimataifa, lakini tunakusihi na kukuomba utumie mamlaka yako, hekima na busara zako kuzifanyia kazi kero zetu zote mapema kwa kuwatuma mawaziri wako kwa maana wananchi wako tunateswa ndani ya Tanzania huru kwa kunyang’anywa ardhi yetu na mauaji ya mara kwa mara yanayotekelezwa na wahamiaji haramu kutoka Kenya.

Mungu akubariki sana Mheshimiwa Rais Dk. John Pombe Magufuli, uliye mwanga na tumaini kubwa la Watanzania wanyonge.

 

Wananchi,

Kijiji cha Kisangiro, Ngorongoro.

Majina ya wananchi walioandika barua hii tumeyahifadhi kwa usalama wao.

5294 Total Views 2 Views Today
||||| 5 I Like It! |||||
Sambaza!