Unaweza usiamini, lakini huu ndio ukweli wenyewe. Tazama hizi picha mbili kwa makini. Nilipoziweka kwenye mitandao ya kijamii, wapo walionitaka niache ‘mzaha’, wakidhani picha na maelezo nilivyoweka vilikuwa vya kuchangamsha baraza!

Picha hizi ni za vituo viwili tofauti vinavyotumiwa na Halmashauri mbili za Monduli na Longido mkoani Arusha, kukusanya ushuru kutoka kwa watalii wa kigeni wanaomiminika nchini mwetu kushuhudia maajabu ya neema tulizojaliwa na Mwenyezi Mungu.

Picha ya kwanza ya kibanda kilichosimama kwa msaada wa nguzo mbili, ndio Ofisi ya Ukusanyaji Ushuru iliyopo eneo la Geti la ‘Longido’. Hapa ni kwenye tambarare ya mlima mzuri na wa kipekee hapa nchini, Mlima Oldonyo Lengai. Mlima huu ndio wenye volkano iliyo hai, na kwa sababu hiyo kuna wakati ‘unakasirika’ na kutoa lava! Mara kadhaa wakazi wa Kijiji cha Engaresero, kilicho jirani- wamekabiliwa na hatari ya volkano. Wamegoma kuhama. Pengine ni kutokana na sababu za kiuchumi katika eneo hili lenye utajiri mkubwa.

Katika mlango wa kibanda hiki, kuna maandishi haya: “GETI YA USHURU, LIPA HAPA”.

Picha ya pili ni ya kibanda ambacho kwa bahati mbaya hakina japo ukuta. Hiki kipo katika Kijiji cha Engaruka, Monduli.

Ndugu zangu, mabanda haya mabovu yanatumiwa na wilaya za Monduli na Longido kukusanya ushuru wa dola 10 za Marekani (Sh zaidi ya 20,000) kutoka kwa kila gari lenye watalii linalopita sehemu hizi.

Wageni wengi wanapita eneo hili kwa ajili ya kufaidi vivutio vya utalii vya Mlima Oldonyo Lengai, maporomoko ya maji, Ziwa Natron, Shimo la Mungu, mandhari nzuri ya Bonde la Ufa, wanyama, ndege na vivutio vingine vingi. Hili Shimo la Mungu, halijatangazwa kabisa. Ni shimo lenye kina kirefu na upana wa kustaajabisha. Profesa Jumanne Maghembe-Waziri wa Maliasili na Utalii- sina hakika kama analikumbuka.

Kilichofanywa na halmashauri hizi ni kuhakikisha kuwa malipo yanafanywa kwa dola za Marekani, na si shilingi. Hili nalo ni tatizo. Watu waliowekwa hapa wanafanya kazi hiyo ili baadaye mapato yaingie katika halmashauri hizo. Sina hakika na hilo la mapato kufika kulikokusudiwa.

Ndugu zangu, si lengo langu kuwashitaki viongozi katika halmashauri hizi wala Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro au Wizara ya Maliasili na Utalii. Naandika haya ikiwa ni changamoto ya kutufikirisha Watanzania kama kuna kitu tulimkosea Mungu hata akaweza kutunyima utashi wa kutambua na kurekebisha mambo madogo kama haya.

Mahali ambako ni chanzo cha mapato kutoka kwa watalii, ni aibu kuwa katika hali hii. Natambua wapo wanaoweza kudhihaki udhaifu huu kwa kusema vibanda hivyo ni sehemu ya “vivutio vya utalii”, lakini ni wazi kwamba hata hao watalii wanatushangaa kweli kweli.

Mgeni anatoka Ulaya, Marekani, Japan, China, Russia au kwingineko duniani, anakuja Tanzania, anakuta hii ndiyo sehemu anayotakiwa ‘kutupa’ pesa alizohangaikia miaka mingi ili aweze kuja kutalii! Huu ni mzaha mkubwa. Hao watalii watarejea nchini mwao wakiwa wanatuweka kwenye kundi gani? Fikiria, hii ndiyo benki, utakuwa na imani nayo?

Nimezungumza na Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Monduli, Ole Nguyaine, kuhusu jambo hili katika eneo lake la utawala la Engaruka.

Anakiri kuwa kweli eneo hilo lipo kwake na ni miongoni mwa vyanzo vya mapato vya halmashauri yake.

Nimemwuliza kama anaijua aibu hii, na yeye amejibu haya:“Hiyo (ubovu wa kibanda cha kukusanyia mapato) ni moja ya changamoto zinazotukabili katika halmashauri yetu ambazo inabidi zitatuliwe.

“Nimefika katika halmashauri hii Oktoba, mwaka jana (2015), kwa kweli sijapita eneo hilo maana ni mgeni bado.”

Nisingependa kuingia kwenye mjadala kutokana na majibu haya, lakini kama kwa miezi zaidi ya mitano ya kuwapo kwake Monduli hajapita eneo lake ambalo kunakusanywa dola, basi wasomaji wanaweza kujua aina ya watendaji tulionao.

Majibu haya yakanifanya nisiwe na shauku ya kuzungumza na Mkurugenzi mwenzake wa Longido. Ukiacha vibanda vibovu, maeneo haya yanayopaswa yawe vituo vya mapumziko mafupi, hayana huduma yoyote iwayo ya kumfaa binadamu. Hakuna sehemu ya kujisaidia au hata kunawa. Ikumbukwe wageni wengi hawajazoea vumbi kwa hiyo huhitaji huduma za kunawa uso.

Lakini jambo jingine la kuhoji ni hili la kuwapo vituo vinne vya ukaguzi watalii -kuanzia Mto wa Mbu hadi Engaresero. Kuna sababu gani ya kuwa na utitiri huu? Kwanini vituo vitatu (Mto wa Mbu, Engaruka na Geti la Longido) visiwe na sehemu moja ya kukusanya, kisha mapato yakaganywa kwa mamlaka husika kwa uwiano? Kwanini wageni wapoteze muda kwa kukaguliwa kila baada ya kilometa kadhaa?

Kero hii ya vizuizi nchini Tanzania si tu kwamba ipo kwenye mizani, bali kila mahali hata maeneo kama haya wanamopita watalii.

Ndugu zangu, nimeona niyaseme haya kwa sababu vibanda hivi ni aibu kubwa kwa Serikali na Watanzania. Tunaonekana kituko machoni mwa wageni. Kama tunashindwa kuthamini mahali panapotuingizia fedha, ni kwanini kina Trump wasipendekeze Afrika itawaliwe kwa mara nyingine? Hivi hili nalo linahitaji mfadhili kama ile aibu tuliyoipata ya Japan kutujengea lango la Ngorongoro ilhali mabilioni yakiishia mifukoni kwa watumishi kadhaa?

Mwonekano wa vibanda hivi unaashiria nini kama si ukweli kwamba kinachokusanywa hapo kinaishia mifukoni mwa wezi waliojaa katika halmashauri zetu? Nani anaweza kusimama kututhibitishia kuwa dola kwenye vibanda hivi vibovu zinawasilishwa kulikosudiwa?

Wakati mwingine inakuwa vigumu kuamini mambo yanavyotendwa katika nchi hii hata kufikia hatua ya kuuliza, tumemkosea nini Mungu wetu? Maeneo haya yanahitaji mabadiliko ya haraka ili kuifuta aibu hii.

By Jamhuri