Uchaguzi Mkuu wa marudio wa Zanzibar Machi 20, mwezi huu, umepita salama salimini na mgombea urais aliyeshinda ametangazwa na kuapishwa rasmi kuwa Rais wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, ambaye ni Dk. Ali Mohamed Shein kutoka  Chama Cha Mapinduzi (CCM).

Ni ukweli uchaguzi umepita salama salimini, lakini umeacha maneno na simulizi ambazo kamwe hazitapita kama moshi hewani kwa sababu mwenendo wa uchaguzi ulizaa makundi mawili yaliyohasimiana – washiriki na watazamaji wa marudio ya uchaguzi.

Washiriki wa uchaguzi wana simulizi zao kwa jamii jinsi walivyojiandaa, walivyopiga kura na walivyosherehekea matokeo ya upigaji kura. Ni yumkini furaha nyusoni mwao na vicheko ndani ya pumzi zao. Furaha hiyo imeonekana hadharani na itaelezwa kwa vizazi na vizazi vijavyo.

Watazamaji au waangalizi nao wana simulizi zao namna walivyojipanga kukataa kushiriki uchaguzi ule kwa madai ni uchaguzi batili na haramu. Mwenendo na matokeo ya uchaguzi umefanya nyuso za watu hao kuwa zenye huzuni na mioyo kupata taharuki. Hivi kweli wenzetu wamefanya uchaguzi pasi na sisi kushiriki?

Makundi mawili hayo kila moja lina sababu zake na hatimaye kuonesha jamii ya Watanzania taswira tofauti. Wote hao ni jamii moja iliyojaa wazawa wa visiwa vya Unguja na Pemba. Wamefikia katika tofauti hiyo kutokana na walivyopokea maana na tafsiri ya dhana ‘demokrasia na misingi ya haki za binadamu’.

Tofauti hiyo imekolezwa nguvu na masahibu wa ndani na nje wa visiwa hivyo. Mfano wa mhunzi anayechochea moto ili chuma kiwe laini na chepesi akipinde katika mkunjo wowote autakao. Hata kama hakuna ushahidi wa kisheria kuthibitisha yaliyotokea Zanzibar, kauli na tuhuma zilizopo za kisiasa zimepevusha tofauti hiyo.

Baadhi ya viongozi wa kisiasa barani Afrika mara kwa mara wanasahau dhana demokrasia iliyoletwa na waghaibuni inavyoichezea Afrika mithili ya mfua chuma. Hivi hawafahamu kuwa demokrasia si moja katika utekelezaji wake duniani?

Hiki chambo ‘haki za binadamu’ kinachowekwa kwenye ndoano na mshipi wake kurushwa Afrika kuopoa Waafrika na mali zao bado hawajakimaizi? Chambo hiki kilichimbuliwa tangu mwaka 1948 na Baraza la Wadhamini la Umoja wa Mataifa (sasa ni Umoja wa Mataifa) hakikutumika hadi mwishoni mwa karne ya 20 baada ya nchi zote za Afrika kuwa huru. Hasa ujio wa vyama vingi vya siasa (kwa Tanzania mwaka 1992) kwa nini iwe hivyo?

Hao waliobuni na kuleta demokrasia Afrika, huko kwao demokrasia si moja. Wala hawaing’ang’anii kama ruba na mguu wa binadamu. Hicho chambo ‘haki za binadamu’ ndiyo kabisa hawakitilii maanani. Wamesahau na hata kupuuza haki aliyopewa binadamu na Mwenyezi Mungu wake. Vipi Waafrika tusitafakari hilo?

Leo, baadhi ya Waafrika katika nchi fulani fulani hawana raha, amani na uhakika wa maisha yao kwa sababu ya demokrasia na haki za binadamu. Baadhi ya viongozi wao wamekubali kuvuliwa kama samaki na kukaririshwa demokrasia ya ughaibuni iliyorembeshwa kwa nje upendo na haki ilhali ndani ina chuki, vita, dhuluma na uporaji wa rasilimali za Afrika.

Cha ajabu, demokrasia hiyo hukolezwa na kupewa mapambio ya aina aina wakati wa kipindi cha uchaguzi mkuu wa nchi yoyote Afrika. Katika kipindi hicho, vikundi vya harakati vya kutoa elimu ya demokrasia na utawala bora hufumuka mithili ya nyuki kutoka kwenye mzinga na kuhamasisha vijana, wananchi na hata baadhi ya wasomi; ambao hupeleka akili zao likizoni na kushabikia uvundo huo. Waafrika lini tutaamka? Tutafakari.

Ninapoangalia mvutano wa kidemokrasia ndani ya Zanzibar, ukweli haukuanza leo au jana. Umeanza tangu zama za usultani ukiwa na sura na tabaka za kijamii. Hata chaguzi za miaka ya harakati za kupigania uhuru wa Zanzibar zilikuwa za mizengwe mizengwe (1957-1963). Simulizi zake ni ndefu. Hapa hapatoshi. Wazanzibari mnajua hilo.

Ndiyo maana hadi sasa, pamoja na mapinduzi kufanyika Januari 12, 1964 wapo Wazanzibari wanaokubali mapinduzi hayo na wapo wanaoyakataa. Huo ni mgogoro. Sijui ni lini Wazanzibari wataimba wimbo mmoja! Ewe Mwenyezi Mungu wape wepesi na wajaalie waja wako hao wawe na kauli moja na kudumisha Zanzibar yenye utulivu na amani. Amin.

Chama kikuu cha upinzani – Chama cha Wananchi (CUF) miaka mitano iliyopita kilifanya uamuzi wa busara wa kukubaliana na chama tawala – Chama Cha Mapinduzi (CCM) kuunda Serikali ya Umoja wa Kitaifa (SUK). Waumini na wapenda demokrasia ya kweli duniani walifurahishwa na kuunga mkono uamuzi huo na kuipa CUF na CCM utukufu mkubwa.

Katika kipindi cha 2010-2015 watu wenye macho, hekima na busara wameshuhudia maendeleo mazuri yakiendeshwa na kusimamiwa pamoja baina ya CUF na CCM kwa minajili ya wazawa wa Unguja na Pemba. Huduma bora za jamii zilitolewa kwa haki. Uboreshaji na upanuzi wa miundombinu ya kijamii na kiuchumi imejengwa. Pato na uchumi wa kitaifa umekua. Kila Mzanzibari amejaa furaha, huba na mahaba kwa mwenzake.

Toba ya Rabbii. Tupo salama. Nini kilitokea Oktoba 25, mwaka jana viongozi wa CUF, CCM na ZEC wanajua undani wake. Wewe na mimi hatujui. Nasema hatujui. Narudia hatujui. Tumepokea tu kauli za viongozi wa jumuiya hizo za kuwataka Wazanzibari washiriki na wasishiriki Uchaguzi Mkuu wa marudio wa Zanzibar, Machi 20, mwaka huu. Uamuzi wa viongozi hao umewagawa wananchi katika makundi mawili ya ‘sisi na wao’.

Mgawanyiko huu si mzuri. Haujengi bali unabomoa umoja wa kitaifa uliodumu miaka mitano, lakini umependwa na kukubalika. Hiyo ndiyo haja ya msingi. Hata kama uchaguzi wa Machi 20 umepita, wananchi na wanachama wa CUF, CCM na vyama vingine vya siasa hawajapita na hawatapita. Nawaomba warudi kwenye mazungumzo wajenge Zanzibar yenye nuru.

Hamaki haijengi, gahamu haishibishi na ubabe hauzai tamu. Tumemsikia Rais wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar Awamu ya Saba, Dkt. Ali Mohamed Shein, alipoapishwa Alhamisi iliyopita (24/3/2016) Uwanja wa Amaan, Zanzibar akiahidi kuunda serikali makini yenye kutenda haki bila kujali itikadi za kisiasa. Wazanzibari mkubali hayo yaishe lau kama macho yanacheka na moyo unalia. Kwaheri.

1534 Total Views 2 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!