Mgogoro ulioibuka kati ya kampuni ya Wingert Windrose Safaris (Tanzania) Ltd (WWS) na Green Mile Safari Company Ltd (GM) unazidi kuibua maswali mengi baada ya kubainika kuwapo kwa mchezo mchafu ndani ya Wizara ya Maliasili na Utalii.

Mchezo huo mchafu umebainika kutokana na kughushiwa kwa ramani halali iliyotolewa kabla ya mwaka 2011 kwa lengo la kuwabeba wamiliki wa kampuni ya Green Mile Safari Company Ltd.

Bila kufuata taratibu, baadhi ya maofisa wa Wizara ya Maliasili na Utalii kwa nia ovu ya kumpotosha Waziri, walianza mbinu za kubadili ramani ya vitalu katika eneo la Ziwa Natron kwa nia ya kubadili jina la kitalu cha GM kutoka Lake Natron Game Control Area (GCA) North kwenda Lake Natron GCA East kwa kubadili ramani rasmi kuhalalisha nia yao hiyo.

 

Historia

Mnamo Septemba 6, 2011 Wizara iligawa vitalu na kuipatia kampuni ya Green Mile kitalu Lake Natron GCA North, na siku hiyo hiyo (Septemba 6, 2011) wakaigawia Wingert Windrose Safaris kitalu kiitwacho Lake Natron GCA North South.

Wizara ya Maliasili na Utalii, Februari, 2012 ilitangaza mgawanyo wa vitalu hivyo na kuonesha kwamba Wingert Windrose Safaris wamepewa vitalu vya Moyowosi GR (S) na Lake Natron GCA (N. South) wakati Green Miles Co. Ltd waligawiwa Selous GR MK1 na Lake Natron GCA North.

Tangazo hilo lilitolewa hadharani katika Maonesho ya Uwindaji ya Safari Club International (SCI) Hunting Show, Las Vegas, Marekani; ambalo pia liliambatana na taarifa ya aliyekuwa Waziri wa Maliasili na Utalii, Ezekiel Maige; tangazo ambalo haliwezi kubadilishwa na Mkurugenzi wa Wanyamapori pekee.

Ilipofika Januari 3, 2013, takriban miezi 16 baada ya mgawanyo wa vitalu kufanyika, Wingert Windrose Safaris ikakuta kipeperushi cha Green Miles katika kongamano la uwindaji la Dallas Safari Club, lililofanyika Dallas, Marekani. Mkurugenzi Mtendaji wa Green Miles, Salum Awadh, alihudhuria kongamano hilo kama mgeni na si mshiriki, lakini alikuwa akigawa vipeperushi kwa wageni kutafuta biashara.

Katika vipeperushi hivyo alivyokuwa akigawa Salum Awadh wa Green Miles, kulikuwa na ramani inayonesha kuwa kitalu cha Wingert Windrose Safaris cha North South, lakini sasa kimepewa jina la Lake Natron GCA East, bila hata ya kuwapo mchakato wa kisheria wa kugawa upya ama kutangazwa kwa zabuni ya kugawa upya.

Maofisa wa Wingert Windrose Safaris walimkabili Salum Awadh katika kongamano hilo na kuhoji kuhusu ramani iliyopo katika vipeperushi vyake na akatoa jibu la kushitusha kwamba “Green Mile wamepata barua kutoka kwa Waziri wakijulishwa kwamba jina la kitalu walichogawiwa Green Mile cha Lake Natron GCA North limebadilishwa na kuitwa Lake Natron GCA East”. 

Hakuweza kutoa ushahidi wowote wakati huo. Hata hivyo, Wingert Windrose Safaris inaendelea kusisitiza kwamba, mabadiliko ya majina ya vitalu hayawezi kubadili eneo kilipo kitalu, hata kingeitwa ‘Juma’ au ‘John’.

Ilibainika baadaye kwamba Green Miles walipewa barua na Mkurugenzi wa Wanyamapori Januari 7, 2013, siku chache baada ya Mkurugenzi Mtendaji wa Green Miles Salum Awadh kudai kwamba wamepewa barua na Wizara alipokuwa katika kongamano la uwindaji, Dallas Marekani.

Awali, hadi Januari 2013 kulikuwa na juhudi za kutaka kupatiwa ramani rasmi na Wizara, Wingert Windrose Safaris iligonga mwamba kupatiwa ramani ya kitalu chao cha Lake Natron GCA North South walichogawiwa Septemba 6, 2011. Ramani za vitalu vyote vya Wingert Windrose Safaris zilipatikana kutoka wizarani isipokuwa kile cha eneo la Lake Natron.

Maelezo ya utata wa Green Miles kujua uwepo wa barua hata kabla haijaandikwa na kuwa na ramani kabla hata ya kutolewa rasmi, kunayapa uzito madai ya Wingert Windrose Safaris kwamba kulikuwa na hila na nia ovu dhidi yao, na ndiyo sababu hasa ya kutotolewa kwa ramani rasmi kwa wakati ili kutoa nafasi kwa maofisa waovu wa wizara kughushi ramani halisi kuwabeba Green Miles.

Hata barua yenyewe ya Januari 7, 2013 iliyosainiwa na Profesa Jafari Kideghesho, ilikiri kuwa Green Miles walipewa kitalu kiitwacho Lake Natron GCA North, lakini barua hiyo ikaeleza kwamba jina hilo lilikosewa kutokana na jiografia ya eneo hilo na hivyo wizara imo katika mchakato wa kubadili jina la eneo hilo na kuwa Lake Natron GCA East na kwamba Waziri angeandika barua kujulisha kampuni husika, jambo ambalo halijafanyika na kwa hiyo hadi sasa hakuna mabadiliko rasmi yaliyofanyika zaidi ya kuwapo hila za kubadilisha.

Januari 25, 2013 Wingert Windrose Safaris ilikutana na Profesa Kideghesho na Mkurugenzi Mkuu wa TAWIRI katika kongamano la kimataifa la Safari Club (SCI), lililofanyoka Reno, Marekani na wote walikana kufahamu chochote kuhusu mabadiliko ya mgawanyo wa vitalu wala majina katika eneo la Ziwa Natron; jambo ambalo linazidisha utata kwani inawezekana vipi mtu aliyesaini barua ya Januari 7, 2013 kukana kufahamu kilichoandikwa humo.

Mapema Februari 2011, ramani ya mgawanyo wa vitalu katika eneo la Ziwa Natron, ilipatikana kutoka TAWIRI Idara ya GIS inayoonesha wazi vitalu vilivyotangazwa Februari 2011 na Wizara.

 

AIBU KWA WIZARA

Mnamo Februari 14, 2013, maofisa wa Wizara wakiongozana na Naibu Mkurugenzi Idara ya Wanyamapori na Mkurugenzi Mkuu wa TAWIRI, walikutana na maofisa wa Wingert Windrose Safaris, na kuonesha ramani kwenye projekta wakidai kwamba ramani hiyo ni ya Februari 2011 kabla ya kutangazwa vitalu.

Ramani hiyo ilikuwa katika mfumo wa ‘PDF’ file na maofisa wa Wingert Windrose Safaris walipobonyeza kwenye ‘properties’ katika ramani hiyo ilionesha kwamba imetengenezwa Februari 2013 na si 2011 kama walivyodai maofisa hao na hivyo kuwa aibu kubwa kubainika kuwa walighushi.

Kwanini ramani hiyo ilighushiwa na kurekebishwa kutoka ramani halisi ya mwaka 2011, ni maswali ambayo majibu yake wanayo wizara.

Kwa hiyo ni dhahiri kwamba Januari 2013; miezi 22 baada ya vitalu kutangazwa, baadhi ya maofisa waovu ndani ya wizara ya Maliasili na Utalii, walijaribu kughushi ili kubadili majina ya vitalu Lake Natron GCA North kuwa East ili kuweza kuwapatia Green Miles Safaris kama inavyoonesha kwenye ramani iliyotolewa na TAWIRI.

Maofisa wa Wingert Windrose Safaris walikutana na Mkurugenzi wa Wanyamapori na maofisa wake katika ofisi za Wizara, jengo la Mpingo Mei 24, 2013 kujadili utata uliojitokeza na kwa mara nyingine inaoneshwa ramani iliyo katika mfumo wa ‘PDF file’ ikidaiwa kuwa imetengenezwa mwaka 2011, lakini baada ya kuingia kwenye ‘properties’ inaonesha tena imetengenezwa mwaka 2013.

Hatua zote hizo za kughushi zimethibitisha nia ovu ya maofisa wa Wizara kujaribu kupindisha ukweli kwa nia ya kuwafurahisha wamiliki wa Green Miles ambao baada ya kugawiwa kitalu chao cha Lake Natron GCA North, walitembelea eneo hilo na kutolipenda kutokana na kuwapo majabali ambayo yangewazuia kufanya uwindaji wa kufukuza wanyama kwa magari kama walivyozea japo kufanya hivyo ni kinyume cha taratibu za uwindaji.

By Jamhuri