Hatimaye wadau wamejitolea kuufufua mchezo wa vinyoya, uliopoteza hadhi yake licha ya kuitangaza Tanzania kimataifa miaka ya 1960 na 1970.

Tayari imeundwa kamati ya muda ya Chama cha Vinyoya Tanzania (Tanzania Badminton Association – TBA) yenye dhamira ya kuuhuisha mchezo huo nchini.

 

Katibu Msaidizi wa TBA, Tony Desonza, amesema nguvu ya mchezo wa vinyoya imefifia kwa miaka 25 nchini sasa, kutokana na viongozi waliokuwapo kuzembea kuandaa mashindano.

 

Pia kuna taarifa kwamba viongozi wa TBA waliopita walijisahau kiasi cha kutoitisha vikao vya kuweka mipango ya maendeleo ya nchezo huo.

 

“Lakini sasa TBA ina uongozi mpya… tumedhamiria kuufufua mchezo huu, na tunaweza kuandaa wachezaji wa kushiriki Olympics (Mashindano ya Kimataifa),” Desonza ameidokeza JAMHURI Dar es Salaam, hivi karibuni.

 

Desonza amesema tayari uongozi mpya wa TBA umeandaa mashindano ya vinyoya kusherehekea Sikukuu za Muungano wa Tanganyika na Zanzibar na ya Wafanyakazi Duniani (Mei Mosi), jijini Dar es Salaam.

 

Hata hivyo, amesema TBA imekosa uwezo wa kuwahudumia wachezaji kutoka mikoani, ambao wameshindwa kushiriki mashindano hayo baada ya kukosa fedha za kujigharamia nauli, chakula na malazi.

 

“Tumeshindwa kuwaleta wachezaji wa mikoani kwa sababu chama [TBA] hakina fedha, hakina support (msaada), hakina wafadhili,” amesisitiza.

 

Kaimu Katibu wa Kamati ya Muda ya kufufua mchezo huo, Timothy Kahoho, anaamini kuwa mchezo huo una nafasi ya kuitangza Tanzania kimataifa kama ilivyokuwa enzi za uongozi wa Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere.

 

“Wakati ule, mchezo wa vinyoya ulifadhiliwa na Mwalimu Nyerere kwa ajili ya kuwaunganisha Waafrika katika kulikomboa Bara la Afrika,” amesema Kahoho na kuongeza:

“Tanzania ilikuwa mshiriki mzuri wa mashindano ya kimataifa ya mchezo wa vinyoya, na kwa njia hiyo ilijitangza na kujulikana sana katika mataifa mbalimbali.”

 

Shabaha ya uongozi mpya wa TBA ni kuona kuwa msukumo unawekwa kuwezesha mchezo wa vinyoya kufufuliwa pia katika shule za msingi, sekondari na vyuoni.

 

“Licha ya ajira, mchezo wa badminton unaburudisha bongo, unamwongezea mchezaji akili, unaimarisha afya na hauna ubaguzi kwani unachezwa na vijana, wanaume na wanawake,” anaeleza Kahoho.

 

Mchezaji maarufu wa vinyoya hapa nchini, Hassanali Haji, ametamba kuwa ana uwezo wa kuibuka mshindi katika mashindano ya kimataifa ya mchezo huo iwapo atapata nafasi ya kushiriki.

 

“Tanzania tumekuwa tukialikwa kushiriki mashindano ya kimataifa ya vinyoya kwa miaka kadhaa, lakini tumekuwa tukishindwa kushiriki kwa kukosa uhamasishaji,” amesema.

Haji ametaja vikwazo vikuu vya mchezo wa vinyoya hapa nchini kuwa ni ukosefu wa vifaa na fedha za uendeshaji.

 

Ametoa wito kwa Serikali kuutazama mchezo wa vinyoya kama michezo mingine, na kufikiria kuutengea bajeti ya kuuhamasisha na kuuendeleza kwa manufaa ya Taifa kwa jumla.

 

 

 

 

 

By Jamhuri