Kuna wakati huwa naona kama ndoto ninapowakumbuka baadhi ya watu. Namkumbuka sana marehemu baba yangu, kwa mtazamo wake na uamuzi wa kifamilia kwa wakati ule. Naona jinsi alivyokuwa na mtazamo wa kitaifa zaidi na si kifamilia.

Namkumbuka sana marehemu kaka yangu aliyekuwa jirani sana na baba, katika pilikapilika za maisha na mtazamo wa maendeleo ya familia na kitaifa. Wote hawakuwa na lengo kwamba siku moja tutakuwa wamiliki wa mali nyingi za familia, badala yake waliiangalia familia kama jamii inayowazunguka.

 

Ninavyowakumbuka hawa vinara katika familia yetu, najua fika ni kizazi kile cha mtazamo chanya wa umaskini wa jamii yao na jinsi ya kuikomboa jamii nzima kuleta maendeleo, na ionekane imepiga hatua mbele. Hapa nawakumbuka viongozi wao wa kitaifa, viongozi ambao wengi wao walipewa majina ya kashfa na kebehi na hao wanaopenda kuiparaganya nia nzuri ya wakati huo.

 

Nawakumbuka akina Kwame Nkrumah, Thomas Sankara,  Frantz Fanon, Julius Nyerere, Leopold Sedar Sengho, Cheikh Anta Diop, Aime Cesaire, Abdulrahman Babu,  Malcom X, Mao Tse Tung, Patrice Lumumba, Jomo Kenyatta, Augustino Neto. Nani anawakumbuka hawa vichwa vya ukweli ambavyo vilikuwa vikiiangalia Afrika kama taifa moja?

 

Sitaki kuwasemea wengine, labda niwasemee marehemu baba, kaka, na Julius, ambao mimi nilikuwa nawafahamu vizuri kama wapigania haki wa kweli, na si blabla ambazo tunaziona katika mataifa mbalimbali walikotoka hao mashujaa wa Afrika.

 

Laiti kama leo Jumanne hii unaposoma gazeti hili, likipigwa baragumu la mwisho wa dunia wafu wafufuke watazame waliyoyaacha nyuma na kujiuliza ni kizazi gani walichokiacha, ni dhahiri mimi nitakuwa wa kwanza kuadhibiwa kwa kushindwa kuwajibika ipasavyo kwa familia ya baba yangu, pili Julius atanitazama kwa jicho baya sana bila kujali dhambi anayopata kwa Mwenyezi Mungu, kwa kushindwa kuwajibika na familia ya kitaifa ilivyoparaganyika.

 

Ni vigumu kidogo kunielewa, lakini ukweli ni kwamba nakusudia kuuzungumzia Ujamaa ambao Mwalimu aliamua kung’atuka ili damu changa iweze kukabiliana na changamoto hizo, na si kuchangamana na changamoto na kupotelea huko huku tukisambaratika kifamilia na kuanza tabia ya umimi kila mmoja.

 

Ni dhahiri kuwa kila kiongozi aliyepigania Uhuru wa taifa lake akajenga misingi imara ya umoja, hatakubali kumwona mrithi wake akiwa amechafua na kuiboronga misingi hiyo. Akina Nkrumah,  Sankara,   Fanon,  Nyerere, Sengho,  Diop, Cesaire,  Lumumba, Kenyatta na Neto hawatakuwa radhi kuyaona yanayoendelea katika mataifa yao, kwa misingi ya demokrasia kuwa pana na kuacha uhuru wa kufanya mambo kwa kigezo cha kulindwa na sheria.

 

Leo nimekumbuka haya kwa sababu kubwa moja ya kujilimbikizia  mali. Kwamba mtu mmoja anaweza kumiliki mali kwa sababu anao huo uwezo wa kumiliki, ambao hauwezi ukauhoji kwa kuwa sheria inamlinda na ataendelea kumiliki mali katikati ya maskini ya wengi wenye uhitaji wa mambo muhimu kwa binadamu kama lishe, shule, hospitali na huduma nyingine za jamii.

 

Katika mataifa mbalimbali yaliyoanza kwa mtindo wa baadhi ya nchi za Afrika, kuitumia vibaya demokrasia na kuingiza ubepari, leo wanashindwa kupiga vita  kuikataa hiyo demokrasia iliyowageuza watumwa ndani ya aridhi yao. Wamejenga matabaka ya walionacho kuendelea kuwa nacho na maskini kufa na umaskini wao.

 

Hili ndilo swali ninaloogopa kuulizwa na baba, kaka na hatimaye Julius. Nitaulizwa mashamba ya pamoja yako wapi? Viwanda viko wapi? Mashirika ya umma yako wapi? Shule zetu ziko wapi? Hospitali je? Nitachanganyikiwa nitakapoulizwa kile kiwanda cha nani? Lile ni eneo la nani? Ile treni ya nani? Hiyo siasa ya nani? Na hiyo nchi ni ya nani?

 

Siamini kama nitaweza kujibu maswali haya, nitaona aibu kwa sababu kama mambo hayo ya kujilimbikizia mali yalikuwa ya msingi sana, basi leo hii kila kitu kingekuwa chetu sisi na si ninyi wenye nacho. Tungemiliki hadi ndege kwa kuwa tulikuwa na uwezo huo kwa ujinga wenu, lakini tulikubali kiwe chetu, sasa iweje leo mtugeuke?

 

Nkrumah amka iangalie nchi yako imetawaliwa na nani?  Sankara fufuka halafu jiulize uliiacha nchi yako hivyo?  Fanon usithubutu kufungua macho utakufuru ulikotoka na upate dhambi,  Nyerere rudi na kitabu chako cha Azimio la Arusha kasome upya halafu angalia kanuni zake, usiseme na mtu, kaa kimya mwangalie huyo mjomba tuliyenaye wa kachupa ka almasi.

 

Sengo, kwako kwafukuta moto umeanza,  Diop, waliendeleza kucheza michezo uchumi wakawaachia wengine, Cesaire kwako ni balaa,  Lumumba nchi yako ni shamba la bibi hata vipofu wanavuna na mwenye shamba anapigwa, Kenyatta mwanao kapewa rungu lakini si kwa KANU tena. Siku hizi kuna vyama hata vya matunda, Neto angalao utapumzika kwa amani.

 

Mungu Ibariki Afrika

Wasalaamu,

Mzee Zuzu,

Kipatimo.

 

 

 

Please follow and like us:
Pin Share