Mchungaji amweka kinyumba kijana

Kituo cha Polisi cha Wazo Tegeta jijini Dar es Salaam katika Mkoa wa Kipolisi wa Kinondoni kimeshutumiwa na wakazi wa eneo hilo kumlinda mhalifu anayedaiwa kumweka kinyumba mtoto wa kiume ambaye ni mwanafunzi (17).

Kijana huyo (jina tunalo) anadaiwa kutekwa na Martha Haule ambaye ni mke wa Mchungaji Mwandamizi wa Kanisa la House of Prayer Shield of Faith Christian Fellowship Church lililoko Boko Magengeni jijini hapa. Martha ambaye ni mwajiriwa wa Taasisi ya  Ufundi Dar es Salaam ( DIT) inadaiwa kwa kutumia wadhifa wake ndani ya Kanisa hilo alimteka kijana huyo na kuishi naye kwenye nyumba mbalimbali za kulala wageni kwa muda mrefu.

Wakati tukio hilo likitendwa kijana huyo alikuwa bado ni mwanafunzi wa kidato cha pili katika Shule ya Sekondari ya Kutukutu, Mkoani Morogoro.

Kijana huyo aliletwa Dar es Salaam na wazazi wake miaka miwili iliyopita kwa ajili ya maombi baada ya jitihada za kutibiwa hospitalini kushindikana.

Kwa mujibu wa uongozi wa kanisa baada ya tukio hilo kugundulika walitoa taarifa katika Kituo Kidogo cha Polisi cha Wazo na kupewa RB na W/RB/7717/2016 na kuendelea kufuatilia bila ya mafanikio.

“Tuliendelea kufuatilia hatima ya tukio hili kituoni hapo bila ya mafanikio yoyote hali ambayo imeendelea kutufadhaisha na kutukatisha tama,” anasema mmoja wa viongozi wa kanisa ambaye hakupenda jina lake kutajwa.

Anasema ilifikia hatua mama huyo (mama Mchungaji) alimtorosha huyo kijana kutoka kituoni na kwenda kumficha kwenye nyumba za wageni huku akijua kuwa kijana huyo bado ni mwanafunzi.

Anasema baada ya kushangazwa na ukimya wa polisi, Kanisa lilichukua hatua za kumsimamisha (mama Mchungaji) kutoa huduma za kichungaji kwa barua yenye kumbukumbu namba HOPSFCF/DSM/YK/564/2014  ya Machi 23, 2014.

Anasema kitendo kilichofanywa na huyu mama kimelifedhehesha kanisa kwa kiwango kikubwa.

“Ni aibu kwa mama mzima wa miaka (40) tena mke wa Mchungaji kutumia wadhifa wake kumdhalilisha mtoto mdogo wa miaka 17 kufanya naye mapenzi,” anasema kiongozi huyo.

Kwa upande wake kijana aliyefanyiwa ukatili huo alikiri kumfahamu mama huyo kupitia kanisani hapo na kukiri kuwahi kuwa na uhusiano wa kimapenzi na mama huyo.

“Mara baada ya kuletwa hapa kanisani nikitokea Morogoro, mama huyu alikuwa miongoni mwa wachungaji ndani ya Kanisa hili,” anasema kijana huyo.

Anasema kwa mara ya kwanza hakujua malengo ya huyo mama kwani alikuwa akimchukulia kama kiongozi ndani ya kanisa kumbe alikuwa na malengo mengine.

Anasema mama huyo alijenga utamaduni wa kumwita mara kwa mara nyumbani kwake mumewe anapotoka kwenda kanisani.

“Mara nyingi nilimchukulia kama kiongozi wangu, lakini alitumia nafasi ya mimi kumheshimu na kujikuta ananishawishi kuwa rafiki yake kimapenzi,” anasema kijana huyo.

 Anasema, alikuwa akimletea zawadi kila mara baada ya kuona kuwa siri ilikuwa inaelekea kujulikana akimweleza kwamba hali imeshakuwa mbaya kwa hiyo watoroke. Ndipo alipomchukua na kumpeleka kwenye nyumba moja ya wageni maeneo ya Ubungo.

“Nilikuwa nikihamishwa kutoka katika nyumba za wageni kila baada ya siku tatu huku akiniambia kuwa ni kwa sababu ya usalama wangu,” anasema kijana huyo.

 Uhusiano wao ulikoma baada ya kijana kufanikiwa kujinasua na kukimbilia kwao, Mkoani Morogoro.

  Anasema  mpaka sasa maisha yake yapo hatarini kwani mama huyo amekuwa akimpigia simu za vitisho na kumwambia kuwa atahakikisha anapambana naye mpaka mwisho.

Anasema mama huyo amekuwa anamtolea vitisho kutokana na yeye kwenda kanisani na kukiri alichokuwa akifanyiwa na mama mchungaji, huku akiungama mbele ya kanisa na kueleza jinsi hali ilivyokuwa kuanzia mwanzo hadi mwisho.

“Hapa nilipo siwezi kutoka nje ya eneo la kanisa maana yule mama bado ananitafuta mpaka leo anadai siwezi kumuacha kienyeji kiasi hicho,” anasema.

Anasema kwa sasa maisha yake yapo hatarini kwani mama huyo anampigia simu za vitisho akidai kuwa yeye ndiye chanzo cha kufukuzwa kanisani.

Mama huyo alikuwa ni mke wa Mchungaji, baada ya kanisa kubaini uhusiano wake  na kijana huyo, alisimamishwa kuhudumu ndani ya kanisa kwa maana ya kutengwa.

Kwa upande wake mama mzazi wa kijana huyo Grace Yusuph Mshana anayeishi mkoani Morogoro anasema analielewa tukio hilo na kwamba limemfedhehesha.

“Mara baada ya kuzipata taarifa hizi imenilazimu kufunga safari kuja jijini kwa ajili ya kuangalia hatima ya jambo hili lililomfika mwanangu,” anasema Mshana.

Anasema mwanae alipatwa na matatizo yasiyofahamika miaka miwili iliyopita hali iliyokatisha masomo yake, baada ya jitihada za kupatiwa matibabu hospitalini kushindikana ndipo alipochukua jukumu la kumpeleka kanisani hapo kwa ajili ya maombi.

“Mimi na baba wa mtoto huyu, tulitengana akiwa na miaka miwili kwa hiyo nimehangaika naye mpaka anafikia hivi halafu mama mtu mzima anatumia wadhifa wake kumdhalilisha kingono? Hii ni aibu,” anasema Mshana.

Anasema kitendo hicho kimechangia kwa kiwango kikubwa mwanae kushindwa kuendelea na shule kwani kimemwathiri kisaikolojia.

Kwa upande wake Martha Haule anaye daiwa kutenda unyama huo alipotafutwa na JAMHURI kuelezea madai hayo, alikataa kulifahamu tukio hilo na kudai kuwa uongozi wa kanisa unataka kumchafulia jina.

“Ni kweli mume wangu alikuwa ni mmoja wa Wachungaji Waandamizi ndani ya kanisa, lakini aliamua kuachana na utumishi ndani ya kanisa hilo kwa hiyo yote hayo yanayosemwa hayana ukweli wowote,” anasema.

Anasema tangu yeye na mume wake waachane na kanisa hilo, uongozi umekuwa ukiwazushia mambo yanayolenga kuwadhalilisha.

Alipotafutwa askari aliyekabidhiwa jalada la kijana huyo kutoka katika kituo hicho cha Wazo aliyefahamika kwa jina moja la Maneno, alikiri kulifahamu suala hilo, lakini akasema yeye si Msemaji wa Jeshi la Polisi.

Alipotafutwa Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Kinondoni, ACP Christopher Fuime amesema halifahamu na hivyo ameahidi kulifuatilia.

“Kama tukio hili liliripotiwa katika kituo hicho halafu wakashindwa kuchukua hatua ni makosa,” anasema Kamanda Fuime.

Anasema kwa kawaida uchunguzi unatakiwa uwe umekamilika ndani ya siku 60 kinyume na hapo labda zijitokeze sababu maalumu.

Pamoja na RPC Fuime kuahidi kufuatilia tukio hilo taarifa zilizolifikia JAMHURI zinaeleza kwamba jalada hilo limepotea katika Kituo Kidogo cha Polisi cha Wazo.