Mtendaji Mkuu wa Taasisi ya Hifadhi za Bahari na Maeneo Tengefu (MPRU), Dk. Milali Machumu, amelalamikiwa na watumishi wa taasisi hiyo kwa matumizi mabaya ya fedha za umma, ubabe na ubaguzi kwa watumishi, mambo  yanayochangia sekta ya utalii kudorora.

Dk. Machumu anatuhumiwa kufanya madudu hayo chini ya kivuli cha Bodi ya Wadhamini ya Hifadhi za Bahari na Maeneo Tengefu na Katibu Mkuu wa Wizara ya Maendeleo ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi (Uvuvi), Dk. Yohana Budeba, kwa madai kwamba amepewa maelekezo na wizara kuwapunguza vyeo na mishahara ya baadhi ya maofisa.

Wanasema hawana makosa yoyote na baada ya utumishi wao mzuri Juni, 2012 Bodi iliwapandisha vyeo na mishahara wakati huo Dk. Machumu akiwa miongoni mwa wajumbe wa Bodi hiyo, lakini kinachowashangaza ni kuidanganya Bodi kwamba watumishi hao walijipandisha vyeo wenyewe na muundo wa taasisi hiyo haukupitishwa na Msajili wa Hazina.

Hata hivyo, wanasema jambo linalowashangaza ni kufanya uamuzi kibabe kwa madai ya kupewa ruhusa na Katibu Mkuu, Dk. Budeba, ya kuwaondoa wajumbe wote wa menejimenti ya taasisi hiyo kwa kuwashusha vyeo walivyopandishwa kihalali kisha kuwahamishia kwenye vituo vidogo.

Pamoja na kufanya ubabe huo, ameshindwa kuwalipa fedha za uhamisho, hali ambayo imewazidishia ugumu wa maisha na familia zao katika maeneo mapya ya kazi waliyopangiwa na baadhi yao kwa zaidi ya miezi mitano sasa hawana mishahara kutokana na kukatwa madeni ya mikopo waliyokuwa wamekopa katika benki.

“Taasisi hii ameigeuza kampuni ya Mhindi, kwani kwa muundo wake ilikuwa na watu wanne walioidhinishwa kuwa watia saini wa benki ambao waligawanywa wawili wawili kwa kundi ‘A’ na ‘B’. Sasa amewatoa wote wa kundi ‘B’ na kusalia kundi ‘A’ tu akiwamo yeye na mhasibu wa taasisi na hapa ndiyo mlango wa matumizi mabaya ya fedha za umma aliojiwekea ulipo,” anasema mmoja wa wafanyakazi.

 

Matumizi mabaya ya fedha za umma

Wakati wa mkutano wa Bunge la bajeti 2015/2016,  Dk. Machumu peke yake ndiye aliyehudhuria kipindi cha maswali na majibu kutoka MPRU ilipofika zamu ya Wizara ya Maendeleo ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi na kutumia Sh milioni 20 kwa siku zisizozidi kumi na matumizi halisi ya fedha hizo hayajulikani.

Pia alichukua Sh milioni 5 kwa ajili ya kuwalipa wajumbe wa kikao cha wadau wa Hifadhi ya Tanga, wakati kituo hicho kina mhasibu ambaye angeweza kufanya malipo hayo na yote hiyo ni njia ya kujipatia fedha zinazotakiwa kulipwa na taasisi.

Kumlipa ‘utilities’ Ofisa Utumishi aliyemwazima kwa muda kutoka wizarani wakati akifahamu kuwa mtumishi huyo hakuwa na sifa ya kulipwa fedha hizo huku Ofisa Utumishi Mwandamizi ambaye alihamishiwa Mtwara hakuwahi kulipwa ‘utilities’ zake wala fedha zake za uhamisho kwa mwaka mzima hadi alipofukuzwa kazi Julai, mwaka jana. 

Alipohojiwa na JAMHURI, Meneja wa taasisi hiyo, Dk. Machumu, kwa nyakati tofauti kuhusu kuiongoza taasisi hiyo kwa ubabe, matumizi mabaya ya fedha za umma na kuwafukuza kazi, kuwashusha vyeo na kuwahamisha baadhi ya watumishi bila kuwalipa stahiki zao, akasema madai hayo yameandikwa mno na kumtaka mwandishi kuandika yale anayodai yameandikwa muda mrefu.

 “Mimi sihusiki na uhamisho wowote wa watumishi. Serikali hii ya Rais Magufuli unahamisha watu kwa fedha zipi za kuwalipa? Anahoji Dk. Machumu ambaye amekwishawahamisha na kuwashusha vyeo bila sababu za msingi maofisa wote wa menejimenti ya taasisi hiyo.

Mwenyekiti wa Bodi ya Wadhamini ya Taasisi ya Hifadhi za Bahari na Maeneo Tengefu, Profesa John Machiwa, ameieleza JAMHURI kwamba malalamiko ya watumishi hao yamepelekwa katika vyombo mbalimbali vya haki na kushughulikiwa na vyombo hivyo.

Profesa Machiwa anasema vielelezo vipo kwenye taasisi husika ambayo nayo inashughulikia suala hilo huku akikana kwamba Bodi hiyo haikuletewa malalamiko na watumishi hao, huku walalamikaji wakieleza kuwa bodi ilipewa taarifa na muundo unaotumiwa na taasisi bado unatumika wa mwaka 2006.

“Kulikuwa na maelezo kwamba inaandaliwa ‘scheme of services’ nyingine naona haijakamilika na sisi hatujaiona,” anasema Profesa Machiwa.

 

Katibu Mkuu (Uvuvi)  

Katibu Mkuu (Uvuvi), Dk. Budeba ambaye anaelezwa na baadhi ya wajumbe wa Bodi hiyo kuwa jina na cheo chake vilitumiwa na Meneja, Dk. Machumu kuwahadaa wajumbe kwamba amepewa idhini na kiongozi huyo kuwashusha vyeo, mishahara na kuwahamisha wajumbe wote wa menejimenti ili atekeleze majukumu yake vizuri anasema amepokea malalamiko ya watumishi hao na kumshauri Waziri kuchukua hatua.

Dk. Budeba anasema wanafanya taratibu za uchunguzi na kuitisha kikao cha Bodi kuhusu ubabe, matumizi mabaya ya madaraka na fedha za umma unaomhusu Meneja wa taasisi hiyo.

“Iweje watu wanashushwa vyeo na wengine kufukuzwa kazi bila kufuata taratibu halafu tunalaumiwa sisi kwamba ndiyo tunaomlinda kiongozi huyu?” anahoji. 

Naye Dk. Chande ambaye alikuwa Meneja wa taasisi hiyo kabla ya Dk. Machumu, anasema anashangazwa na taarifa za kuwashusha vyeo na mishahara watumishi hao kwa madai kwamba walipandishwa vyeo bila utaratibu.

Anasema vyeo vyao walipandishwa kihalali na Bodi kulingana na muundo wa taasisi uliopitishwa na Msajili wa Hazina mwaka 2006, ambao aliukuta ukiwa umeandaliwa na mtangulizi wake alipoteuliwa na Rais John Magufuli wakati huo akiwa Waziri wa Uvuvi.

“Huyu Meneja wa sasa (Dk Machumu) hana uwezo wa kuongoza taasisi hiyo na kinachofanyika sasa ni kuiua kwa kuendekeza chuki na ubabe kwa watumishi walio chini yake.

“Scheme of service inayotumika kwa kada zote wakiwamo wahudumu na madereva haiwezi kubatilisha vyeo vya baadhi ya watumishi, na yeye kwa nini asipunguze mshahara wake kama alivyofanya kwa wengine?” anahoji mmoja wa wafanyakazi.

Hata hivyo, anasema kuinusuru taasisi hiyo, Waziri wa Kilimo, Mifugo na Uvuvi anapaswa kutengua uteuzi wa Dk. Machumu na kumweka mtu mwenye uzoefu wa kusimamia na kuongoza taasisi za Serikali na kuwapa haki zao watumishi hao walioshushwa vyeo na mishahara kwa uonevu.

By Jamhuri