Mtendaji wa Kijiji cha Luchili, Kata ya Nyanzenda, Halmashauri ya Buchosa Sengerema, mkoani Mwanza anatuhumiwa kumtorosha Mchungaji wa Kanisa la Agape, lililopo katika kijiji hicho, Geofrey Kamuhanda, anayetuhumiwa kumbaka na kumlawiti binti wa miaka 13.

Vyanzo vya habari vimeiambia JAMHURI kuwa tukio la kubakwa kwa mtoto huyo na Mchungaji Kamuhanda, lilitokea Januari 10 mwaka huu kijijini hapo.

Siku moja baada ya tukio, Ofisa Mtendaji wa Kijiji cha Luchili, Mathias Njulilo, alimkamata Mchungaji huyo ila ofisi yake ikamwachia katika mazingira ya kutatanisha.

“Baada ya tukio hilo, ofisi ya Mtendaji iliagiza Mchungaji huyo kukamatwa mara moja kwa hatua zaidi ikiwamo kupelekwa polisi, lakini saa chache baada ya kufikishwa ofisini hapo, Mchungaji huyo aliachiwa katika mazingira yenye utata na yaliyoacha maswali mengi kwetu,” anasema mtoa taarifa.

Taarifa zinaonesha baadhi ya wachungaji wa madhehebu ya Kikristo katika kijiji hicho walimchangia nauli Mchungaji huyo akaondoka, huku wananchi wakiutupia lawama uongozi wa kijiji kwa kukumbatia uozo na kuiomba Serikali kuwachukulia hatua kali za kisheria.

Dada wa binti aliyefanyiwa ukatili huo (jina tunalihifadhi) anasema kuwa mdogo wake alifika kwake maeneo ya Kashai, Bukoba Mjini akiwa amebakwa na kuumizwa vibaya kutokana na ukatili huo.

Anasema Mchungaji alimchukua mdogo wake kwa ajili ya kwenda kumsomesha na hakujua kama alikuwa na lengo jingine la kumfanyia unyama huo na ambao umemwachia kilema cha kudumu kilichotokana na kumbaka.

“Naiomba Serikali hii ya awamu ya tano kwa vile imeapa kukomesha vitendo hivi, basi ianze na waliohusika kumtorosha, kwani hawa ndiyo wanaofahamu alipo Mchungaji huyu aliyevaa ngozi ya kondoo wakati ni mbwa mwitu mkali. Wala hatukuwahi kuwaza kwamba ndugu yetu angekuja kukumbana na tukio hili kwenye maisha yake,” anasema dada huku akibubujikwa na machozi.

Akisimulia tukio hilo, binti aliyebakwa (jina linahifadhiwa) anasema Mchungaji alimwomba kwa wazazi wake wanaoishi katika Kijiji cha Izibwa, Wilaya ya Bukoba Vijijini kwa lengo la kwenda naye wilayani Sengerema, mkoani Mwanza amsomeshe.

Anasema baada ya siku nne akiwa nyumbani kwa Mchungaji huyo, alimuuliza kuhusu shule na kujibiwa kuwa atampeleka shule asijali.

Anasema usiku wa siku hiyo saa chache tangu alipotaka majibu ya lini angepelekwa shule, Mchungaji Kamuhanda alimfuata chumbani akiwa amelala na kumkaba koo kisha kumfanyia unyama huo kwa kumbaka na kumlawiti huku akimwacha na maumivu makali sehemu za siri.

“Yaani nilihisi kama nakufa maana maumivu niliyoyapata sikuwahi kuyapata maishani mwangu na kugundua kuwa hiyo ndiyo shule ambayo nililetwa kuisoma kwa Mchungaji huyo, na kinachonisikitisha zaidi hata baada ya kutoa taarifa Ofisi ya Kijiji, Mchungaji alikamatwa na kuachiwa baadaye na viongozi hao bila kujali maumivu aliyonipa wakati ananibaka,” anasema binti huyo.

Shuhuda wa tukio

Asha Hamud ni mmoja wa mashuhuda wa tukio hilo la Mchungaji Kamuhanda, wa Kanisa la Agape, kumbaka na kumlawiti mtoto huyo, anasema alikuwa jirani wa binti huyo na kwamba asubuhi ya Januari 10, mwaka huu binti aliamka asubuhi analia huku mashavu yake wakiwa yamevimba.

Anasema mbali na binti huyo kuvimba mashavu, pia alikuwa anatembea kwa kuchechemea na alipomuuliza alieleza kuwa Mchunguji amembaka usiku na kumwingilia kinyume na maumbile zaidi ya mara mbili.

“Akanieleza kwa sababu hakuwahi kufanya vitendo hivyo, anahisi maumivu makali na ndipo tukachukua jukumu la kumpeleka katika Ofisi ya Mtendaji wa Kijiji hicho kuomba msaada ili mtuhumiwa huyo akamatwe,” anasema.

Baada ya muda Mtendaji wa Kijiji hicho, Mathias Njolilo, alimwagiza Mwenyekiti wa Kamati ya Ulinzi wa Kijiji ambaye ni Mwenyekiti wa Kitongoji cha Luchili Senta, Msazibwa Daud, amkamate na kufanikiwa kumkamata na kumfikisha katika ofisini za kijiji na kumfungia katika chumba cha mahabusu wakisubiri taratibu nyingine za kumfikisha polisi.

Wakiwa wanasubiri taratibu hizo ndani ya nusu saa wakati binti huyo akisubiri kupatiwa huduma za matibabu, harakaharaka zilichangwa fedha za nauli kumsafirisha binti huyo hadi kwao mkoani Kagera.

“Lengo la kuchangwa fedha hizo haraka ilikuwa ni kupoteza ushahidi wa tukio hilo kwani baadaye binti huyo aliambiwa anapelekwa Hospitali ya Wilaya ya Sengerema kuchunguzwa afya yake, lakini cha ajabu alipofikishwa Sengerema mjini alipandishwa kwenye basi linalofanya safari Bukoba, hali iliyoniacha mdomo wazi nisijue kitakachoendelea baada ya hapo,” anasema.

 

Mchungaji azungumza

JAMHURI imemtafuta Mchungaji huyo aliyekiri kuhusika na kitendo hicho, huku akisema masuala hayo anayakabidhi mikononi mwa Mungu kwa vile ndiye anayeweza yote.

“Yote yanayopatikana kwa wanadamu siwezi kusemea lolote juu ya suala hilo, hata mimi sikutegema, naomba msamaha msinitangaze maana ni fedheha kwangu na wachungaji wenzangu. Aombaye kama ametenda kosa husamehewa,” anasema Mchungaji huyo.

Mtendaji wa Kijiji cha Luchuli, Njolilo alipoulizwa kuhusu tuhuma za kumkamata na kumwachia Mchungaji huyo amekana kwamba hafahamu chochote.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Kijiji hicho, Ibrahimu Mbata mbali na kukiri kukamatwa kwa Mchungaji huyo, alithibitisha pia kupatiwa kiasi cha Sh 20,000 kama mgao wake akiwa ofisini, lakini hakujua fedha hizo alizopewa zilikuwa za nini.

Mkuu wa Wilaya ya Sengerema, Emmanuel Kipole, anasema hana taarifa za tukio hilo, na kuahidi kulifuatilia haraka iwezekanavyo na kwamba atachukua hatua stahiki iwapo atabaini mtendaji huyo amehusika kwa namma moja au nyingine kufanikisha uovu huo.

“Kama kweli mtendaji huyo amefanya makosa hayo ya kumwachia mtuhumiwa, nitaagiza vyombo vya usalama vimkamate na amtafute mtuhumiwa aliko pia atoe maelezo kwa nini amemwachia mtuhumiwa wa kosa hilo badala ya kumpeka katika vyombo husika,” anasema Kipole.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza, Ahmed Msangi, alipoulizwa kuhusu tukio hilo na hatua zilizochukuliwa dhidi ya wahusika, hakukiri wala kukana na badala yake alitaka atafutwe baadaye.

Hata hivyo, alipopigiwa tena simu hakupokea wala kujibu ujumbe mfupi wa maneno aliotumiwa.

Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake (TAMWA) kimefanya tafiti mbalimbali kupunguza ukatili wa wanawake kupitia habari za ushahidi wa matendo hayo na kupendekeza suluhisho mwafaka.

Lengo kuu la utafiti huo lilikuwa ni  kukusanya taarifa za awali zinazoonesha hali ya ubakaji na watoto wa kike wanafunzi kulazimishwa kuolewa, ukeketaji, ubakwaji, vipigo kwa wanawake na watoto na wanawake kutelekezwa kujenga msingi wa kisayansi juu ya chanzo cha ukatili huo na kutafuta ufumbuzi wa kudumu.