. Watu wanatuma mawazo bunifu kupitia Tweeter

. Washindi wazawadiwa Sh mil 1.8 kila mwezi

Katika juhudi za kutafuta ufumbuzi wa umaskini Tanzania, Mwenyekiti wa kampuni za IPP, Dk. Reginald Mengi, ameanzisha shindano la mawazo mapya yanayotaja mbinu bora za kutokomeza tatizo hilo.

Shindano hilo limeanza rasmi Mei 13, mwaka huu, kupitia mtandao wa kijamii wa Tweeter na litadumu kwa miezi 12 (Mei 2013 – Aprili 2014).

 

Tayari washindi watatu wa Mei mwaka huu wametangazwa na kukabidhiwa Sh milioni 1.8. Mshindi wa kwanza ni Jilly Kiomo (26) aliyezawadiwa Sh milioni moja, akifuatiwa na Peter Ngugulu (19) aliyetuzwa Sh 500,000 na Ludovick Angelino (22) aliyepewa Sh 300,000.

 

Akizungumza katika hafla ya kukabidhi zawadi hizo kwa washindi hao jijini Dar es Salaam wiki iliyopita, Dk. Mengi amesema shindano hilo litasaidia kuonesha njia sahihi za kukabili umaskini mkubwa unaoendelea kuwaganda Watanzania.

 

“Hata baada ya miaka 50 ya uhuru, umaskini umewaganda Watanzania kwa namna ya ajabu na inayotia aibu. Hili linaonekana mpaka kwenye mahitaji ya msingi kama vile chakula,” anasema Dk. Mengi na kuongeza:

 

“Watanzania wengi ni maskini mno kiasi kwamba hawawezi kula milo miwili kwa siku, achilia mbali chakula kilichokamilika chenye lishe bora.

 

“Maisha ya Watanzania wengi ni ya dhiki sana, hawajui kesho watakula nini, wengine wamekata tamaa ya kuishi. Mwanadamu akifikia hatua ya kukata tamaa anashawishika kufanya mambo yasiyo ya kawaida.

 

“Serikali imeshafanya hatua nyingi kukabili umaskini lakini labda mawazo na fikra ambazo zimekuwa zikitumika si sahihi ndio maana bado umaskini upo.”

 

Mwenyekiti huyo wa IPP anaeleza kusikitishwa na taswira ya umaskini kuchukua hatamu katika nchi ya Tanzania yenye utajiri mkubwa wa rasilimali za kila aina.

 

Kwa sababu hiyo, anasema kwamba ili Tanzania iweze kuondokana na umaskini lazima kuwepo na mikakati mipya yenye majibu sahihi juu ya nini kifanyike kufuta tatizo hilo.

 

“Ni dhahiri kuwa mafanikio ya kuondoa umaskini yatawezeshwa na fikra, mawazo na ushauri kutoka kwa Watanzania wenyewe, ndio maana nimeanza kukaribisha mawazo mapya kupitia Tweeter,” anafafanua Dk. Mengi.

 

Mpango huu wa Dk. Mengi unatarajiwa kuibua idadi kubwa ya mawazo mapya yatakayopendekeza mbinu madhubuti za kuupiga vita umaskini na kuwezesha maendeleo ya kweli nchini.

 

Matarajio ni kwamba serikali kupitia mipango yake itatumia mawazo hayo kushughulikia changamoto kubwa ya kuondoa umaskini na kuwezesha maisha bora kwa kila Mtanzania.

 

Kwa upande mwingine, Dk. Mengi anaamini kuwa vitendo vya rushwa na ufisadi katika taasisi za umma ni miongoni mwa vyanzo vikuu vya umaskini wa Watanzania.

 

Katika uchambuzi wa mawazo yanayotolewa na wananchi katika shindano hilo, Dk. Mengi anashirikiana na Dk. Donath Olomi ambaye ni Ofisa Mtendaji Mkuu wa Taasisi ya Uongozi na Maendeleo ya Ujasiriamali cha jijini Dar es Salaam.

 

Dk. Olomi anampongeza Dk. Mengi kwa uamuzi wa kuanzisha shindano hilo akisema ni mpango wenye umuhimu mkubwa utakaoibua mawazo bunifu na kuchochea kasi katika jitihada za kupambana na umaskini hapa nchini.

 

Tweets za Mei 2013

Kwa mujibu wa Dk. Olomi, watu 481 wameshiriki kutoa mawazo yao kati ya Mei 13 na 31, mwaka huu kupitia mtandao wa Tweeter.

 

Dk. Olomi ambaye ni mtaalamu wa masuala ya ujasiriamali na mapambano dhidi ya umaskini, ndiye aliyeongoza shughuli ya uchambuzi wa mawazo hayo hadi kuwapata washindi hao watatu.

 

“Yametolewa mawazo mengi juu ya namna ya kuondoa umaskini ambayo yamegawanyika katika sehemu tatu,” anasema Dk. Olomi na kuendelea:

 

“Mawazo tuliyoyapokea ni jinsi mtu anavyoweza kufikiri na kutenda ili aondoke kwenye umaskini, jinsi inavyotakiwa kufikiri na kuondoa umaskini, na serikali na wadau wengine wafanye nini kuwaondolea wananchi umaskini.

 

“Kwa mantiki hiyo, tumechagua tweet moja iliyotugusa kuliko zote kupata zawadi ya kwanza ya shilingi milioni moja, ili kutoa hamasa.

 

“Katika kufanya uchaguzi tumeangalia vigezo vitatu muhimu. Kwanza, wazo linaloeleweka na kuelezeka kirahisi. Pili, wazo bunifu ambalo halijasikika na kuonekana kwenye sera au mipango ya nchi. Tatu, wazo linalowezekana kutekelezwa katika mazingira ya Tanzania.”

 

Wazo lililomwezesha Jilly Kiomo kuibuka mshindi wa kwanza linasema, “Tuwe na utamaduni wa kupenda kile tukifanyacho, kukifanya kwa moyo, uadilifu, heshima na kujali muda, hata kama it’s self employed.”

 

Dk. Olomi anatoa sababu ya kuchagua wazo hilo kushika nafasi ya kwanza katika shindano hilo kuwa linahimiza kila mtu kutu katika kuia mbinu hizo kupambana na umaskini.

 

“Watu wengine wanafikiri mafanikio yanakuja kwa kufanya mambo ya ajabu, lakini chochote utakachokifanya, iwe nyumbani, shuleni, kwa mwajiri au kwenye biashara kwa kukipenda kwa moyo, uadilifu, heshima na kujali muda si rahisi kubaki maskini,” anasema Dk. Olomi.

 

Wazo lililomwezesha Peter Ngugulu kushika nafasi ya pili linasema, “Kuweka mfuko wa mikopo kwa vijana wanaowekeza kwenye kilimo na kukuza sekta ya kilimo na viwanda vyenye uhusiano wa moja kwa moja.”

 

Wazo hilo linakumbusha kwamba rasilimali mojawapo inayoweza kutumika kuzalisha ajira nyingi kwa vijana wanaotoka vyuoni na shuleni ni ardhi, katika kupunguza umaskini miongoni mwa jamii ya Watanzania.

 

Naye Ludovick Angelino ametwaa nafasi ya tatu katika shindano hilo kutokana na wazo lake linalosema, “Uongo ndio chanzo cha umaskini, tunachekea ufisadi, tunashindwa kuchagua na kuteua watu sahihi wa kutuongoza.”

 

Ni kweli kwamba miongoni mwa mambo yanayochangia umaskini wa Watanzania walio wengi ni ufisadi na ukosefu wa uongozi bora katika ngazi mbalimbali.

 

Kwa msingi huo, Dk. Mengi na Dk. Olomi wanatoa wito kwa wananchi kujitokeza kwa wingi kushiriki shindano hilo kwa kutoa mawazo mapya yaliyo bora zaidi yanayofaa kutumiwa katika kutokomeza umaskini Tanzania.

 

Kwa yeyote anayehitaji kushiriki shindano hilo anashauriwa kufungua mtandao wa Tweeter na kutafuta jina la Dk. Mengi kwa kuandika neno ‘regmengi’ ili kupata ukurasa wa kuandika wazo lake.

 

1303 Total Views 1 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!