Shilingi milioni 200 zilizotengwa kwa ajili ya ujenzi wa skimu ya umwagiliaji katika vijiji vya Nyamboge kilichopo Kata ya Katoma; na Nzera katika Kata ya Nzera, Wilaya ya Geita mkoani, ‘zimeyeyuka’.

Fedha hizo zilitengwa kupitia Programu ya Uwezeshaji Miradi ya Kilimo Wilaya (DASIP).

 

Mradi huo unaojulikana kama Nyamboge-Nzera unahusisha vijiji hivyo vinavyopakana. Una ukubwa wa eneo la hekta 2,000 ukiwahusisha wakulima 289.

 

DASIP ilianzishwa mwaka 2006 chini ya Wizara ya Kilimo kuwajengea uwezo wakulima kwenye miradi kadhaa ikiwamo ya umwagiliaji, machinjio, maghala, ujenzi wa malambo, mashine za kusaga nafaka na vyama vya akiba na mikopo (SACCOS).

 

Miradi ya DASIP iliibuliwa katika mikoa ya Shinyanga, Mara, Mwanza, Kagera na Kigoma.

 

Ofisa Kilimo na Mifugo Wilaya ya Geita, Peter Mtagwaba, anasema kuwa mradi wa Nyamoge-Nzera hauko kwenye programu ya DASIP, bali upo kwenye programu ya ASDP.

 

Kuhusu taarifa zote za idara yake ya kilimo za Halmashauri hiyo kwenda kwenye vikao vya uamuzi hasa Baraza la Madiwani kuonesha kuwa mradi huo unatekelezwa na DASIP, lakini anasema ni mradi wa ASDP, alijibu kuwa ni makosa ya wanaopeleka taarifa hizo kwa madiwani.

 

“Taarifa hizo hazijatoka kwangu, labda zimetoka ofisi nyingine,” anasema Ofisa Kilimo huyo.

 

Anasema kuwa mradi huo umeshatumia shilingi zaidi ya milioni 134 kwa ajili ya upembuzi yakinifu.

 

Wakati Ofisa Kilimo na Mifugo akisema kwamba mradi huo unasimamiwa na ASDP, nyaraka za Halmashauri hiyo zinaonesha kuwa  katika kikao cha Baraza la Madiwani cha Mei 10,  2011 taarifa iliyotolewa ya mradi huo ni kuwa umetengewa fedha za ruzuku ya Serikali za Mitaa ya Sh milioni 200; na siyo ASDP.

 

Taarifa hiyo inaeleza kwamba Sh milioni 135.549 zimetumika kufanya upembuzi yakinifu na sehemu ya fedha hizo zilipelekwa kwa wakulima.

 

Mwenyekiti wa Kikundi cha Wakulima, Saleh Shagembe anakanusha kupokea fedha zozote kutoka Halmashauri ya Geita.

 

“Hutujawahi kupokea pesa yoyote kwa ajili ya mradi wetu wa skimu ya umwagiliaji,” anasema.

 

Anasema kuwa wakati wa kufanya upembuzi yakinifu wakulima walijitolea nguvu na baadhi ya vitendea kazi, akitoa mfano kuwa yeye mwenyewe alichangia makarai 10 ya kokoto na Bwana Shamba alichangia makarai matano ya kokoto.

 

“Bado nadai laki mbili, lakini leo nashangaa kusikia matumizi ya milioni zaidi ya mia moja wakati sehemu kubwa ya kazi tulijitolea sisi wakulima. Kama kweli wamelipana pesa hiyo, huo ni ufisadi kwa wakulima,” anasema.

 

Katika mkutano wa kawaida wa Baraza la Madiwani wa Oktoba 25, 2011 madiwani waliambiwa kuwa mradi huo umetekelezwa kwa kutumia fedha za Mfuko wa Uwezeshaji Kilimo cha Umwagiliaji Wilayani.

 

Pesa hizo ziko katika mchanganuo wa Sh milioni 17. 765 za kufanya upembuzi yakinifu wa skimu hiyo (Geotechnical survey), kufanya stadi ya maji kwa Sh milioni 4.8 na ongezeko la hekta 50 kwa kuzifanyia upembuzi (Sh milioni 4.42).

 

Mutagwaba alipoulizwa kwanini anasema idara yake ilitumia Sh milioni 135.5 kufanya upembuzi yakinifu, lakini kwenye Baraza la Madiwani nyaraka zinaonesha zilitumika Sh milioni 26.9, alisema kuwa nyaraka hizo hazikutoka kwake.

 

Bajeti ya Halmashauri ya Geita kwa mwaka wa fedha wa 2010/2011 iliidhinisha Sh milioni 200 kwa ajili ya mradi huo. Katika kikao cha madiwani wa Halmashauri hiyo cha mwaka 2011, Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri hiyo alitoa taarifa katika kikao hicho kuwa Sh milioni 135 zilitumika kujenga mradi huo ikiwa bado wana upungufu wa Sh milioni 65.

 

Taarifa ya DASIP ya nusu mwaka ya mwaka 2010/2011 iliyotolewa Desemba 2010 inaonesha kuwa katika Kijiji cha Nyamboge na Kijiji cha Nzera hapakuwa na mradi wa kujengwa kwa skimu ya umwagiliaji iliyokamilika au inayosubiri kupata pesa.

 

Pia katika taarifa ya DASIP ya 2011/2012 iliyotolewa Januari 2012 hakuoneshwa mradi wa ujenzi wa skimu ya umwagiliaji katika vijiji hivyo.

 

Katika taarifa kwa madiwani hao, ilisisitizwa kuwa fedha hizo zilitumika kuendeshea mafunzo kwa wakulima na nyingine zilipelekwa kijijini kwenye mradi wenyewe ili kuendeleza ujenzi wa mradi huo.

 

Katibu wa Wakulima wa Kamati ya Mradi huo, Abel Katemi, anasema kwamba wao kama kikundi cha wakulima ambao ndiyo wanaosimamia ujenzi wa mradi huo, hawajawahi kupokea kiasi chochote cha fedha kwa ajili ya ujenzi wa bwawa au lambo.

 

“Ninachokifahamu ni kwamba Ofisa Kilimo na Mifugo wa Wilaya ya Geita alikuja akatupa mafunzo ya siku saba kwa kikundi chetu chenye wanachama 15 na kila mmoja alilipwa shilingi elfu kumi tu, labda kama hiyo ndiyo wanayosema walitumia shilingi milioni mia mbili za kujenga skimu,” anasema.

 

Mwenyekiti wa Kijiji cha Nyamboge, Fugo Ablaisus (63), anasema kuwa yeye hana taarifa ya kujengwa kwa mradi huo wa umwagiliaji, bali anachokumbuka ni semina ya siku saba aliyohudhuria kufundishwa namna ya kuendesha mradi huo.

 

Anasema kwamba yeye alisikia taarifa kutoka kwa Mwenyekiti wa Mkoa wa Geita wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Joseph Musukuma, ambaye pia ni Diwani wa Kata ya Nzera, kwamba Sh milioni 200 zilishalipwa na Halmashauri ya Geita, na kuwa skimu ilishajengwa.

 

Diwani wa Kata ya Katoma, Komanya, anasema, “Sijawahi kupata taarifa yoyote ya kuwapo mradi wa umwagiliaji katika kata yangu, kama upo basi ni mradi hewa na hiyo pesa watakuwa wamelipana wao wenyewe, maana kama pesa ingeingia kwenye akaunti ya kijiji ningejua. Mkurugenzi angeniandikia barua kunijulisha ujio wa pesa hizo, lakini hakuna pesa iliyowahi kuja kwa ajili ya mradi huo.”

 

Pamoja na Halmashauri hiyo katika vikao mbalimbali vya Baraza la Madiwani kupitisha matumizi ya Sh milioni 200 kujenga mradi wa skimu ya umwagiliaji, na matumizi ya zaidi ya Sh milioni 135.5 kwa upembuzi na semina, mwaka huu wa fedha wa 2013/2014 imetenga Sh milioni 32.5 kwa ajili ya mafunzo kwa wakulima wale wale ambao walishafundishwa kwa kutumia Sh milioni 135.5.

 

Utafiti wa mwandishi wa makala haya unaonesha kuwa mwaka 2011 kikundi cha wakulima wa vijiji vya Nyamboge na Nzera chenye wakulima 15 kilitumia Sh milioni 135.5 katika semina ya kujengewa uwezo, lakini mwaka huu wa fedha 2013/2014 wakulima 300 katika vijiji 20 watatumia Sh milioni 31.5 tu kwenye semina ya kuwajengea uwezo; chanzo cha fedha kikiwa ni DASIP.

 

Pia Halmashauri hiyo imepitisha Sh milioni 39.2  kwa ajili ya kusajili vikundi 20 vya wakulima kikiwamo Kikundi cha Wakulima cha Nyamboge-Nzera ambacho kilishasajiliwa na Wizara ya Mambo ya Ndani mwaka 2011.

 

Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Geita, Ali Kidyaka, alipotakiwa kutoa maelezo juu ya mkanganyiko uliopo juu ya matumizi ya fedha hizo na mradi kutokuwapo, alisema kuwa yeye wakati huo hakuwapo, hivyo anahitaji muda ili afuatilie.

 

“Mwaka 2011 sikuwapo Geita, sijui kilichofanyika juu ya mradi huo na miradi mingine, nipe muda nifuatilie ili nijiridhishe,” anasema.

Please follow and like us:
Pin Share