* Akodi vijana, wavunja nyumba, watembeza mkong’oto

* Baba mwenye nyumba atekwa, atelekezwa porini

* Watu 17 wakosa makazi

Vilio, simanzi na huzuni vimetawala katika Kitongoji cha Shinde, Kijiji cha Buhalahala, Kata ya Kalangalala wilayani Geita, kufuatia familia moja katika eneo hilo yenye watu 17 wakiwamo watoto wachanga, kukosa makazi baada ya makazi yao kubomolewa.

Makazi ya Damas Masasila (56) na familia yake yalibomolewa na kundi la vijana waliokodiwa na mfanyabiashara mmoja wa mjini hapa, chini ya usimamizi wa mtendaji wa mtaa huo, hatua inayodaiwa kuwa ni nia ya kutaka kupora eneo hilo ajenge hoteli ya kitalii.

 

Kitongoji hicho cha Shinde kimepakana na Msitu wa Hifadhi wa Buhalahala, nje kidogo ya mji wa Geita, wenye wanyama hatari kwa binadamu wakiwamo fisi.

 

Inadaiwa mfanyabiashara huyo, Mesenja Mayanda, ametenda unyama huo kutokana na jeuri ya fedha aliyonayo, ikiwa ni pamoja na kuwatumia baadhi ya vigogo wa Serikali wilayani hapa kutekeleza uporaji wa eneo hilo akilenga kujenga hotel ya kitalii.

 

Kitendo hicho kimeiacha familia hiyo katika mazingira yanayoilazimu kulala nje katika eneo linalozungukwa na wanyama kama fisi, ambao kwa siku za karibuni wameripotiwa kula watoto kadhaa wenye umri wa chini ya miaka mitano.

 

Mbali ya genge hilo la vijana 10 waliokodiwa na mfanyabiashara huyo likiongozwa na Ofisa Mtendaji wa Mtaa wa Shinde, Mathias Mbassa, kubomoa nyumba nne za mkazi huyo, pia linadaiwa kupora fedha zaidi ya Sh milioni mbili, kutembeza mkong’oto na kuwadhalilisha baadhi ya mabinti wa mzee huyo kwa kuwatomasatomasa sehemu mbalimbali za miili yao yakiwamo matiti.

 

Imeelezwa kuwa siku ya tukio hilo, Agosti 3, mwaka huu, saa tano asubuhi, kabla ya vijana hao kuanza kubomoa makazi hayo, walimteka Masasila wakamfunga mikono na miguu na kumfungia ndani ya gari aina ya Hiace ili asione udhalilishaji wanaofanyiwa binti zake kabla ya kusambaratisha makazi yake kwa kutumia nyundo kubwa na vipisi vya nondo.

Baba wa familia asimulia

 

Akizungumza na mwandishi wa habari hizi aliyefika eneo la tukio hilo, Masasila ambaye ni mlezi wa familia hiyo na mhanga wa tukio zima, alidai kuwa siku ya tukio kundi la vijana wapatao 10 liliingia ghafla nyumbani kwake na kabla ya kuhoji kulikoni, alijikuta amepigwa kabari (tanganyika jeki) na kutolewa nje alikoanza kupigwa bila kujua kosa lake.

 

“Nilipotolewa nje huku nikishambuliwa nilifungwa kamba miguu na mikono, wengine walinipiga kwenye vikombe vya miguu, wengine walikuwa wananipiga makofi na mateke na wengine walinichapa fimbo.

 

“Kwa kweli siku hiyo mke na watoto wangu walilia sana kuona unyama ninaotendewa mbele yao, na hata nilipojaribu kuhoji kosa langu hawakunijibu. Kwa kweli nilipigwa sana na baadaye walinibeba juujuu na kwenda kunifungia kwenye gari aina ya Hiace iliyowaleta.

 

“Nikiwa kwenye gari hiyo nilikuwa nasikia vishindo lakini sikutambua vinakotokea, nilikuja kujua baadaye majira ya mchana baada ya kurejea nyumbani na kukuta nyumba zote nne tulizokuwa tukiishi zimebomolewa na vijana hao.

 

“Ni hivi ndugu mwandishi, wao baada ya kumaliza kubomoa makazi yangu walikuja lilipo gari kisha kuliondoa eneo hilo na baadaye wakanipeleka kunitupa porini kwenye Msitu wa Hifadhi wa Buhalahala wakijua nikilala huko nitaliwa na fisi, lakini haikuwa hivyo kwani baada ya kunitelekeza msituni nilijivingirisha huku nikipiga makelele, ndipo baadaye wasamaria wema waliniokoa na baada ya kurejea nyumbani nikakuta hali hiyo,” alisema Masasila.

 

Alipohojiwa iwapo kwenye kundi hilo la vijana wa mfanyabiashara huyo kuna aliowatambua, Masasila alikiri kuwatambua Ofisa Mtendaji wa mtaa wao, Mathias Mbassa, na Mesenja Mayanda, mfanyabiashara aliyedaiwa pia kwamba alipata kupora shamba lake kwa kuwatumia baadhi ya vigogo wa Serikali akiwamo Mtendaji Mbassa.

 

“Niliowatambua ni Mtendaji wa Mtaa wetu, Mbassa, na mfanyabiashara Mayanda maana hili sasa ni tukio la pili kwani miaka ya nyuma huyu mfanyabiashara aliwahi kunipora mbuga ya kulima mpunga, na kama unavyoona hali yetu ya umaskini, niliamua kusamehe nikiogopa kufia jela maana baadhi ya viongozi wa Serikali walinionya niache kupambana na mwenye fedha nitafia jela, hivyo nikamuachia shamba lote, kumbe ndiyo nilikuwa nakaribisha balaa zaidi,” alisema.

 

Maelezo ya mama wa familia

Meleciana Ndalahwa, mke wa Masasila na  mama wa familia hiyo anasema: “Yaani baba sijawahi kuona vijana wanyama kama wale… maana kipigo walichompa mume wangu utadhani hatuko kwenye nchi yetu, toka mwaka 1985 tunaishi hapa hatujawahi kudhulumu cha mtu lakini mtu kwa fedha zake anamdhalilisha mume wangu, mimi na watoto bila sababu.

 

“Sikutegemea kama ningemuona tena, nilijua mwisho wake ulikuwa huo… mimi na wanangu tulilia sana pasipo msaada wowote na baadaye wakaenda kumfungia kwenye gari akiwa amefungwa miguu na mikono.

 

“Waliporudi  waliingia ndani ya vyumba na kuanza upekuzi na kibaya zaidi waliwadhalilisha mabinti zangu waliokuwa ndani kwa kuwashikashika sehemu mbalimbali za miili na baadaye walitufukuza eneo hilo wakaanza kuvunja nyumba moja baada ya nyingine kama unavyoona… tulilia sana na hata tuliposogea kuwazuia tulipigwa sana, mwishowe tukaamua kumuachia Mungu.

 

“Walitoboatoboa masufuria ya kupikia, walitoboatoboa mabati tuliyokuwa tumeezekea nyumba zetu, walivunja vyungu vya kupikia, kulikuwa na pesa tulizokuwa tumeuza mpunga kiasi cha shilingi milioni 2.6 nazo wakabeba… wakachanachana madaftari ya shule ya watoto, yaani sijui walikuwa wamevutishwa bangi.

 

“Baada ya kumaliza kubomoa makazi yetu yule tajiri [Mayanda] alichomoa mahela mengi na kuanza kuwagawia wale vijana na nyingine akampa Mtendaji Mbassa na kumtaka ahakikishe tunahama hapa, baadaye waliondoka na mume wangu.

 

“Walituambia eneo hilo si mali yetu tena, wakatuahidi wangerudi usiku wa siku hiyo na kama wangetukuta wangetubaka lakini hatujawaona tena tunaomba Serikali itusaidie kwani tuna watoto wachanga, kuendelea kulala nje wanaweza kupata magonjwa ya baridi (nimonia) na hata kuliwa na fisi wakati tumelala maana huku fisi ni wengi na wanakula watu,” alisema Ndalahwa.

 

Watoto waililia Serikali

Baadhi ya watoto wa Masasila akiwamo Grace (14), Happynes (16) wanaosoma darasa la saba, Laurent (12) darasa la tano, Emanuel (10) na Chausiku Damas (7) wanaosoma darasa la tatu na Lameck Jeremiah (10) wa darasa la kwanza katika Shule ya Msingi Buhalahala, wameiomba Serikali kuingilia kati mgogoro huo ikiwa ni pamoja na kuwapa mahema ya kujihifadhi ili waendelee na shule, na kwamba tangu siku ya tukio wamesimama masomo.

 

Mwenyekiti wa mtaa anena

Mwenyekiti wa Mtaa wa Shinde, Thomas Luzaria, amemwambia mwandishi wa habari hizi kwamba mbali ya kusikitishwa na tukio hilo, ameiomba Serikali kuwadhibiti na kuwachukulia hatua kali matajiri ambao wamekuwa wakiutumia vibaya utajiri walionao sambamba na kuwawajibisha baadhi ya vigogo wanaosahau wajibu wa kuwatumikia wananchi ambao ndiyo waajiri wao na kuwa vibaraka wa matajiri.

 

Mtendaji naye azungumza

Hata hivyo, katika hali ya kushangaza Ofisa Mtendaji wa Mtaa wa Shinde, Mathias Mbassa, anayedaiwa ‘kuwekwa mfukoni’ na mfanyabiashara huyo, alipopigiwa simu, mbali ya kukiri kufanya unyama huo alimwomba mwandishi kukutana naye kwa lengo la kumziba mdomo.

 

“Sikiliza ndugu yangu… ni kweli tumefanya hivyo kwa kibali maalum, sasa sikiliza usiandike kwanza hiyo habari…uko wapi nije ndugu yangu tutayamaliza tu,” alisikika akijitetea kwa mwandishi bila mafanikio.

 

Mfanyabiashara ang’aka

Kwa upande wake, mfanyabiashara huyo Mesenja Mayanda, baada ya kupokea simu na kugundua aliyepiga ni mwandishi wa habari, haraka alijibu: “Siongei na wewe mimi naongea na mwenye mbwa,” akakata simu.

 

Polisi wanena

Ofisa mmoja wa Jeshi la Polisi ambaye hakutaka jina lake liandikwe gazetini kwa kuwa si msemaji wa jeshi hilo, alikiri kuwa na taarifa za tukio hilo na kuongeza kuwa watuhumiwa wote wanatafutwa kwa shambulio la kudhuru mwili na kwamba jarada la uchunguzi: GE/RB/6077/13 limekwisha kufunguliwa.

1181 Total Views 2 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!