Mfanyabiashara Lodrick Uronu, ameingia katika mgogoro wa kisheria akituhumiwa kuvunja nyumba iliyopo katika kiwanja Na. 23 Mtaa wa Sokoni, Manispaa ya Moshi bila kuwa na amri halali ya korti.

Nyumba hiyo mali ya marehemu Mwanaisha Suleiman na Zubeda Suleiman, ipo katika mgogoro wa kifamilia wa nani hasa msimamizi halali wa mirathi ya mali za marehemu hao kutokana na kuwapo mvutano.

Nyaraka mbalimbali ambazo JAMHURI imeziona zinaonesha kuwa nyumba hiyo iliuzwa kwa Uronu mwaka 2009 na mtu aitwaye Lucy Edward Lema kwa malipo ya Sh milioni nane huku kukiwapo kesi mahakamani inayohusu mirathi. Uchunguzi umebaini kuwa katika kikao cha Novemba 11, 2005 kilichohusisha ukoo wa Lema; Lucy Nanga aliteuliwa kuwa msimamizi wa mirathi hiyo; na si Lucy Edward Lema aliyeuza nyumba hiyo.

Hata hivyo, mfanyabiashara huyo ameliambia JAMHURI kuwa ana nyaraka zote zinazomhalalisha yeye kuwa mmiliki wa nyumba hiyo na hati ya mauziano kati yake na Lucy Lema.

Akizungumza na JAMHURI, Aisha Lema ambaye mwaka 2007 alithibitishwa na Mahakama ya Mwanzo kuwa msimamizi wa mirathi namba 162/2007na kuendesha kesi ya kupigania haki hiyo   kwa mwaka wa tisa sasa, amesema nyumba hiyo imevunjwa bila uhalali wowote kisheria.

Anadai kuwa Mei 19, 2011 Naibu Msajili wa Mahakama Kuu Kanda ya Moshi alimpa haki mfanyabiashara huyo ya kuwaondoa watu waliokuwa wakiishi kwenye nyumba hiyo.

Hata hivyo, anasema baada ya barua hiyo ya Msajli ya Julai 25, 2011 alimwandikia barua Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu – Kanda ya Moshi, Stella Mugasha akilalamikia hatua ya kupokwa nyumba hiyo bila uhalali wowote kisheria.

Kutokana na malalamiko hayo, Jaji Mugasha alitengua barua hiyo ya msajili kutokana na kile kilicholelezwa kuwa ilikuwa ya kiutawala na haikuwa amri halali ya mahakama.

Jaji Mugasha alisisitiza katika barua yake ya Julai 26, 2011 kwenda kwa msajili kwa kueleza kuwa, mtu yeyote asivunje nyumba hiyo bila kuonesha amri halali iliyotolewa na mahakama ya kuvunja nyumba hiyo.

“Baada ya kupitia kumbukumbu za majalada kuhusiana na nyumba husika, hakuna amri halali yoyote ya mahakama inayomhalalisha Lodrick Emmanuel Oronu kumwondoa Aisha Juma Lema kutoka katika nyumba iliyopo ploti na. 23 Block K section III bondeni Moshi,” inaeleza barua hiyo.

Barua hiyo ya Jaji Mugasha iliyokuwa ikijibu malalamiko ya Aisha Juma Lema, ilitoa maelekezo ya kufuatwa ikiwamo kumpa taarifa mlalamikaji (Aisha) kuwa mtu yeyote atakayetaka kumwondoa katika nyuymba hiyo, sharti ampatie amri halali ya mahakama.

Ikaelekezwa pia kuwa barua hiyo inakiliwe kwa RPC – Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kilimanjaro, msajili wa hati, Mkurugenzi Manispaa ya Moshi, Lucy Lema na Ofisi ya Mtendaji wa Kata.

“Majembe Auction Mart waandikiwe barua kuonywa kutokiuka maadili ya kazi ya udalali kwa kuegemea barua ya kiutawala kama amri halali ya Mahakama na kumtisha Aisha Juma Lema wakati wanafamu kuwa si sahihi,” inasema sehemu ya barua hiyo.

Jaji Mugasha alieleza kuwa barua ya Msajili ni barua ya kiutawala tu na si amri halali ya Mahakama; na kwa sababu hiyo haimhalalishi Uronu kumwondoa Aisha kutoka kwenye nyumba tajwa.

 

Nyumba yabomolewa

Pamoja na onyo hilo, mwezi uliopita, mfanyabaishara huyo akiitumia kampuni ya udalali ya Lonzadu, kundi la vijana wapatao 50  pamoja na polisi waliosheheni silaha za moto na mabomu ya kutoa machozi, waliizingira nyumba hiyo alfajiri na kuiboa huku mali za watu zikifukiwa humo bila huruma na bila wahusika kuonesha amri ya mahakama.

Mfanyabiashara huyo aliegemea kwenye barua ya msajili ya Mei 19 ya 2011 ambayo hata hivyo ilifutwa na barua ya Jaji Mugasha kutokana na kutokuwa amri halali ya mahakama.

Wakati wa utekelezaji wa zoezi hilo, familia iliyokuwa ikiishi kwenye nyumba hiyo wakiwamo wapangaji waliokuwa wakiendesha biashara zao kwenye nyumba hiyo, hawakupewa hati ya kusudio la kuondolewa katika nyumba hiyo.

Kabla ya kuvunjwa kwa nyumba hiyo, Ofisa Mtendaji wa Kata ya Bondeni ilipo nyumba hiyo, J. Mmonyo, alitoa zuio la kutovunjwa nyumba hiyo kutokana na kampuni hiyo ya udalali kushindwa kuonyesha amri halali ya mahakama.

“Baada ya kupitia vielelezo kutoka upande wa pili nimeridhika kwamba huna uhalali wowote kwa sasa wa kuvunja nyumba hiyo kwani taratibu kadhaa za kisheria hazikufuatwa,” inasema barua hiyo ya Novemba 2, 2015.

 

Udanganyifu

Oktoba 18, mwaka huu, mfanyabiashara huyo aliiandikia barua Manispaa ya Moshi akiomba kupewa kibali cha kuivunja nyumba hiyo kwa madai kuwa ni mbovu, chakavu na haikuwa inafaa kwa maisha ya binadamu na shughuli zake.

Kutokana na ombi hilo, Manispaa hiyo ilimpa kibali mfanyabiashara huyo cha kuivunja nyumba hiyo kupitia barua ya Novemba 2, mwaka huu iliyosainiwa na Niki Kimaro kwa niaba ya Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri hiyo. Kwa upande wake, ofisa huyo wa manispaa ameliambia JAMHURI kuwa walimpa kibali cha kuvunja nyumba hiyo baada ya mfanyabiashara huyo kuwasilisha nyaraka muhimu zinazohusiana na nyumba hiyo ikiwamo hati ya nyumba na hukumu ya mahakama.

 

Sakata latinga Takukuru

Kutokana na mkanganyiko huo, sakata hilo sasa limetinga mikononi mwa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa nchini (Takukuru) kwa ajili ya uchunguzi na taarifa za awali za ndani ya taasisi hiyo zimedhibitisha kuwa upo ‘mchezo’ mchafu katika suala hilo.

Kamanda wa Takukuru Mkoa wa Kilimanjaro (RBC), Alexander Kuhanda, amedhibitsha sakata la nyumba hiyo kuvunjwa kutinga ofisini kwake alipotetea na waandishi wa habari hivi karibuni, lakini kutokana na kubanwa na kanuni na maadili ya kazi yake, hakuweza kulitolea ufafanuzi zaidi.

Kutinga Takukuru sakata hilo kunatokana na barua ya malalamiko ya Aisha Juma Lema kwa taasisi hiyo ya Novemba  4, mwaka huu akilalamikia kile alichokiita kuvunjiwa nyumba yake, kuporwa mali zake na kudhalilishwa.

By Jamhuri