Said Bakhresa asalimu amri

bakhresaKampuni ya Said Salum Bakhresa imelipa kwa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) dhamana ya Sh bilioni 4.2 kama sehemu ya kuwabana wafanyabiashara waliokwepa kulipa kodi ya makontena zaidi ya 300 yaliyopotea kwenye Bandari Kavu (ICD) ya Azam inayomilikiwa na bilionea Said Bakhresa (pichani).

Taarifa zilizopatikana kutoka TRA zinasema nusu ya kiwango hicho kililipwa na Bakhresa Novemba 20, mwaka huu, na wiki iliyopita kiwango kama hicho kililipwa katika Mamlaka hiyo.

Pamoja na Bakhresa, kampuni zenye makontena ambazo hadi mwishoni mwa wiki iliyopita zilikuwa zimelipa kodi iliyokwepwa ni Tuff Tyres Center iliyolipa Sh bilioni moja Desemba 2, mwaka huu; Binslum Tyres iliyolipa Sh bilioni 1.4 mnamo Desemba 2; na kulipa kiasi kingine cha Sh bilioni 1.151 Desemba 3, mwaka huu; na Kiungani Trading imelipa Sh milioni 506.728.

Desemba 3, mwaka huu Rais John Magufuli, aliwapa wafanyabiashara siku saba wawe wamelipa kodi zote wanazodaiwa. Alisema ambaye angekiuka agizo hilo, sheria zingechukuliwa dhidi yake.   

Msemaji wa Kampuni ya Said Salim Bakhresa, amesema makontena yote yaliyopotea kwenye ICD ya Azam hayamilikiwi na kampuni hiyo.

Msemaji huyo, Hussein Sufiani anasema: “Siku ile Waziri Mkuu Mheshimiwa Majaliwa Kassim amefanya ziara ya kwanza pale bandarini na kupewa taarifa juu ya makontena 349 na thamani yake ni Sh bilioni 80, sisi tulitajwa.

“Ukweli ni kwamba makontena yaliyopotea katika bila kulipiwa kodi ni 329. Ni kweli kwamba hayo makontena 329 yalipotea katika Bandari Kavu ya Azam na thamani ya kodi yake ni Sh bilioni 12.6. lakini kati ya hayo, hakuna hata moja ambalo ni mali ya Azam. Hiyo fact (kweli) kabisa.

“Makontena hayo ni ya makampuni 10 ambayo TRA imetangaza wazi kuwa wamiliki wake wameanza kulipia kodi kwa mfano Bin Slum amelipa kodi yote. Sasa kwanini yalikuwa kwenye ICD ya Azam? Sisi ndiyo tuliyoyadhamini makapuni hayo.

“Kwa mujibu wa taratibu sisi guarantor (wadhamini) tunatakiwa ku-deposit (kuweka) kiasi hicho cha fedha katika akaunti ya Mamlaka ya Mapato (TRA) ili inapotokea wenye makontena hawajalipa kodi, basi mdhamini anawajibika kukatwa kiasi cha fedha kulingana na thamani ya kontena.

“Kati ya Sh bilioni 21.6 sisi tayari tume-deposit Sh bilioni 4.2, lakini uzuri ni kwamba wenye makontena wanalipa wakiwamo hawa wa Tybat Trading na Bin Slum. Ni matumani yetu kwamba kabla ya tarehe iliyotangazwa na Rais Magufuli, watakuwa wamelipa.

“Baada ya uchunguzi na kuridhika kwamba tumefuata taratibu TRA wenyewe wametuandikia barua kutuambia kwamba wameifungulia Bandari Kavu yetu maana waliifunga. Hii ni baada ya kutoa ushirikiano ambao umewaridhisha TRA na Serikali.

“Azam ni kampuni ya kizalendo, tunalipa kodi. Hatuwezi kushindwa kulipa kodi. Halafu jingine ni kwamba kampuni zetu zote zimesajiliwa huku Tanzania Bara, kule Visiwani tumesajili Azam Marine na Azam Diary, ile ya maziwa. Kwa hiyo sisi wazalendo bwana na ni miongoni mwa walipa kodi wakubwa.”