Na Deodatus Balile

Kwa muda mrefu ninapokuwa safarini huangalia jambo la kurejea nalo nyumbani. Nimesafiri nchi kadhaa duniani, hivyo nashukuru Mungu kuwa kusafiri huko kumeniongezea uelewa. Katika nchi nyingi, iwe zilizoendelea au zinazoendelea, zimeweka mtazamo na msisitizo mpya katika miundombinu.
Nchi nyingi zimebaini kuwa maendeleo ya kweli yanatokana na urahisi wa mawasiliano (Teknohama), miundombinu – barabara, reli, magati ya majini, viwanja vya ndege na njia nyingine za usafirishaji. Kubwa wanalolifanya ni kuhakikisha miundombinu inayotengenezwa inapitika. Haina vizuizi (bottlenecks).

Sitanii, kabla sijaendelea nizungumzie uzinduzi wa Daraja la Juu la Tazara, Dar es Salaam lililoitwa Mfugale Flyover. Kitambo makutano ya TAZARA yamekuwa kero. Si kwa ajali tu, bali foleni pia. Kwa wasafiri wa kwenda Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere wanaowahi ndege za mchana kama Emirates inayokwenda Dubai na Guangzhou au ATCL inayokwenda Mbeya mchana, TAZARA ilikuwa pasua kichwa.
Mara mbili au zaidi nusura nichelewe ndege ya kwenda Mbeya mwaka juzi na mwaka jana. Tena ndege yenyewe unacheleweshwa Fastjet. Hawa jamaa ukichelewa hata dakika mbili, nauli yote inapotea. Naamini si mimi peke yangu, ila foleni ya TAZARA ilikuwa hatari na moto wa kuotea mbali.

Sitanii, wiki mbili tangu daraja la TAZARA lianze kutumika nimepata burudani kubwa. Foleni imepungua kwa kiwango cha kutisha. Unaweza kusema foleni imekwisha. Rais John Magufuli wakati anazindua daraja la TAZARA alilolipa jina la Mfugale, Septemba 27, mwaka huu, amesema foleni inagharimu uchumi wa Tanzania wastani wa Sh bilioni nne kwa mwezi.
Wapo wanaoonyesha kuwa gharama hii inaweza kufikia Sh bilioni 200 kwa mwaka. Hapa kinachojitokeza ni kuwa hatuna utaratibu rasmi wa kutunza takwimu, lakini kama mtu anatoka nyumbani saa 11 alfajiri, halafu akafika ofisini saa 3 asubuhi, hapo kuna gharama kubwa zaidi ya mafuta.
Jambo kubwa ninalolizungumza hapa ni utamaduni wa kujiandaa kama taifa kuwa na miundombinu inayotabiri ukuaji wa uchumi. Mwaka 2000 wakati nahama kutoka Buguruni kwenda Kitunda, Barabara ya Nyerere haikuwa na matuta na ungeweza kukaa dakika 20 ndipo lipite gari jingine.

Leo hadi inajengwa flyover ya TAZARA barabara hii ilikwisha kugeuka janga. Nampongeza Rais Magufuli kwa ujenzi wa daraja hili. Nimemsikia akisema kuwa zitajengwa flyover pale Ubungo, DIT Temeke, Kamata na maeneo mengine. Ujenzi huo ni faraja. Tena niongeze jingine. Ujenzi huo uendane na kasi ya kujenga madaraja ya waenda kwa miguu.
Wiki ambayo Rais Magufuli amezindua daraja, kuna watu kwa mawazo yao pale Kipawa (Uwanja wa Ndege) wakaweka matuta yenye ncha kali. Foleni ikawa kubwa kuliko kabla ya uzinduzi wa daraja. Nadhani nao wameona aibu, maana Ijumaa wameyarekebisha matuta. Sasa tuhame kwenye matuta. Kila barabara inapojengwa tuweke madaraja ya waenda kwa miguu.

Sitanii, katika miji mipya mingi kama huko China, Ulaya na Amerika kwa sasa ni sera. Hata majirani zetu wa Kenya na Uganda wameziona. Kila inapojengwa barabara kwa kiwango cha lami, makutano yote lazima zijengwe flyover na madaraja ya waenda kwa miguu. Siyo tusubiri barabara ikisha kuzinduliwa, tuanze tena kuvunja kujenga flyover au daraja la waenda kwa miguu!
Mwaka 2004 tukiwa katika Hoteli ya New Africa, Dar es Salaam, wakati huo Rais Magufuli akiwa Waziri wa Ujenzi, nilimuuliza kwa nini hatujengi flyover? Wakati huo alinijibu hivi: “Balile, huko kwenu Wazira Nkende hawana barabara za lami, leo tuanze kujenga flyover? Hii si kipaumbele kwa sasa.”

Sitanii, Rais Magufuli ikiwa wakati ule suala la flyover halikuwa kipaumbele cha taifa letu, nakuomba sasa liwe kipaumbele katika miji yote mikubwa nchini na hata huko Makao Makuu Dodoma, kwani bila kufanya hivyo tutatengeneza msongamano wa magari na kupoteza gharama kubwa kama ilivyokwisha kuanza kujitokeza hapa nchini. Hongera pia Injinia Patrick Mfugale kwa utumishi wako kutambuliwa pia.

By Jamhuri