Na Deodatus Balile

Kwa muda mrefu ninapokuwa safarini
huangalia jambo la kurejea nalo nyumbani.
Nimesafiri nchi kadhaa duniani, hivyo
nashukuru Mungu kuwa kusafiri huko
kumeniongezea uelewa. Katika nchi nyingi, iwe
zilizoendelea au zinazoendelea, zimeweka
mtazamo na msisitizo mpya katika
miundombinu.
Nchi nyingi zimebaini kuwa maendeleo ya kweli
yanatokana na urahisi wa mawasiliano
(Teknohama), miundombinu – barabara, reli,
magati ya majini, viwanja vya ndege na njia
nyingine za usafirishaji. Kubwa wanalolifanya ni
kuhakikisha miundombinu inayotengenezwa
inapitika. Haina vizuizi (bottlenecks).
Sitanii, kabla sijaendelea nizungumzie uzinduzi
wa Daraja la Juu la Tazara, Dar es Salaam
lililoitwa Mfugale Flyover. Kitambo makutano ya
TAZARA yamekuwa kero. Si kwa ajali tu, bali

foleni pia. Kwa wasafiri wa kwenda Uwanja wa
Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere
wanaowahi ndege za mchana kama Emirates
inayokwenda Dubai na Guangzhou au ATCL
inayokwenda Mbeya mchana, TAZARA ilikuwa
pasua kichwa.
Mara mbili au zaidi nusura nichelewe ndege ya
kwenda Mbeya mwaka juzi na mwaka jana.
Tena ndege yenyewe unacheleweshwa Fastjet.
Hawa jamaa ukichelewa hata dakika mbili, nauli
yote inapotea. Naamini si mimi peke yangu, ila
foleni ya TAZARA ilikuwa hatari na moto wa
kuotea mbali.
Sitanii, wiki mbili tangu daraja la TAZARA
lianze kutumika nimepata burudani kubwa.
Foleni imepungua kwa kiwango cha kutisha.
Unaweza kusema foleni imekwisha. Rais John
Magufuli wakati anazindua daraja la TAZARA
alilolipa jina la Mfugale, Septemba 27, mwaka
huu, amesema foleni inagharimu uchumi wa
Tanzania wastani wa Sh bilioni nne kwa mwezi.
Wapo wanaoonyesha kuwa gharama hii
inaweza kufikia Sh bilioni 200 kwa mwaka.
Hapa kinachojitokeza ni kuwa hatuna utaratibu
rasmi wa kutunza takwimu, lakini kama mtu
anatoka nyumbani saa 11 alfajiri, halafu akafika
ofisini saa 3 asubuhi, hapo kuna gharama
kubwa zaidi ya mafuta.
Jambo kubwa ninalolizungumza hapa ni
utamaduni wa kujiandaa kama taifa kuwa na

miundombinu inayotabiri ukuaji wa uchumi.
Mwaka 2000 wakati nahama kutoka Buguruni
kwenda Kitunda, Barabara ya Nyerere haikuwa
na matuta na ungeweza kukaa dakika 20 ndipo
lipite gari jingine.
Leo hadi inajengwa flyover ya TAZARA
barabara hii ilikwisha kugeuka janga.
Nampongeza Rais Magufuli kwa ujenzi wa
daraja hili. Nimemsikia akisema kuwa
zitajengwa flyover pale Ubungo, DIT Temeke,
Kamata na maeneo mengine. Ujenzi huo ni
faraja. Tena niongeze jingine. Ujenzi huo
uendane na kasi ya kujenga madaraja ya
waenda kwa miguu.
Wiki ambayo Rais Magufuli amezindua daraja,
kuna watu kwa mawazo yao pale Kipawa
(Uwanja wa Ndege) wakaweka matuta yenye
ncha kali. Foleni ikawa kubwa kuliko kabla ya
uzinduzi wa daraja. Nadhani nao wameona
aibu, maana Ijumaa wameyarekebisha matuta.
Sasa tuhame kwenye matuta. Kila barabara
inapojengwa tuweke madaraja ya waenda kwa
miguu.
Sitanii, katika miji mipya mingi kama huko
China, Ulaya na Amerika kwa sasa ni sera.
Hata majirani zetu wa Kenya na Uganda
wameziona. Kila inapojengwa barabara kwa
kiwango cha lami, makutano yote lazima
zijengwe flyover na madaraja ya waenda kwa
miguu. Siyo tusubiri barabara ikisha

kuzinduliwa, tuanze tena kuvunja kujenga
flyover au daraja la waenda kwa miguu!
Mwaka 2004 tukiwa katika Hoteli ya New Africa,
Dar es Salaam, wakati huo Rais Magufuli akiwa
Waziri wa Ujenzi, nilimuuliza kwa nini hatujengi
flyover? Wakati huo alinijibu hivi: “Balile, huko
kwenu Wazira Nkende hawana barabara za
lami, leo tuanze kujenga flyover? Hii si
kipaumbele kwa sasa.”
Sitanii, Rais Magufuli ikiwa wakati ule suala la
flyover halikuwa kipaumbele cha taifa letu,
nakuomba sasa liwe kipaumbele katika miji
yote mikubwa nchini na hata huko Makao
Makuu Dodoma, kwani bila kufanya hivyo
tutatengeneza msongamano wa magari na
kupoteza gharama kubwa kama ilivyokwisha
kuanza kujitokeza hapa nchini. Hongera pia
Injinia Patrick Mfugale kwa utumishi wako
kutambuliwa pia.

Ends…

Please follow and like us:
Pin Share