OKTOBA 2, mwaka huu Mfuko wa Pensheni wa PPF ulifanya mkutano wa 23 wa mwaka wa wanachama na wadau ambao uliofanyika mkoani Arusha.

Mkutano huo ulienda sambamba na kutimiza kwa miaka 35 tangu kuanzishwa kwake.  Katika mkutano huo ulihudhuriwa na wajumbe zaidi ya 800 kutoka sehemu mbalimbali nchini.

 

Kikubwa ambacho kilijidhihirisha kwenye mkutano huo ni utendaji wa mfuko huo kuonekana kuigusa Serikali kutokana na mafanikio ambayo PPF imekuwa ikipata tangu kuanzishwa kwake.


Akitoa maelezo ya Mfuko huo, Makamu Mwenyekiti wa Bodi ya Wadhamini ya Mfuko wa PPF,Dkt. Aggrey Mlimuka, alisema mfuko huo unaadhimisha miaka 35 tangu kuanzishwa kwake ukiwa unaweza kutimiza majukumu yake ya kulipa mafao bila kulazimika kukopa au kuuza rasilimali zake.


Pia unafanya shughuli zake kwa asilimia 80 kwa kutumia teknohama  na kushiriki miradi mbalimbali ya uwekezaji yenye manufaa kwa Taifa.


Makamu Mwenyekiti wa Bodi ya wadhamini wa PPF alisema kwamba Mada kuu ya Mkutano wa mwaka huu  ulizingatia mchango mkubwa wa wanachama na wadau kufikisha miaka 35 ambapo alisema kauli mbiu ni   “PPF na Wadau: Miaka 35 ya kukua  pamoja.


Vilevile katika hotuba yake Dkt. Mlimuka alielezea jinsi  thamani ya Mfuko wa PPF ilivyokua kutoka sh. bilioni 894.5 mwaka 2012 hadi sh.trilioni 1.09 mwishoni mwaka 2012, ambapo ni ongezeko la asilimia 21.8.


Anasema hadi kufikia mwishoni mwa Juni, mwaka huu thamani ya Mfuko iliongezeka na kufikia sh. trilioni 1.29


Kwa upande wa idadi ya wanachama, Dkt.Mlimuka anasema imeendelea kuongezeka na kufikia  wanachama 203,981 mwishoni mwa mwaka 2012 kulinganisha na wanachama 180,049 mwishoni mwa mwaka 2011.


“Hadi mwishoni mwa Juni, mwaka huu (2013) wanachama wa PPF waliongezeka na kufikia 224,193


Kwa upande wa ukusanyaji wa Michango Mfuko wa Pensheni wa PPF uliendelea kukusanya jumla ya sh. bilioni 226.5 mwishoni mwa mwaka 2012, ikilinganishwa na sh. bilioni 187.5  zilizokusanywa mwaka 2011.”


Anaongeza kwamba katika kipindi cha miezi sita ya mwaka huu, jumla ya sh. bilioni 134.57 zimekusanywa, ambapo lengo ni kukusanya sh. bilioni 281.7 kufikia mwisho wa mwaka 2013.


“Mapato yatokanayo na uwekezaji yalipanda kwa asilimia 11.3 kutoka sh. bilioni 91.37 zilizopatikana katika mwaka 2011 hadi kufikia jumla ya sh. bilioni 115.15 zilizopatikana mwaka 2012.


Makamu Mwenyekiti aliendelea kwa kuelezea kwamba katika Uwekezaji wa Mfuko ulionaofanywa unazingatia miongozo iliyotolewa kwenye nyaraka za Sera ya Uwekezaji wa Mfuko, Sheria za Mfuko (PPF ACT),miongozo iliyotolewa na Benki Kuu ya Tanzania (BoT) kwa kushirikiana na Msimamizi wa Hifadhi ya Jamii.


Pia Mfuko huo, unawekeza kwa kufuata kanuni za uwekezaji ambazo ni usalama, uwezo wa kulipa, mapato manufaa ya kijamii.


Pia mafanikio hayo katika nyanja ya uwekezaji yametokana na uwekezaji katika maeneo ya mikopo, Hati Fungani za Serikali, Dhamana za Serikali,Hati Fungane za Mashirika,Akaunti za Muda Maalum, Hisa za Makampuni na uwekezjai wa mifuko ya pamoja kama vile UTT.


Eneo jingine ambalo limefanikisha mafanikio hayo ya PPF kwa upande wa uwekezaji, ni Mfuko kuwekeza hisa kwenye kampuni zilizoorodheshwa kwenye Soko la Mitaji (DSE) na yasiyoorodheshwa.


Mfuko wa PPF ndio Mfuko wa kwanza kuanzisha mikopo ya SACCOS kwa wanachama wake ambapo ilianza mwaka 2004 kwa lengo la kuwawezesha wanachama kuanzisha biashara na miradi kwa kupitia mikopo yenye riba nafuu.


Takwamu zinaonesha kuwa hadi kufikia Juni, mwaka huu sh. bilioni 56.45 zilikuwa zimeishatolewa kwa wanachama wa PPF na zinarejeshwa kwa wakati kupitia udhamini wa waajiri.


Jumla ya SACCOS zilizokwishanufaika na zinazoendelea kunufaika na mikopo hiyo ni 46. Pamoja na mafanikio hayo katika mwaka 2012 Mfuko ulikumbana na changamoto mbalimbali za uwekezaji na za kiutendaji yakiwemo malalamiko kutoka kwa wanachama juu ya kuchelewa uoanishaji wa vikokotoo vya malipo ya pensheni, kuchelewa kwa ufumbuzi juu ya fao la kujitoa (withdrawal).


Ucheleweshaji wa kuwasilisha michango, ya wanachama unaofanywa na baadhi ya waajiri. “Uchelewaji huu unaleta matatizo ya kiutendaji kwenye reconciliation; unasababisha Mfuko kushindwa kulipa kwa wakati na kuukosesha Mfuko fedha za uwekezaji,” anasema Dkt. Mlinuka.


Changamo nyingine kwa mujibu wa Dkt. Mlinuka, ni utoaji wa huduma ya Hifadhi ya Jamii katika Sekta isiyo rasmi, bado ni tatizo kwa jinsi sekta yenyewe isiyo rasmi ilivyo.


Kuhusu hatua ambazo zimekuwa zikichukuliwa na Mfuko kukabiliana na changamoto hizo ni pamoja na kuwasiliana na SSRA kuhusu suala la vikokotoo na lile la fao la kujitoa; kuwachukulia hatua waajiri wanaochelewesha michango na unafanya utafiti utakaoambatana na utoaji elimu kuhusu hifadhi ya jamii kwa sekta isiyo rasmi.


Akizungumza changamoto ya fao la kujitoa wakati wa mkutano huo, Naibu Waziri wa Kazi na Ajira, Dkt. Makongoro Mahanga, alisema watu wanaopigia debe fao la kujitoa kwenye mifuko ya hifadhi ya jamii ni kutokana na kutokuwa na elimu ya kuweka akiba pamoja na tamaa.


Anasema duniani kote pensheni ni kwa ajili ya uzeeni sio kwa ajili ya ujana, lakini kwa sasa inashangaza kuona leo hii watu wanapigania fao la kujitoa.


Anasema watu wanapenda fao la kujitoa kutokana na kutokuwa na utamaduni wa kujiwekea akiba na tamaa pale ya fedha wanapoona michango yao imekuwa mikubwa kwenye mifuko ya hifadhi ya jamii.


“Ni lazima tuwe wakweli, leo hii tuna wazee milioni 2.5 tunahangaika kuona tuwafanyeje…sasa tukiruhusu hawa waliowahi kufanyakazi wajitoe kwenye pensheni tutakuwa na shida ya wazee wengi ndani ya taifa hili,” anasema Dkt. Makongoro na kuongeza;


“Tuwe waangalifu tusikubali watu kujitoa kwenye mafao.


Mhadhiri katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM),Chris Mauki, alisema wengine wanaotaka kujitoa kwenye mafao maono yao hayaoni mbali.


“Ukitia aibu maisha yako ya leo, hata kesho siku ya msiba wako unaweza kutia aibu,”alisema Mauki.Aliwataka wafanyakazi na wananchi kwa ujumla kujenga utamaduni wa kujiandaa kwa ajili ya kesho badala ya kukimbilia kujitoa kwenye ya hifadhi ya jamii.

By Jamhuri