Kwenye anga za uchumi na biashara kumekuwa na changamoto inayojirudia kutoka kwa baadhi ya wasomaji kuhusu dhana ya ujasiriamali.

Licha ya wasomaji kuzikubali makala hizi lakini wamekuwa na walakini ikiwa inawezekana Watanzania wote tukawa wajasiriamali.  Hata mimi ninafahamu kuwa si watu wote wana ‘karama’ za kuwa wajasiriamali wa kibiashara.

Hata hivyo nimekuwa mwanaharakati wa kuhamasisha ujasiriamali wa kibiashara ili angalau Taifa lipate watu wa kutosha ambao wataanzisha biashara na kampuni. Ninaamini biashara na kampuni hizi zitakawaokoa maelfu ya wale wenye miito ya kuajiriwa wapate kazi. Hii ni kwa sababu Tanzania imefika mahali ambapo watengeneza ajira wamekuwa wachache kuliko wachukua ajira. Matokeo ya hali hiyo ni mrundikano wa nguvukazi isiyotumika.

Lakini hebu nifafanue dhana ya ujasiriamali; hapa nitatumia ufafanuzi wangu binafsi uliotokana na misingi ya wanazuoni wengi pamoja na uzoefu wangu binafsi katika biashara. Ujasiriamali ni kitendo cha mtu yeyote aliyepo mahali popote anayefanya kazi yoyote, kugundua ama kutambua hitaji ama upungufu katika eneo ama miongoni mwa watu.

Kisha kutumia ‘ubunifu’ wa kulitatua hitaji ama kurekebisha upungufu; na wakati huo huo akipata faida ya kifedha, kisifa, kicheo ama nyingine inayoendana na hiyo.

 

Kwa maana hii mjasiriamali anaweza kuwa mfanyabiashara, mfanyakazi, mama wa nyumbani, mwanafunzi, rais, mwandishi wa habari, kahaba na hata mchungaji au shehe. Hivyo basi utaona kuwa mfanyakazi anaweza kuwa mjasiriamali katika kazi yake, vile vile si kila mfanyabiashara ni mjasiriamali!

 

Kuna wafanyabiashara wengi sana ambao wanaendesha biashara kimazoea, hawana ‘ubunifu’ wa kutatua mahitaji ya watu ama kurekebisha upungufu katika soko.

Msingi wa ujasiriamali ni ‘uvumbuzi’ na ‘ubunifu’. Mfanyabiashara ambaye haendelezi ‘uvumbuzi’ na ‘ubunifu’ katika biashara zake huyo kiukweli hana sifa ya kuitwa mjasiriamali!

ukiona mfanyabiashara hana uvumbuzi ama ubunifu, basi ujue siku za uhai wa biashara yake zinahesabika.

 

Kutokana na mchanganyiko wa tafsiri ya ujasiriamali wanazuoni huweka makundi mawili kuwakilisha dhana hii; moja ikiwa ni ujasiriamali wa kibiashara (entrepreneurship), nyingine ikiwa ni ujasiriamali wa kikazi (intrepreneurship).

 

Kundi la kwanza linawakilisha uvumbuzi na ubunifu katika biashara binafsi na kundi la pili linawakilisha uvumbuzi na ubunifu katika ajira.

Hata hivyo, binafsi naona haina maana kubwa kuhangaika na tafsiri za kidhana ambazo ni ‘mbwembwe’ za watafiti na wanazuoni (pamoja na watunga sera); jambo la msingi ni kuziweka dhana na nadharia hizo katika utendaji. Tunachohitaji ni matokeo si ripoti na tafiti za vitabu.

Katika anga za uchumi na biashara kiuchumi kuna watu wa makundi manne (mimi huyaita mraba wa fedha); mfanyakazi, aliyejiajiri, mfanyabiashara na mwekezaji. Mfanyakazi ni mtu anayeuza muda wake kwa malipo ya fedha iitwayo mshahara (person working for money).

Aliyejiajiri ni mtu anayeuza ujuzi ama maarifa yake kwa malipo ya fedha iitwayo gharama za huduma. Mfano wa watu waliojiajiri ni kama mwanasheria wa kujitegemea, mwandishi wa kujitegemea, daktari mwenye zahanati lakini akawa anatibu mwenyewe, mtu mweye duka lakini akawa anahusika mwenyewe kwa kila kitu.

Watu waliojiajiri kikawaida wao ndiyo biashara na biashara ndiyo wao, mwanasheria wa kujitegemea akiugua na hela inakoma kuingia mfukoni mwake kwa sababu anakuwa hana uwezo wa kuwahudumia wateja tena.

 

Vivyo hivyo kwa mwenye duka na akawa anahusika yeye mwenyewe kwa asilimia mia moja. Dhana ya kujiajiri tunaiita kwa Kiingereza ‘a person working for himself’.

Mfanyabiashara ni mtu anayeanzisha biashara kisha anaajiri watu wengine kuendesha biashara hiyo, huku akipata kitu kiitwacho faida. Wafanyabiashara wanahusisha watu wenye kampuni, wenye maduka lakini wameajiri watu wengine pamoja na biashara nyingine.

Mfanyabiashara halazimiki kuwapo katika biashara ili kuzalisha faida, akiugua anaweza kuendelea kulipwa faida kutoka katika biashara zake, kwa lugha ya kigeni tunaita, ‘people working for a person’.

Kundi la mwisho ni mwekezaji. Huyu ni mtu anayeingiza fedha yake katika mradi ama biashara fulani pasipo kujihusisha moja kwa moja na uendeshaji wa biashara hiyo, kwa malipo ya fedha iitwayo gawio.

Mfano kununua hisa, kujenga nyumba za kupangisha, kuwekeza katika ushirika na kuacha mshirika mwingine kusimamia mradi. Hii tunaiita  ‘money working for a person.

Kwa bahati mbaya sana kuna watu wamejiajiri lakini wanajiita ama tunawaita wafanyabiashara!

Pia wapo watu ambao wameunganisha kujiajiri na ufanyabiashara, hakuna lililo baya; ni mfumo tu wa uamuzi unaopelekea katika uhuru wa kiuchumi na kifedha. Binafsi kila ninapofikiria biashara, huwa naangalia ile ambayo itanifanya niwe mfanyabiashara ‘pure’ ama mwekezaji, kuliko zile zitakazoniunganisha na kuwa niliyejiajiri.

Daima huwa natafsiri uhuru wa kifedha na kiuchumi kwa jinsi hii, ‘kuwa na fedha za kutosha, muda wa kutosha pamoja na furaha wakati wote’. Kumbe sasa utagundua kuwa hakuna haja ya watu kuogopa kufanya ujasiriamali wa kibiashara.

Mfanyakazi anaweza kuanzisha biashara kisha akaajiri watu wengine na yeye akaendelea zake na ajira yake.

 

Mfanyakazi huyo huyo anaweza kuamua kuwa mwekezaji huku akiendelea kuvuna gawio pasipo kuiacha ajira yake.

Ninafahamu kuna watu wanapenda sana ajira zao, kuna watu hawapo tayari kuyaacha marupurupu ya makazini kwao na pia wapo wale wanaopenda usalama (job security).

Pamoja na hayo, hawa wakitambua mbinu hizi za kiuchumi wanakuwa na nafasi ya kuwa wafanyabiashara na wawekezaji, wakaongeza vipato vyao maradufu na kutengeneza maelfu ya ajira.

Mwingine anaweza kusema, “Nikianzisha biashara wataniibia, bora niweke fedha zangu benki”; kwa mtu wa hivi napenda nimjibu hivi; zipo mbinu za kujenga mfumo wa biashara na pia ipo sayansi ya kuajiri wafanyakazi na kuwadhibiti, kisha utavuna faida bila wasiwasi wowote.

Kikubwa ni kujifunza na kukutana na wazoefu.

Matatizo ya mishahara isiyotosha ukilinganisha na gharama za maisha pamoja na matakwa ya waajiriwa imezalisha wezi, wadokozi na wala rushwa makazini. Usalama pekee wa kujikwamua na hili ni kujifunza biashara na uwekezaji. Uzuri wa biashara na uwekezaji ni kwamba unaweza kufanya pasipo fedha na ukazalisha fedha.

Kwa bahati nzuri nimewahi kuajiriwa, hivyo ninafahamu vizuri sana hiki ninachokisema hapa; huko mbeleni nitaandika makala ya, “Mfanyakazi na mbinu za kuwekeza vitegauchumi”

Ujasiriamali utaleta ushindi, dhidi ya ukosefu wa ajira!

0719 127 901

stepwiseexpert@gmail.com


1437 Total Views 1 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!