Bodi ya Mfuko wa Barabara imo mbioni kuzindua mfumo wa Teknolojia na Mawasiliano (Tehama) utakaowashirikisha wananchi katika kufuatilia uharibifu na matengenezo ya barabara.

Lengo la kuanzishwa kwa mfumo huo ni kuwawezesha na kuwashirikisha watumiaji wa barabara kutoa taarifa kwa mamlaka husika juu ya uharibifu wa miundombinu hiyo.

Hayo yamesemwa na Eliud Nyauhenga, Meneja wa Mfuko wa Barabara wakati wa kilele cha sherehe za kuwaaga wajumbe wa bodi ya mfuko huo  na kuwakaribisha wajumbe wapya.

Sherehe hizo zilifanyika Julai 24, mwaka huu jijini Mbeya, zikiwa zimehudhuriwa na Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Mhandisi Isack Kamwelwe.

Waziri Kamwelwe amewaeleza wajumbe wapya wa bodi hiyo kuwa serikali imeweka mikononi mwao jukumu la kuitunza na kuihifadhi rasilimali yenye thamani kubwa.

Wajumbe hao ili waweze kutekeleza majukumu hayo kwa ufanisi, serikali imeahidi kufanya nao kazi bega kwa bega na kwamba wasisite kufanya mawasiliano ya mara kwa mara na Wizara ya Uchukuzi, Mawasiliano na Ujenzi.

“Serikali itakuwa nanyi bega kwa bega ili kuwawezesha kuyatekeleza majukumu yenu kwa ufanisi,” amesema Kamwelwe.

Aidha, amesema maendeleo ya barabara ni moja ya kichocheo muhimu cha kiuchumi na kijamii, hivyo serikali imeweka mkazo katika kuimarisha miundombinu ya usafiri ikiwemo barabara ili kuwezesha uchumi wa viwanda na taifa kuwa la uchumi wa kati ifikapo mwaka 2025.

Kwa mwaka wa fedha 2019/2020, Mhandisi Kamwelwe amesema serikali imetenga Sh bilioni 839 kwa ajili ya matengenezo ya mtandao wa barabara na kwamba bodi inatakiwa kuzisimamia fedha hizo.

Waziri amewataka bodi na menejimenti ya mfuko kuhakikisha wanatumia weledi wa hali ya juu katika kutekeleza majukumu yao huku akiwaonya kujiepusha na vitendo vya rushwa na utendaji mbovu wa kazi za barabara.

“Sote tunajua jinsi ambavyo inagharimu fedha nyingi kurekebisha kazi za barabara au kufanya matengenezo baada ya muda mfupi pale ambapo kazi zinakuwa zimetengenezwa chini ya viwango vinavyokubalika, niwaombe mfanye kazi kwa umakini,” amesema Kamwelwe.

Aidha, amesema serikali haitawavumilia watu wanaofanya wizi wa alama za barabarani, kuzidisha uzito na kumwaga mafuta barabarani, kwani wanasababisha madhara makubwa kwa wananchi wengine.

Naye Mwenyekiti wa Bodi ya Mfuko wa Barabara, Joseph Haule, amesema mtandao wa barabara zilizorasimishwa kwa sasa una urefu wa kilomita 89,000 wenye thamani ya takriban dola za Marekani bilioni 8.964, sawa na Sh trilioni 20.76.

Hata hivyo amesema kuna mtandao wa barabara wa kilometa 82,000 ambazo bado hazijarasimishwa na kwamba barabara ni mtandao wa usafiri unaotumiwa na wananchi wengi zaidi ukilinganisha na mitandao ya usafiri mwingine.

Kutokana na umuhimu wa mtandao huo, Haule anasema mfumo wa teknolojia unaoandaliwa (application software) utasaidia watumiaji wa barabara kutoa taarifa zinazohusu uharibifu wa miundombinu ya barabara kwa nchi nzima.

Ameipongeza serikali kwa kuanzisha Wakala wa Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA) kwamba uamuzi huo umeibua mageuzi makubwa katika kusimamia barabara za wilaya.

“Barabara nyingi ambazo zilikuwa hazipitiki hapo awali kwa sasa zinapitika na zinawawezesha wananchi kushiriki kikamilifu katika shughuli zao za kiuchumi na kijamii,” amesema Haule.

Amewashukuru wajumbe waliomaliza muda wao kwa kufanya kazi yao kwa ufanisi mkubwa kwani sehemu kubwa ya mafanikio kwenye miundombinu ni matokeo ya kazi yao.

“Tuwaombe wawe tayari kutupatia ushauri wa kitaalamu pale ambapo itakapohitajika, kwani wana hazina kubwa ya uzoefu juu ya usimamizi wa barabara,” amesema.

By Jamhuri