Siku chache baada ya polisi kutangaza kumkamata Hamis Said Luwongo (38), kwa tuhuma za kumuua na kumchoma moto mke wake, Naomi Marijani, taarifa za kina zimeanza kuvuja na inaonekana simu ya mkononi ilichangia kutokea kwa mauaji hayo.

Uchunguzi unaonyesha kuwa miaka mitatu iliyopita, familia ya Hamis na Naomi, iliingia katika majaribu ya hali ya juu baada ya wanandoa hao kutiliana shaka na kuamua kudukuana simu zao za mkononi. Hali hii ilizua tafrani kwa kiwango ambacho kama si Baba Mkwe, Mchungaji mzee Said Hamis Luwongo (72), basi ndoa hiyo ilikuwa ivunjike mwaka 2016.

“Mwanamke alikuwa hamwamini mumewe. Nililetewa ugomvi usiku wa manane, miaka mitatu iliyopita kwamba mwanamke (Naomi) ailikuwa ameunganisha mawasiliano yote ya simu ya mume wake (Hamis) kwenye simu yake bila mwanamume kujua… kilichomshangaza ni kuwa kila alichopanga kufanya, basi mkewe alikifahamu.

“Hili lilimkasirisha sana Hamis, akataka amrudishe kwao. Waligombana hasa. Mimi nilimkatalia, nikamwambia ‘huwezi kumrudisha kwao kwa ajili ya simu – kama amekushinda, mlete aishi kwangu.’ Baada ya hapo walitulia, na sikupata kusikia tena vurugu… yapata miaka kama mitatu hivi iliyopita,” anasema baba wa Hamis, Mchungaji Luwongo.

Mchungaji Luwongo ametoa taarifa nzito juu ya mwanae Hamis, akisema miaka mitatu iliyopita, amepata kutubu kwake akisema anataka kuachana na kutenda maovu: “Niliongea naye hapo katikati akanikubalia, nikamwongoza sala ya toba, lakini baada ya hapo hakurudi kanisani… nilimwombea kwenye simu, akaniambia ‘Baba nataka kumrudia Mungu maana haya maisha ninayoishi siyo’.

“Akasema ‘Maisha haya ninayoishi yana mwisho haya, kwa hiyo nimeona nimrudie Mungu’,” amesema Mchungaji Luwongo anayesema anajisikia aibu mno kuona mtoto wa mchungaji anatuhumiwa kufanya mauaji ya kinyama kwa mkewe, ila akaongeza: “Kwa kujificha hisia, yuko vizuri sana. Alikuja hapa akasema anaangua nazi ampelekee mtoto matumizi baada ya mama yake (Naomi) kuwa amepotea. Usingeweza kuona hisia za aina yoyote. Alikuwa kama mtu ambaye hajatenda lolote.”

 “Mimi niseme kwa upande wangu, tukio hili limenisikitisha sana sana, kwa sababu si la kiutu, kama kuna mtu anafikiri baba yake amefurahia, sivyo nilivyo.”

Hamis, ambaye ni mtoto wa 5 katika uzao wa watoto 6 wa Mchungaji Luwongo, ambaye alikuwa Mwislamu, lakini mzee huyo akaongoka na kuokoka mwaka 1988 baada ya kuugua ugonjwa wa akili (psychiatry) kwa miaka 14, ilimchukua mwezi mmoja kumfahamisha baba yake juu ya upotevu wa Naomi.

 “Sikumbuki siku, lakini alinipigia simu kama mwezi mmoja uliopita, akanijulisha kwamba mke wake amepotea na kwamba ameishatoa taarifa polisi kuwajulisha suala hilo,” anasema baba mzazi wa Hamis katika mahojiano na JAMHURI. Kisha baba huyu anasema hakushiriki kumtafuta Naomi baada ya kutaarifiwa kuwa amepotea kutokana na historia ya matatizo katika ndoa ya wawili hao.

“Wale walikuwa na siri, mambo yao walikuwa wanayamaliza wenyewe. Kama miaka 5 hivi iliyopita walikuwa na ugomvi mkubwa, hata mtoto alikuwa hajazaliwa (kwa sasa mtoto wao Gracious ana miaka 6)… mara chache sana walifika kunisalimu, hatukuwa na mawasiliano ya karibu,” anasema Mchungaji Luwongo.

Aliachaje Uislamu?

Mchungaji Luwongo anasema mwaka 1974 alipata ugonjwa wa afya ya akili (psychiatric), na ugonjwa huo ulidumu hadi mwaka 1988. “Ukristo nimeingia mwaka 1988. Niliugua miaka 14, tangu mwaka 1974 hadi mwaka 1988.

“Niliongea na watu wakanishauri kuwa nenda uombewe pale Jangwani kwenye mkutano wa The Big November. Nilipoombewa nikapona kabisa. Kwa kweli sikuwa na namna ila kuokoka. Ila sasa tangu mwaka 2010 umenirudia tena na uko katika makundi matatu.

“Kundi la kwanza ni la Hukumu. Hata hivi tunavyozungumza ni kama narekodi mkanda. Baada ya muda nikibaini nimesema neno lisilo la kweli, nitakuwa na hema hadi nikupigie simu kukuomba msamaha ndipo natulia, vinginevyo situlii.

 “Kundi la pili unanifanya ninyanyapae. Hivi siwezi kushika chuma chenye kutu. Nikikishika naona kama nakufa vile, kuna watu wananiambia ni mawazo tu, lakini mimi nasema ni tatizo. Maana nikishika chuma chenye kutu, hata nikigusa nguo niliyovaa najihisi napaswa kuivua maana nayo naisikia ina kutu, mpaka ninawe mikono kwa sabuni ndipo nitulie.

“Kundi la tatu ni mgonjwa sipatani naye. Nikiona mgonjwa yeyote hata kwenye basi nitamwachia hadi kiti, maana naona ataniambukiza ugonjwa alionao na muda wowote nitakufa. Hii inanitesa sana. Makundi haya matatu yananitesa sana. Hata nilipopata taarifa hizi, ile hali ya kuhema ikapanda sana,” amesema.

Mchungaji huyo anaongeza kuwa hadi sasa hakuna askari polisi yeyote aliyefika nyumbani kwake kumhoji yeye au wanafamilia. Hana uhakika kama upande wa pili wa mzazi umehojiwa, kwani anasema kwa sasa hawana mawasiliano.

Familia ya Mchungaji

Familia ya Luwongo ilianza kupata misukosuko siku nyingi. Baba na Mama Luwongo walitengana mwaka 1983, ikiwa ni miaka miwili tu, tangu Hamis azaliwe na ukiwa ni mwaka aliozaliwa Abdul. Mchungaji Luwongo anaeleza sababu ya kutengana kwao: “Alikuwa haelewani na mama mkwe, yaani mama yangu, ikabidi tutengane.” Mke wa Mchungaji Luwongo, au mama wa Hamis alikuwa anatokea mkoani Kagera, ambaye awali alijulikana kwa jina la Victoria Emmanuel Tilutoija, ila baadaye alipoolewa na Luwongo alibadili dini na kuitwa Lukia.

 Yapo mambo yanayomsikitisha Mchungaji Luwongo: “Hamis sasa si Mkristo, ameacha Ukristo muda mrefu sana. Hata huyo mkewe (Naomi) inaelezwa kuwa alikuwa haendi kanisani inavyotakiwa.” Hata hivyo, mzee huyo anasema Hamis alikuwa mtu mpole na mtu wa msaada, kwani hata nyumba anayoishi mtoto huyo ndiye aliyeisiliba.

Kuchelewa kupata taarifa

Mchungaji Luwongo anasema inamsumbua yeye kuchelewa kupata taarifa za tukio la kupotea au kuuawa kwa Naomi. “Inanisumbua sana. Tukio litokee Mei, mimi nipate taarifa Julai? Huyu mtu alikuwa anatunza siri kweli kweli. Ilipita mwezi mzima ndipo akaniambia… hizi taarifa zinaogofya. Sikufuatilia au kuzizungumza na mtu, maana naogopa kuzisema kwenye simu, naona bora kukutana na mtu uso kwa uso,” amesema.

Alipoulizwa tangu tukio hili litokee yeye akiwa mchungaji amepata kumwombea mtoto wake Hamis kwa haya yaliyompata, akasema: “Nimeomba lakini kuna shida. Kati ya mwombaji na mwombewa, Mungu anataka kuangalia huyo Hamis yeye anamwamini Mungu kiasi gani au ana mahusiano gani na Mungu?

“Katika maandiko matakatifu kwenye Biblia, upo mfano ambao Samweli alikuwa anamwombea Sauli, kumbe Mungu aliishamwacha Sauli akamwambia Samweli, acha usimwombee… ila kwa kuwa kwa Mungu hakuna linaloshindikana, matumaini ya kumwona tena Hamis yapo, kwa kuwa yeye si wa kwanza kutenda jambo hili.”

Alipoulizwa akikutana naye kwa sasa atamwambia nini Hamis, akasema: “Kwa sasa sijui nafasi itakuwa ni ya uhuru kiasi gani tunapokutana… ni kama niseme nimeishachelewa, maana sina cha kumwambia kimwokoe tena sasa hivi.”

Kazi aliyokuwa anaifanya Hamis

Baba mzazi anasema kazi ya msingi aliyokuwa anaifanya Hamis ni udalali wa viwanja na nyumba. Kazi hii imemwezesha kumiliki nyumba tano huko Kigamboni, ikiwamo nyumba ya wageni inayoitwa Man U.

Kabla ya kufanya udalali, alikuwa anauza vitunguu na viazi kutoka mikoa ya Iringa na Mbeya alivyokuwa anasafirisha na kuvileta jijini Dar es Salaam.

Anaongeza kuwa Hamis alikuwa mpenda michezo na huko Kigamboni anamiliki timu ya mpira wa miguu ambayo huwashindanisha na kuwapatia zawadi mbalimbali mara kwa mara.

Luwongo ambaye ni Mchungaji wa Kanisa la Tanzania Assemblies of God (T.A.G) Kigamboni, jijini Dar es Salaam, ameliambia Gazeti la JAMHURI kwamba tukio hilo kwa ujumla limempa wakati mgumu baada ya kupata taarifa za mauaji hayo kupitia gazeti hili.

“Habari hizi nilizipata kutoka kwenye gazeti lenu (JAMHURI). Nilipigiwa simu na mwanangu anaitwa Abdul, yeye anaishi Morogoro. Gazeti sikulifuata isipokuwa lilinikuta hapa hapa kwangu. Polisi walikwenda Gezaulole, mwanangu wa kike (Sofia), akaniambia baadaye atakuja kwangu na ninakumbuka kwamba alifika hapa kwangu kama saa tano hivi usiku.

“Nilipata wakati mgumu sana, maana unajua nina matatizo ya afya ya akili. Nilimwomba kijana hapa anisomee, alipofika katikati nikamwambia basi,” anasema Mchungaji Luwongo katika mazungumzo na timu ya uchunguzi ya JAMHURI iliyofika nyumbani kwake Kibugumo, Kigamboni jijini Dar es Salaam wiki iliyopita.

Kuhusu mtoto wake Hamis, Mchungaji Luwongo anasisitiza: “Kwa kweli nikiri kama ni ujasiri, anao wa aina yake. Alikuwa anaonekana mtulivu na asiye na wasiwasi wowote kwa kiwango ambacho huwezi kuamini, hata baada ya taarifa za kupotea mke wake kuenea. Ni ujasiri wa kutisha kwa kweli.”

Yafuatayo ni mahojiano kati ya timu ya JAMHURI na Mchungaji Saidi Luwongo yaliyofanyika nyumbani kwake Kibugumo:-

JAMHURI: Taarifa tulizonazo wewe ni Mchungaji, lakini kuna swali linajitokeza kuhusu uchungaji wako huu kwani una majina yanayoweza kutajwa kuwa ya Kiarabu au Kiislamu. Tunaomba ufafanuzi wa hili.

Majina yangu ninaitwa Saidi Hamis Luwongo (72). Tulitoka kwenye Uislamu, na mimi ni mchungaji wa Kanisa la T.A.G. Hamis ni mtoto wa tano, nina jumla ya watoto sita, wawili walishafariki dunia.

JAMHURI: Ulipataje taarifa za tukio hili la mauaji ya mkwe wako, Naomi?

Mchungaji Luwongo: Alinipigia (Meshack) simu akiniambia kwamba mke wake amepotea, akasema ameshatoa taarifa polisi. Baada ya hapo shughuli za kumtafuta zikaendelea. Sikuwahi kushiriki kumtafuta, maana baada ya kuniambia ameshatoa taarifa polisi, nikadhani polisi wanaendelea na kutafuta. Mwanangu na mkewe walikuwa wasiri sana, mambo yao huwa wanayamaliza wenyewe.

JAMHURI: Umewahi kuletewa mashtaka?

Mchungaji Luwongo: Ni zamani kidogo, walikuwa hawajapata hata mtoto wao…chanzo cha ugomvi wao ilikuwa wivu, hakuwa anamwamini mumewe. Mwanamke aliunganisha simu ya mumewe kwenye simu yake, hivyo kila kitu kilichokuwa kinaingia kwenye simu ya mumewe alikuwa anakipata. Hamis (Meshack) alifikiria kumrudisha huyo mwanamke kwao, nikamwambia kama anataka kumrudisha basi amlete kwangu. Hawakuwa wanakuja kunisalimia.

JAMHURI: Kuna mawasiliano baina ya familia hizi mbili za mume na mke?

Mchungaji Luwongo: Hapana, si kwamba tumegombana. Uvivu wa kutembeleana.

JAMHURI: Mama wa Hamis (Meshack) anayeitwa Lukia kwa mujibu wa jina lililomo kwenye cheti cha kuzaliwa cha Hamis bado ni mkeo?

Mchungaji Luwongo: Hapana si mke wangu tena, tulitengana mwaka 1983, Hamis alikuwa na miaka kama miwili hivi. Tulitalikiana na mke wangu maana hakuwa anaelewana na mama yangu (Mwanamkuru binti Makame). Mama yangu amefariki dunia mwaka 1994. Mimi nilikuwa mtoto wake wa mwisho kati ya watoto wake saba, sasa tumebaki wawili, yaani wa kwanza na mimi mtoto wa mwisho.

JAMHURI: Sasa mchungaji, umeshawasiliana na mama yake Hamis kuhusu tukio hili?

Mchungaji Luwongo: Sijawasiliana naye kwa jambo hili. Wakati ninamwoa alikuwa anaitwa Victoria Emmanuel Tilutoija. Kwao ni chini kidogo ya kijiji kinaitwa Rwome.

 JAMHURI: Taarifa za Hamis kukiri kumuua mkewe ulizipata lini?

 Mchungaji Luwongo: Habari hizi nilizipata kutoka kwenye gazeti lenu (JAMHURI). Nilipigiwa simu na mwanangu anaitwa Abdul, yeye anaishi Morogoro. Gazeti sikulifuata isipokuwa lilinikuta hapahapa kwangu, polisi walikwenda Gezaulole, mwanangu wa kike (Sofia), akaniambia baadaye watakuja kwangu na ninakumbuka kwamba walifika hapa kwangu kama saa tano hivi usiku.

JAMHURI: Uliposoma gazeti ulijisikiaje?

Mchungaji Luwongo: Nilipata wakati mgumu sana, maana unajua nina matatizo ya afya ya akili, nilimwomba kijana hapa anisomee, alipofika katikati nikamwambia basi.

 JAMHURI: Tangu tukio hili limetokea, umeweza kwenda kanisani?

 Mchungaji Luwongo: Sijaweza kwenda kanisani, isipokuwa juzi Jumapili (Julai 21, 2019). Baadhi ya waumini wamekuja kunisalimia. Nianze kwa ushuhuda, Hamis si Mkristu, aliacha na kurejea Uislamu. Inanipa wasiwasi kwamba tabia yake ilibadilika, Hamis na mkewe hawakuwa wanaelewana kwa zaidi ya miaka miwili.

JAMHURI: Unamfahamu vipi Hamis, ukiachilia mbali tukio hili?

Mchungaji Luwongo: Kuhusu tabia yake…(kimya kama dakika tatu hivi), sijui nisemeje! Hamis ni mtu wa msaada kwa mfano akikuta una shida anakusaidia bila kujali kama ni ndugu yake. Jambo hili (mauaji) limenishtua sana na sijui kama ni akili yake ama alikuwaje. Kwa upande wangu binafsi, nyumba yangu hapa Hamis ndiye amepiga plasta. Nimepata ushuhuda kwamba hivi karibuni alikwenda kwa dada yake (Salma) na kumkuta mwanaye anaumwa Hamis alitoa fedha mpwawe apelekwe hospitali.

 JAMHURI: Mwaka 1981, wakati Hamis anazaliwa ulikuwa bado Muislamu?

Mchungaji Luwongo: Ndiyo, nimeingia Ukristo mwaka 1988, baada ya kuugua tangu mwaka 1974 bila kupona. Niliombewa kwenye mkutano wa Big November pale Jangwani. Ila sasa naona kama limeanza kujirudia, ninaumwa psychiatry (ugonjwa wa akili). Ugonjwa wangu umegawanyika kama sehemu tatu. Napata hukumu sana, nikisema uongo napata shida sana. Jambo la pili, kunyanyapaa, nikiona chuma chenye kutu, nafsi inaniambia nisishike, ninakufa. Nikikaa na mgonjwa, napata feeling (hisia) kwamba nami nitaambukizwa, sifanyi vurugu.

Jumatatu ya wiki iliyopita nilipata shida sana, ile hali ya kuhema ikaanza kunisumbua sana. Tukio limefanyika mwezi wa tano halafu taarifa zinakuja kujulikana mwezi wa saba, maana hata hiyo kupotea si kwamba alipotea jana akaja kuniambia leo, hapana ulipita kama mwezi.

JAMHURI: Mchungaji unafahamu adhabu itokanayo na mauaji?

Mchungaji Luwongo: Ninajua, ni suala la kisheria hilo. Tuache sheria ichukue mkondo wake, tukio hili limetikisa familia. Mke wangu hajanitafuta kuniuliza kama kuna jambo lolote. Ninamuombea Hamis, lakini naona kama ni mzigo fulani, mara nyingi Mungu hupokea maombi yenye usafi pande zote mbili. Mungu ataangalia huyo ninayemuombea ana uhusiano gani na Mungu. Samweli alikuwa anamwombea Sauli bila kujua kwamba Mungu hakuwa anapendezwa naye, akamwambia acha.

JAMHURI: Unayo matumaini ya kuonana na Hamis tena?

 Mchungaji Luwongo: Kwa kuwa kwa Mungu hakuna lisilowezekana, matumaini hayo bado ninayo, maana yeye si wa kwanza. Nikikutana naye katika hali aliyomo, sijajua nafasi nitakayoipata itakuwa ya uhuru kiasi gani, kama mazingira hayaruhusu tutaishia kusalimiana habari gani? Hujambo, sijambo. Nahisi nimechelewa maana sina cha kufanya ili kumwokoa sasa hivi!

JAMHURI: Umewahi kupata fursa ya kumfunda Hamis kwenye maisha yake ya kawaida?

Mchungaji Luwongo: Makatazo au mafunzo binafsi sijawahi, isipokuwa huwa nimejenga utamaduni wa kuzungumza na familia yangu yote. Ninafahamu Hamis alikuwa anafanya kazi ya udalali, hiyo ndiyo inafahamika.

Baada ya kutokea tukio hili, nami ndiyo nikaanza kusikia, pale alipo (anapoishi) ana timu ya mpira wa miguu. Mtu kama huyo ukisema hashirikiani na watu, hapo kuna walakini. Tangu tukio hili limetokea, ninyi JAMHURI ndio kwanza mmekuja kunihoji!

JAMHURI: Hamis anapendelea nini?

Mchungaji Luwongo: Hamis anapenda michezo. Ndiyo maana ameanzisha hata timu.

JAMHURI: Familia ina mpango wa kumuwekea wakili Hamis?

Mchungaji Luwongo: Naendelea kufuatilia kwa karibu…suala hili limewatisha sana hata ndugu zangu, sasa tunahofia hata kuwasiliana kwa simu. Maana ile habari mliiandika kiufundi sana. Hamis hakuja kuniambia isipokuwa alinipigia simu…katika mazungumzo yetu hakuonekana kuwa na wasiwasi.

JAMHURI: Tumezungumza na baadhi ya wanafamilia, wanasema jambo hilo ni la aibu, hapa hali ikoje?

Mchungaji Luwongo: Jambo hili limenifedhehesha sana, maana sasa anayetajwa ni Luwongo… Luwongo ni Mchungaji, anaaminiwa na watu. Miaka mitatu iliyopita, Hamis alinipigia simu usiku wa manane akitubu, nikamwita na kumfanyia sala ya toba. Alikiri kwamba amekuwa anaishi maisha yasiyompendeza Mungu. Sijajua jambo gani lilimgusa, alikuwa ananiambia maisha haya yana mwisho bora nimrudie Mungu tu.

Hamis alikuja hapa siku ya Jumatano (Julai 10, 2019), ambapo Jumatatu iliyofuata ndiyo alikamatwa, alikuja kuangua nazi kwenye shamba lake hapa jirani na nyumbani. Hakuweza kuonyesha hisia zozote kwetu, ni msiri sana wala hatukuweza kubaini jambo lolote!

JAMHURI: Nini maoni yako juu ya mkasa huu!

 Mchungaji Luwongo: Kwa upande wangu hili tukio limenisikitisha sana, maana si tukio la utu. Kama kuna mtu anadhani baba yake Hamis amefurahi, ameridhika hapana, sivyo nilivyo.

JAMHURI: Mzazi mwenza ungepata fursa ya kumpa ujumbe, ungemwambia nini?

Mchungaji Luwongo: Labda ningemuuliza mwenzangu amelipokeaje jambo hili.

Kauli ya Mkemia Mkuu

Akizungumza na JAMHURI kuhusu maendeleo ya uchunguzi wa kimaabara wa sampuli za mabaki ya mwili wa Naomi, Mkemia Mkuu wa Serikali, Dk. Fidelice Mafumiko, amesema kazi hiyo imekamilika kwa upande wao na jana Jumatatu walitarajia kuikabidhi kwa Jeshi la Polisi kwa ajili ya hatua zaidi.

“Sisi kazi yetu imekwisha kukamilika, tunarudisha matokeo ya kazi hiyo kwa wahusika. Si kazi yetu kutoa matokeo ya uchunguzi. Hiyo ni kazi ya vyombo husika,” amesema Dk. Mafumiko.

Katika hatua nyingine, mmoja wa wanafamilia amelieleza JAMHURI kwamba sampuli zilizochukuliwa kwa ajili ya kuoanisha na mabaki ya mwili yanayoaminika kuwa ya Naomi zimetoka kwa mtoto wa Naomi na Meshack, Gracious. Huyo ndiye mtoto pekee wa wanandoa hao akiwa na umri wa miaka sita.

Kazi ya awali ya JAMHURI

Gazeti la JAMHURI limekuwa la kwanza kufichua tukio hili kupitia toleo namba 407 lilipoandika habari kuhusu Naomi yenye kichwa kinachosomeka: Ameuawa?

JAMHURI lilieleza kuwa Jumamosi ya Mei 18, 2019 mume huyo wa Naomi alikwenda nyumbani kwa mzee Robert Mchome anayeishi Mabibo (Dar es Salaam) kutoa taarifa kuwa Jumatano ya Mei 15, 2019 saa 1:30 jioni alipokea ‘meseji’ kutoka kwa mkewe kupitia namba 0655 527 203 (namba aliyokuwa akiitumia mke wake) ikisema: “Naondoka na mtoto namwacha nyumbani peke yake na kesho nasafiri nje ya Tanzania.” Dakika 10 baadaye, saa 1:41 akadai kupokea ‘meseji’ ya pili ikisema: “Na hutonipata kwa namba hii tena, hudumia mtoto vizuri,” kwenda kwenye namba zake za 0685043374 na 0714812530.

Akaongeza kuwa, alirudi nyumbani usiku saa tatu na kukuta mtoto akiwa peke yake, akaenda kumnunulia chakula akala, siku iliyofuata akamuandaa mwenyewe mtoto na kwenda shule.

Kwamba mkewe kadai kamtaarifu ameondoka na kamwacha mtoto Mei 15, 2019 na akamkuta mtoto yuko peke yake. Swali lilibaki ni kwa nini hakupiga simu kokote kuulizia kuhusu mkewe kupotea siku hiyo ya Jumatano, na siku mbili zilizofuata, Alhamisi na Ijumaa hadi Jumamosi asubuhi ndipo alipofunga safari kwenda Mabibo kutoa taarifa. Je, ni kitu gani kilikuwa kinaendelea ndani ya hizi siku tatu; Jumatano, Alhamisi na Ijumaa?

Uchunguzi wa JAMHURI kwa kushirikiana na familia, na wataalamu wa mitandao ulibaini kuwa simu ya Naomi ya 0655527203 ilitumika kumpigia Meshack (mume wake) na kumtumia ‘meseji’ saa 7:37 mchana kwenye namba 0677009128 ambayo kwa mujibu wa Meshack, Naomi haijui hiyo namba. Hapa swali linajengeka: “Aliijuaje mpaka akaipigia?”

Maswali yalikuwa mengi kuliko majibu. Habari hizi zilizotangulia kuchapishwa zinapatikana kwenye www.jamhurimedia.co.tz.

Mkuu wa Upelelezi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Camilius Wambura, ameliambia JAMHURI kuwa uchunguzi umefikia hatua nzuri.

5817 Total Views 2 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!