Wiki iliyopita, makala hii iliishia kwa kuonesha kuwa Wazayuni waliitumia vyema bahati ya mtende – juu ya kufunguliwa kwa milango ya Wayahudi kuhamia Palestina – na ndani ya robo karne idadi ya Wayahudi iliongezeka mara kumi zaidi. Je, unafahamu nini kimetokea? Endelea…

 

Ilikuwa ni katika mchakato huu wa suala zima la uhamiaji ambapo ufanikishwaji wa uanzishwaji wa Taifa la Israel-Palestina ulitekelezwa chini ya Jina la Israel.

Tafakuri  hii fupi inatusaidia kupata ‘connection’ ya kihistoria kati ya Wayahudi na Wapalestina katika picha,  na taswira  halisi kwa ujumla wake inaonesha makosa ya dhana ya sasa inayojengwa kwa makusudi ya kwamba Wapalestina walikuwa ndiyo wavamizi wa Palestina wakati wa uvamizi wa Waislamu katika karne ya saba. Hii si sahihi kihistoria. 

Wapalestina ni wakazi wa awali na wakongwe wa Palestina. Utekaji wa Waislamu Waarabu wa Palestina wa A.D. 637 haikuwa hatua yao ya mwanzo ya kukalia nchi. Waarabu ni Waislamu wa awali. Waliishi Palestina na sehemu nyingine za  Mashariki ya Kati kabla ya kuibuka kwa Waislamu. 

Professor Maxime Rodinson ananena; “Idadi ya Wapalestina ya wakati ule ilikuwa ni mkusanyiko wa watu asili kwa maana yake. Wapalestina wa leo ni uzao wa Wafilisti, Wakanaani na makabila mengine ya awali  yaliyokalia nchi ile.”

Wameishi katika nchi hiyo  tangu enzi na enzi za historia. Kuishi kwao  Palestina, kunaweza kurejewa takribani karne 40.

Kulikuwa na matabaka ya wakazi wengine yaliyochangamana na Wapalestina kutoka Ugiriki, Rumi, Waislamu Waarabu na Makruseda (Crusaders). Lakini jumuiko hili la Wapalestina – linalounganisha Waislamu na Wakristo – liliendelea kuunda kikonyo maalumu cha wakazi hawa, hadi walio wengi walipofurumushwa na Waisraeli mwaka 1948.

Kwa hiyo, madai ya Uzayuni juu ya hatimiliki kwa Palestina yalisukumwa kwa mara ya kwanza na Zionist orgnization katika mkutano wa amani wa Paris mwaka 1919, ‘Memorandum’ yake ya Februari 3, 1919 kwenda kwa Baraza la Juu la Muungano wa Mataifa (The Supreme Council of the Allied Powers).

Organaizesheni ya Zayuni ilipoendekeza utekelezaji wa azimio ambapo muungano wa mataifa makubwa utambue hatimiliki ya kihistoria ya Wayahudi kwa Palestina na haki ya Wayahudi kuunda nchi yao ndani ya Palestina, ‘memorandum’ ile ilidai ya kuwa nchi ile ilikuwa ni nchi ya kihistoria  ya Wayahudi na kwamba kwa kutumia mabavu waliondolewa kutoka Palestina.

Chini ya  kichwa cha habari “The historic title” ‘memorandum’ ile iliendelea kuelezea msingi wa madai ya Wazayuni kama ifuatavyo:

Madai ya Wayahudi juu ya Palestina yametuama katika mambo ya msingi  yafuatayo:

i) Ardhi ni nchi ya kihistoria ya Wayahudi. Pale walifanikiwa kupata maendeleo makubwa.

ii) Katika baadhi ya sehemu duniani na hasa mashariki mwa Ulaya,  maisha ya mamilioni ya Wayahudi yanachukuliwa kuwa ni muhimu kupewa upenyo mpya.

iii) Lakini Palestina siyo kubwa kiasi hicho kuweza kuwahifadhi  Wayahudi walioko sehemu mbalimbali za dunia.

iv)Ardhi yenyewe inahitaji kuhuishwa. Sehemu iliyo  kubwa bado haijafanyiwa kazi.

Akitoa maoni juu ya uwasilishaji wa suala la Wazayuni katika mkutano wa Oman kule Paris, Colonel Bonsal anatanabahisha katika shajara yake.

“Kama mawazo/mtazamo wa Wazayuni  utaendelea kushamiri, kuna tatizo siku za usoni; wengi  tena watu wengi na wasomi  wakiwamo Wayahudi wenye upeo wanakiri hili. Inakubalika ya kwamba wakazi wa sasa wa Palestina wamelikalia eneo kwa karne nyingi…”

Madai ya Uzayuni juu ya hatimiliki ya kihistoria ya ardhi ya Palestina hayana msingi, hasa kwa sababu mbili:-

Palestina si makazi ya kihistoria ya Wayahudi. Mnamo mwaka 1920 baada ya suala la udhamini wa Uingereza kwa Palestina lilipojadiliwa na Bunge – The House of Lords Lord Sydenham – alitamka. Je, unafahamu lilitamka nini? 

 

Itaendelea

 

Mwandishi wa makala hii anapatikana kwa:-

+255 784 142137/+255 713 333141 

Au barua pepe:[email protected]/[email protected]

By Jamhuri