Mhamiaji wa Mali amepongezwa kama shujaa baada ya kukwea sehemu ya mbele ya jengo la ghorofa mjini Paris kumuokoa mtoto aliekuwa kwenye uzio wa ubaraza wa ghorofa ya nne kwenye jengo refu.

Video ya Mamoudou Gassam akimuokoa mtoto ilisambaa sana kwenye mitandao ya kijamii.

Alivuka kutoka kwenye ubaraza mmoja hadi mwingine kwa muda wa chini ya dakika moja akamvuta mtoto huyo aliyekuwa amekwama na kumsalimisha.

Meya wa Paris Anne Hidalgo pia alisifu sana ushujaa wa mwanaume huyo mwenye umri wa miaka 22, na akasema alimpigia simu kumshukuru.

Alimuelezea kama “Spiderman wa 18”, akimaanisha wilaya nambari 18 ambako uokoaji huo ulifanyika mjini Paris.

“Hongera kwa Mamoudou Gassama kwa tendo lake la ujasiri la kumuokoa mtoto,” ulisema ujumbe wa Twitter wa Hidalgo.

“Alinielezea kwamba alikuwa amewasili kutoka nchini Mali miezi michache iliyopita akiwa na ndoto ya kujenga maisha yake hapa.

“Nilimjibu kwamba ishara yake hii ya ushujaa ni mfano kwa raia wote na kwamba Jiji la Paris bila shaka litakuwa tayari kumuunga mkono katika juhudi zake za kuishi Ufaransa.

Kisa hicho kilifanyika Jumamosi jioni kwenye mtaa mmoja uliopo kaskazini mwa jiji la Paris.

Bw Gassama aliwaambia waandishi wa habari kuwa alikuwa akipita tu mtaani ndipo alipoona umati wa watu umekusanyika mbele ya jengo.

“Nilijitolea kwa sababu alikuwa ni mtoto,” gazeti la Le Parisien lilimnukuu akisema . “Nilikwea jengo… Namshukuru Mungu nilimuokoa.”

Wahudumu wa kampuni ya zima moto jijini Paris walifika eneo la tukio na kupata tayari mtoto ameokolewa.

“Kwa bahati nzuri , kulikuwa na mtu mwenye nguvu za mwili na mwenye ujasiri wa kwenda na kumchukua mtoto,” aliliambia shirika la habari la AFP.

Maafisa wa eneo hilo walionukuliwa na vyombo vya habari vya Ufaransa walisema kuwa wazazi wa mtoto huyo hawakuwa nyumbani wakati alipookolewa.

Baba yake amekuwa akihojiwa na polisi akishukiwa kumuacha mwanae bila mtu wa kumuangalia, zimeeleza taarifa za mahakama.

Inaaminiwa kuwa, mama yake hakuwa Paris wakati wa tukio hilo.

By Jamhuri