Hotuba ya rais wa kwanza wa Ghana, Kwame
Nkrumah siku ya uhuru wa nchi yake Machi 6, 1957
ilikuwa na ujumbe mmoja mzito: Uhuru wa Ghana
hautakuwa na maana yoyote iwapo nchi nyingine za
Afrika zitabaki chini ya utawala wa kikoloni. Aliona
jukumu la Ghana ni kusaidia kulikomboa Bara la
Afrika kupata uhuru kamili.
Miaka sita baadaye kwenye kikao cha Umoja wa Nchi
Huru za Afrika (OAU) Nkrumah alitoa ujumbe
akihimiza serikali za Afrika kuungana mara moja
kuunda serikali moja ya Bara la Afrika. Alisema Afrika
inapaswa kuungana au, isipoungana, iteketee kwa
sababu nchi moja moja za Afrika hazikuwa na uwezo
wa kuhimili mikakati ya kiuchumi na biashara
iliyokuwa inadidimiza maslahi ya nchi hizo.
Alisisitiza kuwa uhuru wa kisiasa ulikuwa hatua
mojawapo tu ya mapambano dhidi ya ukoloni na

kusema hatua ya pili na muhimu ilikuwa uhuru wa
kupanga mipango na mikakati ya kiuchumi na kijamii
bila kuingiliwa na kudhibitiwa na nguvu za ukoloni
mamboleo.
Atakumbukwa kama kiongozi aliyeamini kuwa utajiri
wa rasilimali wa Bara la Afrika, pamoja na umoja wa
kisiasa na mikakati ya pamoja ya uchumi, viwanda,
kilimo, na miundombinu vingeimarisha Bara la Afrika
na kuhakikishia maendeleo kwa watu wake.
Baadhi ya viongozi wa Afrika wakati huo, ikiwa ni
pamoja na Mwalimu Nyerere, waliamini kuwa umoja
wa Afrika haukupaswa kuharakishwa mara moja, lakini
ungepitia hatua – kwa nchi chache kuungana kabla ya
kuingia hatua ya umoja wa nchi zote za Afrika.
Makundi haya mawili hayakuweza kukubaliana juu ya
hatua muafaka za kuchukua kufikia lengo la kuimarisha
umoja miongoni mwa nchi za Afrika. Ni tofauti
ambazo bado zinatawala mijadala miongoni mwa wale
wanaoamini kuwa umoja huo ni suluhisho la kuleta
kasi ya maendeleo ya kijamii na kiuchumi kwa
Waafrika.

Miaka 61 baada ya uhuru wa Ghana nchi 27 za Afrika,
ambazo ni zaidi ya nusu ya nchi zote za Afrika, ni
miongoni mwa nchi maskini kuliko zote duniani.
Tanzania ipo kwenye orodha hiyo. Aidha, wimbi
kubwa la Waafrika wanakimbilia Ulaya na nchi
nyingine tajiri kutafuta ahueni ya maisha ambayo haipo
Afrika.
Hatuna uhakika iwapo umoja aliohubiri Nkrumah
ungeleta kiwango cha maendeleo makubwa
yaliyokusudiwa, lakini yapo matokeo tunayoweza
kubashiri kutokea.
Tuna uhakika Afrika ingelazimika kuunda mikakati ya
pamoja ya viwanda, uchumi, biashara, miundombinu,
na utafiti ambayo ingepangwa kwa umoja wake na
kuepuka migongano inayozuka kwa kuwapo zaidi ya
nchi 50 ambazo zinapanga mikakati ya peke yake.
Muda mrefu unapotezwa sasa na nchi za Afrika
kujadili migongano ya aina hii.
Hazina kubwa ya Afrika ni rasilimali zake. Kwa sasa ni
rahisi kwa nchi tajiri kurubuni nchi moja moja za
Afrika kuingia mikataba yenye kuleta hasara kwa

wenye mali na kufanikisha kuhamisha faida kwa
wengine. Serikali moja ya Afrika kuunganisha taaluma
na mikakati inayolenga kulinda rasilimali zake
kungesaidia kubakisha barani Afrika sehemu kubwa ya
faida inayotokana na rasilimali zake.
Afrika ingejiongezea uzito wa sauti yake ulimwenguni.
Nchi moja ya Kiafrika inayowakilisha milioni chache
tu ya watu haiwezi kuwa na sauti na ushawishi ule ule
unaowakilishwa na Afrika moja ya watu zaidi ya bilioni
moja na milioni mia mbili. Ipo mifano kadhaa ya nchi
za Kiafrika kukosa nafasi za uwakilishi kwenye taasisi
za kimataifa kwa sababu ya kuhujumiana zenyewe kwa
zenyewe, Mwafrika mmoja akifanya kampeni dhidi ya
Mwafrika mwenzake. Hayo hayawezi kutokea kama
Afrika ni moja.
Ipo mifano ya aibu ya wawakilishi wa nchi za Afrika
kusaliti wagombea wenzao Waafrika wa nafasi za
uwakilishi kwenye taasisi za kimataifa kwa kuhongwa
nafasi za masomo kwa wanafamilia wao, au
kununuliwa chakula.

Leo hii nchi moja moja za Afrika zinapanga msululu
kwenye ofisi za taasisi za fedha za kimataifa kuomba
mikopo yenye masharti magumu yenye riba kubwa
inayozifanya nchi hizo kuwa watumwa wa kulipa
madeni kwa vizazi na vizazi. Umoja kamili wa Afrika
ungefungua fursa kwa Afrika moja kuunganisha mitaji
na kugharimia miradi ya pamoja kwa uwezo mkubwa
zaidi bila masharti magumu.
Gharama nyingi pia zingechangiwa. Tuna mfano mzuri
Dar es Salaam wa nchi tatu za Ulaya – Uingereza,
Ujerumani, na Uholanzi – waliojenga jengo moja la
ubalozi na kujipunguzia gharama za kila nchi kujenga
jengo lao. Nchi tajiri zinaunganisha nguvu zao
kupunguza gharama, wakati msululu wa nchi za Afrika
kila moja kufungua balozi kwenye nchi za nje na
kujitajirisha kwa umaskini.
Hata gharama za ulinzi zingepungua kwa sababu jeshi
lingekuwa moja. Kwa kifupi, faida ni nyingi tu na
zinahitaji nafasi kubwa kuziorodhesha zote.
Nkrumah alitahadharisha kuwa kuchelewesha umoja ni
kuchelewesha maendeleo ya Bara la Afrika. Si hivyo tu,

muda utakavyozidi kupita mizizi ya utengano
itashamiri na ari ya kuchukua hatua za kufikia umoja
kamili itapungua.
Hayo yametimia kwa kiasi fulani. Anapotokea kiongozi
wa Afrika anayehimiza umoja wa kisiasa anasemwa
kuwa anasukumwa na tamaa ya kuongoza wenzake.
Lengo kuu la kufikia umoja linafunikwa na hofu ya
nani atakayeongoza wenzake.
Na ajenda ya Umoja Sasa!, kama Nkrumah
alivyohimiza, sasa imekuwa ajenda ya mwaka 2063,
inayojulikana rasmi ndani ya Umoja wa Afrika kama
‘Agenda 2063’ au mikakati ya kuimarisha ushirikiano
miongoni mwa nchi za Afrika. Hatuna tena haraka ya
kuungana, tunataka kukaa, kujadili, na kujiandaa kwa
mipango ya kisekta kuelekea mwaka 2063.
Tumechelewa? Hapana, kwa sababu hakuna tarehe ya
mwisho ya kujikwamua kutokana na unyonge
unaotukabili. Tunajifunza? Ndiyo, lakini polepole sana.

1824 Total Views 1 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!