Aliposhika Biblia na kuapa kuwa Rais wa tano wa Tanzania Novemba, mwaka 2015, Dk. John Magufuli, aliahidi kuleta mabadiliko makubwa kiuchumi na kijamii.

Aliahidi kuipeleka Tanzania kwenye kipato cha kati kupitia uchumi wa viwanda. Alipolihutubia Bunge baadaye mwaka huo, akajipa kazi ya kutumbua majipu, akimaanisha kuondoa uozo uliozoeleka serikalini na katika taasisi za umma.

Miaka minne baadaye, tathmini inaonyesha kuwa kwa kiasi kikubwa anafanikiwa kutekeleza yale aliyoahidi. Ingawa bado kuna matatizo, lakini mwelekeo unaonyesha kuwa Tanzania ambayo Dk. Magufuli aliahidi inatimia. 

Moja kati ya mambo yaliyomjengea sifa ya kipekee Rais Dk. Magufuli ni ujasiri wake wa kutekeleza mambo ambayo awali Watanzania wengi, na watu wengine kutoka nje ya Tanzania, waliamini kuwa hayawezi kutekelezwa hivi sasa.

 Ipo mifano kadhaa kama vile utekelezaji wa miradi mikubwa ya kimkakati, safishasafisha serikalini na uamuzi wa kuhamia Dodoma. 

Kazi kubwa ya ujenzi wa uchumi na kurudisha nidhamu ya utendaji serikalini ni mambo ambayo bado yanabakia kuwa kielelezo cha utendaji wa Serikali ya Awamu ya Tano.

Uchumi wa viwanda

Kazi ya ujenzi wa viwanda imeshika kasi nchini kote. Hadi mwezi uliopita, tayari zaidi ya viwanda 4,000 vya ngazi mbalimbali vilikuwa vimejengwa nchini kote kwa mujibu wa Dk. Magufuli.

Pamoja na kuongeza ajira, viwanda hivyo pia vimeongeza uwezo wa Tanzania kuzalisha bidhaa ambazo baadhi yake zinauzwa nje ya nchi. 

Pamoja na kuongezeka kwa uwezo huo, lakini bado Tanzania inaagiza bidhaa nyingi kutoka nje, jambo linalotokana na ujenzi wa viwanda vipya, kwani nchi inalazimika kuagiza mitambo na malighafi nyingi kwa ajili ya ujenzi wa viwanda na kuhudumia vile ambavyo vimekwisha kuanza kazi.

Watalaamu wa uchumi wanabainisha kuwa kinachotakiwa hivi sasa ni nchi kuongeza uzalishaji wa malighafi ili viwanda vipunguze au kuacha kabisa kuagiza malighafi kutoka nje. 

Katika hotuba yake ya Bajeti ya 2019/20, Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, alilieleza Bunge kuwa ili kuhakikisha uchumi wa viwanda unakua, serikali imeshatenga jumla ya ekari 127,859 kwa ajili ya matumizi ya viwanda. 

Amesema serikali kwa kushirikiana na mamlaka za upangaji za halmashauri za wilaya za Kibaha na Kilosa, imetenga hekta 2,710 za ardhi kwa ajili ya uwekezaji wa viwanda vikubwa na vidogo.

Waziri Mkuu amesema serikali imeziagiza Mamlaka za Upangaji zizingatie utengaji wa asilimia 10 ya kila eneo la mpango kabambe wa mji kwa ajili ya uwekezaji wa biashara na viwanda.

 Amesema katika mwaka 2018/2019, serikali imeandaa mwongozo wa tathmini ya mazingira kimkakati ambao utawezesha mpango wa uchumi na viwanda kufanyiwa tathmini ya mazingira kimkakati.

Miradi ya kimkakati

Moja kati ya mambo ambayo yameifanya Serikali ya Awamu ya Tano ionekane ni ya tofauti ni utekelezaji wa miradi mikubwa ya kimkakati. Mingi ya miradi hiyo inatekelezwa kwa kutumia fedha za ndani, jambo ambalo limewafanya watu wengi ndani na nje ya nchi wasiamini.

Mara zote Rais Magufuli mwenyewe amekaririwa akisema kuwa Tanzania ina uwezo mkubwa kifedha kutekeleza miradi yake na amelithibitisha hilo kutokana na hatua za kubana matumizi na kuhakikisha fedha zinazokusanywa zinatumika ipasavyo. 

Baadhi ya miradi mikubwa ambayo serikali inaitekeleza hivi sasa ni ujenzi wa bwawa kubwa la Nyerere la kuzalisha umeme kwa nguvu ya maji.

Bwawa hilo linalojengwa katika Wilaya ya Rufiji, mkoani Pwani, litakuwa na uwezo wa kuzalisha megawati 2,115 za umeme na kuifanya Tanzania kuwa moja ya nchi zinazozalisha umeme kwa wingi barani Afrika. 

Bwawa hilo litakalokuwa la nne kwa ukubwa barani Afrika, litaiwezesha Tanzania kuzalisha umeme mwingi kwa ajili ya kuhudumia viwanda na kubaki na ziada ya kuuza nje ya nchi.

Mradi huu ulibuniwa na Serikali ya Awamu ya Kwanza lakini haukutekelezwa kutokana na kuelezwa kuwa gharama zake zilikuwa kubwa kwa Tanzania kumudu. 

Lakini Rais Magufuli amesema kuwa hiyo si sababu ya msingi na amedhihirisha hilo kwa kutoa fedha za serikali kwa ajili ya utekelezaji wa mradi huo unaogharimu zaidi ya Sh trilioni 7.

Pia kuna mradi wa ujenzi wa reli ya kisasa (SGR) kutoka Dar es Salaam hadi Kigoma. Awali, ilielezwa kuwa mradi huo ni wa gharama kubwa lakini Serikali ya Awamu ya Tano imefanikiwa kupata fedha kwa ajili ya kuanza utekelezaji wa mradi huo. 

Tayari kazi imeshaanza katika kipande cha Dar es Salaam – Morogoro na Morogoro – Dodoma. Hivi sasa serikali ipo katika mchakato wa kuwapata wakandarasi kwa ajili ya vipande vilivyosalia kuelekea Kigoma na Mwanza. 

Reli hiyo ya kisasa itarahisisha usafiri na usafirishaji wa abiria na mizigo. Kwa kuwa ni pana kuliko reli ya sasa, itakuwa na uwezo wa kubeba mzigo mwingi zaidi. Aidha, ikiwa na kasi ya zaidi ya kilometa 160 kwa saa, reli hiyo itapunguza muda wa usafiri.

Ujenzi wa barabara za juu katika eneo la Ubungo jijini Dar es Salaam na ujenzi wa barabara nane kati ya Kimara na Kibaha mkoani Pwani ni miradi mingine kielelezo inayotekelezwa na serikali hivi sasa.

Zitakapokamilika, barabara hizo zitaleta ahueni kubwa miongoni mwa wasafiri na wasafirishaji katika maeneo hayo na nchi kwa ujumla, kwa sababu barabara hiyo ni kiungo muhimu kati ya Bandari ya Dar es Salaam ambayo ndiyo lango kuu la kiuchumi nchini.

Daraja la Mfugale Jijini Dar es Salaam ni mradi mwingine ambao umesaidia sana kuondoa kero ya msongamano wa magari katika Barabara ya Nyerere.

Ziwa Victoria

Kuna miradi kadhaa inayoendelea katika Ziwa Victoria, ambako serikali imewekeza zaidi ya Sh bilioni 300 kuimarisha miundombinu ya usafiri katika ziwa hilo kubwa kuliko yote barani Afrika.

Pamoja na ukarabati wa meli zinazofanya kazi hivi sasa, lakini serikali imetenga kiasi cha Sh bilioni 150 kwa ajili ya ujenzi wa meli mpya ya kisasa kutoa huduma za usafiri katika ziwa hilo. Kazi ya ujenzi wa meli hiyo imeashaanza.

Pia kuna mradi wa ujenzi wa daraja lenye urefu wa kilometa 3.2, refu kuliko yote katika Ziwa Victoria, kati ya Kigongo na Busisi likiunganisha mikoa ya Mwanza na Geita.

Rushwa na utendaji

Kati ya mambo ambayo yamemwezesha Rais Magufuli kuheshimika si tu katika ukanda wa Afrika Mashariki, bali Bara lote la Afrika na nchi nyingine duniani, ni ujasiri wake katika kupambana na rushwa, ubadhirifu na uzembe, hasa miongoni mwa watumishi wa umma. 

Baadhi ya vyombo vya habari nje ya nchi vimefikia hatua ya kumpachika jina la ‘bulldozer’, yaani katapila, kutokana na kutokuwa na simile pale anaponusa harufu ya rushwa na ubadhirifu.

Moja katika hatua madhubuti ambazo zimechukuliwa na Serikali ya Awamu ya Tano katika eneo hilo ni kuunda mahakama maalumu inayoshughulikia makosa ya rushwa na uhujumu uchumi.

Mahakama hiyo maarufu kama mahakama ya mafisadi, tayari imeshaanza kazi na sasa kesi kadhaa zinaendeshwa huko.

Aidha, Dk. Magufuli amekuwa hana uvumilivu kuwaondoa viongozi na watendaji ambao wanashindwa kuendana na kasi ambayo yeye angependa serikali iwahudumie wananchi. 

Katika kazi yake aliyojipa ya kutumbua, Dk. Magufuli amekuwa akifanya mabadiliko ya mara kwa mara ya viongozi na watendaji katika ngazi zote kuanzia na Baraza la Mawaziri. Mwenyewe ameshawahi kusema kuwa hakuna aliye salama katika serikali yake. 

Mabadiliko ya wakurugenzi wa wilaya, mikoa, taasisi za umma, wakuu wa wilaya, wakuu wa mikoa, mawaziri na watendaji wa taasisi za umma ni jambo la kawaida katika Serikali ya Awamu ya Tano.

Mathalani, ni mawaziri wchache sana ambao Dk. Magufuli alianza nao alipounda serikali kwa mara ya kwanza bado wanaendelea kuwemo kwenye Baraza la Mawaziri hivi sasa.

Charles Kitwanga, ambaye anaelezwa kuwa mtu wa karibu sana na Dk Magufuli, Nape Nnauye na Januari Makamba ambao ni miongoni mwa watu wanaoaminika kufanya kazi kubwa wakati wa kampeni kufanikisha ushindi wa CCM katika uchaguzi uliopita, ni miongoni mwa watu ambao Dk. Magufuli hakusita kuwatumbua pale alipoamini kuwa wamemwangusha.

Wafanyakazi hewa

Katika kipindi cha miaka minne, Dk. Magufuli tayari amefanikiwa kuondoa zaidi ya wafanyakazi hewa 20,000 kutoka kwenye orodha ya watumishi wa umma.

Watumishi hao hewa walikuwa wakilipwa mabilioni ya shilingi kila mwezi kama mishahara na stahili nyingine.

Kampeni ya kuwaondoa wafanyakazi hewa iliendana na kuwaondoa katika utumishi wa umma watumishi ambao hawakuwa na sifa za elimu inayotakiwa. 

Maelfu ya watumishi wa umma ambao hawakuwa na vyeti stahiki waliondolewa baada ya zoezi la uhakiki lililowahusisha watumishi wote wa umma.

Huduma za jamii

Kumekuwa na uboreshaji wa upatikanaji wa huduma za jamii katika sekta za afya, elimu na maji. Utekelezaji wa miradi hiyo umeboresha na kurahisisha upatikanaji wa huduma za kijamii katika maeneo mengi nchini.

Elimu bure

Moja kati ya mambo ambayo Dk. Magufuli na serikali yake ililitumia kujitambulisha kwa Watanzania ni mpango wa kufuta ada katika shule za serikali kuanzia shule za msingi hadi sekondari.

Chini ya mpango huo ujulikanao kama ‘Elimu Bure’ serikali hutoa zaidi ya Sh bilioni 23 kila mwezi kugharamia masuala ya elimu katika ngazi husika. 

Mpango huo umesaidia kuongeza idadi ya watoto wanaojiunga na elimu ya msingi nchini na kuibua matatizo mengine kama vile uhaba wa vyumba vya madarasa, walimu, nyumba za walimu na vifaa vya kufundishia. 

Hayo nayo yameshughulikiwa, kwani katika miaka michache iliyopita serikali imeajiri walimu wengi na kuongeza upatikanaji wa vifaa vya kufundishia katika shule zote nchini. 

Ujenzi wa madarasa nalo ni jambo ambalo lilishikiwa bango na kuwezesha watoto wengi kupata maeneo mazuri ya kujifunzia.

Afya

Sekta ambayo imepiga maendeleo makubwa katika eneo la ustawi wa jamii ni afya, ambako vituo zaidi ya 300 vya kutolea huduma za afya vimejengwa nchini kote. Vituo hivyo vinahusisha zahanati, vituo vya afya, hospitali za wilaya, hospitali za rufaa za mikoa na hospitali za rufaa za kanda.

Hili limefanikiwa chini ya mpango wa ujenzi wa zahanati kila kijiji na kituo cha afya kila kata. Aidha, serikali imejenga zaidi ya hospitali za wilaya 70 nchini kote kwa mara moja, jambo ambalo halijawahi kufanyika tangu Uhuru.

Serikali pia imefanikiwa kuimarisha Kituo cha Saratani cha Ocean Road na Taasisi ya Tiba ya Magonjwa ya Moyo ya Jakaya Kikwete, hivyo kuongeza uwezo wa nchi kukabiliana na magonjwa hayo makubwa mawili. 

Uboreshaji wa Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete, mathalani umeiwezesha Tanzania sasa kupokea wagonjwa wa moyo kutoka nchi nyingine wanaohitaji matibabu ya moyo.

Idadi ya Watanzania wanaosafirishwa nje ya nchi kwa ajili ya matibabau ya moyo nayo imepungua kwa kiasi kikubwa kwa sababu watu wengi sasa wanatibiwa nchini. 

Wakala wa Dawa nchini, MSD, nayo imeongezewa uwezo kupitia ongezeko la bajeti ya kununulia dawa kutoka Sh bilioni 29 hado Sh bilioni 262.

Sekta ya nishati

Ukiacha ujenzi wa Bwawa la Kuzalisha Umeme la Nyerere, serikali imefanya kazi kubwa kuhakikisha nchi inakuwa na umeme wa uhakika. 

Shirika la Umeme nchini, Tanesco, limefanya kazi kubwa ya kuhakikisha kuwa uzalishaji, usafirishaji na usambazaji umeme unaimarika nchini kote ili kuwawezesha Watanzania wengi kupata huduma hiyo muhimu. 

Chini ya mipango ya Tanesco, uzalishaji wa umeme kutoka vyanzo mbalimbali umeongezeka kiasi kwamba hivi sasa nchi inazalisha umeme wa ziada. 

Miradi kama vile Kinyerezi I, II, na III, mradi wa ujenzi wa bomba la gesi kutoka Mtwara hadi Dar es Salaam ni kati ya mambo ambayo yamewezesha uzalishaji wa umeme wa kutosha nchini.

Kama hilo halitoshi, Tanesco imejikita pia katika uzalishaji wa umeme kutoka vyanzo vingine kama vile jotoardhi katika mradi mkubwa unapangwa kufanyika katika Ziwa Ngozi mkoani Mbeya.

Ili kuhakikisha kuwa wananchi wengi wanapata umeme, serikali ilikuja na mpango wa umeme vijijini na kuanzisha Wakala wa Umeme Vijijini (REA) ambaye hadi hivi sasa ameshafanya kazi kubwa kuhakikisha kuwa vijiji vingi vinaunganishwa kwenye mfumo wa umeme. Katika wamu ya tatu ya miradi ya REA, vijiji vyote nchini vitapatiwa umeme. 

Katika usafirishaji, Tanesco imetekeleza miradi kadhaa mikubwa ukiwamo mradi ujulikanao kama ‘Backbone’ uliohusisha ujenzi wa njia ya kusafirisha umeme wa msongo wa kilovolt 400 kutoka kituo cha Tegamenda mkoani Iringa hadi Ibadakuli, Shinyanga.

Ujenzi wa nia hiyo kumeiwezesha Tanesco kusafirisha megawati 2,000 za umeme kwa mara moja kuelekea katika maeneo ambako njia hiyo inapita katika mikoa ya Dodoma, Singida na sehemu ya Mkoa wa Tabora. 

Aidha, tanesco hivi sasa inatelekeleza mradi mwingine wa ujenzi wa njia kama hiyo ya umeme kutoka Singida hadi Namanga kwenye mpaka na Kenya. Njia nyingine ya umeme yenye uwezo huo itajengwa kuelekea maeneo ya Nyanda za Juu Kusini.

Kukamilika kwa miradi hiyo kutaiweka Tanzania katika nafasi nzuri ya kufanya biashara ya umeme kwani itakuwa ina uwezo wa kuunganisha nchi za Kusini na Mashariki ya Afrika.

Hii ndiyo sababu inayowafanya wataalamu wengi wa uchumi kuipongeza serikali kuamua kujenga Bwawa la Nyerere litakalozalisha megawati 2,115 za umeme, kwani Tanzania itakuwa kwenye nafasi nzuri ya kuuza umeme huo.

Kuhamia Dodoma

Kati ya mambo ambayo yaliwakatisha tamaa Watanzania na kuamini kuwa hayawezi kufanywa na serikali ni kuhamishia makao makuu wa serikali Dodoma. 

Kwa mara ya kwanza dhamira ya kuhamia Dodoma kutoka Dar es Salaam ilielezwa na rais wa kwanza wa Tanzania, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, katika miaka ya 1970 akizitaja sababu za kilojistiki kuwa ndizo zilisukuma azima yake hiyo. 

Jambo hilo lilisisitizwa na kila rais aliyefuata baada ya Rais wa kwanza na Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere lakini hakuna aliyefanikiwa kuhamisha makao makuu ya nchi mpaka zaidi ya miaka 49 baadaye. 

Rais Magufuli alipotamka kuwa atakahakikisha serikali inahamia Dodoma, wengi walidhani kuwa ni sehemu ya ahadi hewa ambazo zilikwisha kutolewa na viongozi wakuu wote waliopita. Lakini hivi sasa serikali yote, akiwamo rais mwenyewe, imeshahamia Dodoma.

Ununuzi wa ndege

Jambo jingine kubwa ambalo serikali imelifanya katika miaka minne iliyopita ni ununuzi wa ndege ambazo zimetumika kulifufua shirika la ndege Tanzania, ATCL. 

Hadi hivi sasa, ndege nane mpya tayari zimeshaingia nchini zikiwa chini ya Wakala wa Ndege za Serikali ambaye amezikodisha kwa ATCL. Ndege nyingine tatu zimeshafanyiwa oda na zinatengenezwa. 

Katika kipindi hiki kifupi cha miaka minne, sasa ATCL imeungana na mashirika ya ndege Afrika ambayo yanaendesha ndege aina ya Boeing 787 Dreamliner na toleo jipya la ndege aina ya Airbus 320-200. 

Jambo kubwa katika hili ni kuwa ndege hizo zimenunuliwa kwa fedha taslimu, hivyo kutoacha deni lolote kwa nchi. Aidha, serikali imenunua ndege hizo moja kwa moja kutoka kwa watengenezaji bila kupitia kwa madalali ambao wangeweza kuongeza bei. 

Hivi sasa ATCL imeanza kujijengea uwezo wa kushindana katika soko ikiwa imeshaanza safari kadhaa za kimataifa huko India, Zambia na nchi nyingine za Afrika Mashariki. Safari za Afrika Kusini zilisitishwa kutokana na machafuko ya ubaguzi yaliyotokea nchini humo hivi karibuni.

Bandari

Ikiwa ni lango kuu la uchumi, maendeleo ya bandari yamepewa msukumo wa kipekee na Serikali ya Awamu ya Tano.

Katika miaka ya hivi karibuni imeshuhudiwa upanuzi wa bandari na kuanzishwa kwa bandari nyingine mpya kama sehemu ya kuongezea wigo Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA).

Upanuzi mkubwa umefanyika katika Bandari ya Dar es Salaam ambayo sasa ina uwezo wa kupokea meli kubwa ya aina yoyote.

Aidha, uboreshaji wa bandari za maziwa kumeiwezesha Bandari ya Mwanza kuanza kupokea shehena kubwa inayosafirishwa kwa reli kuelekea Uganda. 

Serikali pia imekwisha kununua meli mpya kwa ajili ya maziwa makubwa yote nchini ya Victoria, Tanganyika na Nyasa. Kazi ya ujenzi wa meli hizo za mizigo na abiria inaendelea.

Rekodi za safari

Tofauti na viongozi wengi wa Afrika na hata duniani, Rais Magufuli ameweka rekodi ya kutosafiri mara kwa mara nje ya nchi.

Katika miaka minne madarakani, Rais Magufuli hajawahi kufanya safari yoyote nje ya Bara la Afrika. Safari chache alizozifanya ni ndani ya Afrika na kwa kiasi kikubwa ni katika eneo la Afrika Mashariki. 

Imekuwa ni kawaida ya viongozi wengi wa Afrika kufanya safari za nje, hasa Ulaya na Marekani wakidai kuwa safari hizo zinawawezesha kuwasiliana na wahisani na wawekezaji moja kwa moja.

Lakini licha ya Dk. Magufuli kutosafiri nje ya nchi kwa kipindi hicho, Tanzania imeendelea kuwa moja ya nchi ambazo zimeendelea kuvutia wawekezaji. Wahisani nao wameendelea kufanya kazi na Tanzania kwa karibu licha ya Dk. Magufuli kutosafiri kwenda kwenye nchi zao.

Siasa

Kumekuwa na malalamiko kutoka kwa vyama vya upinzani nchini kuwa licha ya kufanya vizuri kwenye uchumi serikali imebana sana demokrasia. 

Wanatoa mifano ya kuzuiwa kwa mikutano ya vyama vya siasa na wapinzani kukamatwa na kufunguliwa kesi kuwa moja ya vigezo vinavyoonyesha kuwa demokrasia inaminywa nchini.

Hata hivyo, Rais Magufuli amekuwa akisisitiza kuwa siasa ndilo jambo ambalo kwa muda mrefu limekwamisha maendeleo nchini, kwani watu wanashindwa kushiriki kwenye shughuli za maendeleo kisa siasa. 

Viongozi wengine wa serikali nao wamekuwa wakisisitiza kuwa hakuna aliyekatazwa kufanya siasa nchini, kwani viongozi wa kuchaguliwa kama vile wabunge na madiwani wanaruhusiwa kufanya kazi za kisiasa katika maeneo yao. 

Haya ni kati ya mambo makubwa mengi Serikali ya Awamu ya Tano imeyafanya katika kipindi cha miaka minne iliyopita. JAMHURI linakuahidi kuwa litaendelea kukuletea mambo yaliyofanyika katika kipindi hicho na changamoto ambazo serikali ya Dk. Magufuli inakabiliana nazo katika ujenzi wa Tanzania mpya.

By Jamhuri