Miongoni mwa vitu vinavyowavutia wapenzi wa michezo ni kuona nchi inasonga mbele kimichezo, kwa kufanya vizuri hadi ngazi ya kimataifa.

Moja ya mambo yanayoweza kuboresha michezo ni kuwa na viongozi bora ambao pia wana upeo kimichezo na wanaweza kuongoza michezo.

Ubora wa viongozi unapimwa kutokana na utendaji wao ambao kwa namna moja ama nyingine lazima uambatane na mipango thabiti inayolenga kuboresha na hatimaye kukuza michezo.

Lakini pia mafanikio ya viongozi yanatokana na ushirikiano wa wadau wengine wa michezo. Kwa hali ilivyo sasa Watanzania tunatakiwa kujipanga upya katika ulimwengu wa michezo kutokana na rekodi mbaya iliyopo kwa sasa.  Tumejaribu soka ambalo linapendwa na wengi, hadithi imebaki kuwa ile ile ya kujisogeza karibu na mafanikio, lakini mwisho wa siku hakuna kitu. Kuna haja ya kujiuliza chanzo cha kuboronga kila mchezo na kuanza upya ili kujijenga.

Kuna haja ya kurudi nyuma na kujiuliza: Je, Watanzania waliopata kufanya vizuri katika anga za kimataifa walifanyaje hadi wakafikia hapo? Filbert Bayi na Juma Ikangaa ni mfano wa wanamichezo waliopata kufanya vizuri katika medani za kimataifa kwa upande wa mchezo wa riadha.

Lakini pia, tujiulize kwamba nyakati zile za miaka ya 1980 ilikuwaje timu ya soka ya Tanzania, Taifa Stars, ikaweza kushiriki Kombe la Mataifa ya Afrika? Mipango iliyofanyika wakati ule imeshindikana kwa wakati huu?

Natamani kama Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere, angefufuka leo akashuhudia jinsi baadhi ya michezo ilivyosahaulika na kutoa kipaumbele kwa michezo michache kwa sababu ya maslahi ya watu wachache. Kuna harufu ya unyonyaji katika kuendeleza michezo ya sasa. Hali ilivyo kwa sasa, mchezaji mpira akicheza soka ananyonywa, mcheza filamu naye ananyonywa na msambazaji wake kwani wakitoa nyimbo zao na albamu zao zinaishia katika mikono ya watu wachache.

Hali hii inaonekana pale kunapokosekana mgawanyo sawa wa mapato kutokana na kadiri mtu alivyovuja jasho. Imefikia hatua sasa hakuna anayefikiria kukuza michezo mingine zaidi ya soka na ngumi au michezo ya filamu kwa sababu wengi wamegundua kuwa hapo ndipo kuna maslahi ya chap chap.

Kuna michezo mingi ambayo kama Taifa litahamasisha vijana tutapata wachezaji wazuri kwa wakati ujao. Kwa mfano, michezo inayohitaji kuhamasishwa ni kama vile kulenga shabaha, kutupa mkuki, kutupe jiwe, kuendesha baiskeli, kuogelea, kuruka juu, kuruka chini, kunyanyua vitu vizito, na mingineyo mingi ambayo naona siku hizi imekufa kabisa nchini kwetu, lakini kwa wenzetu inaendelea kuwapatia medali katika mashindano ya kimataifa.

Jana ilikuwa siku ya kumbukumbu ya kifo cha Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere, anayetimiza miaka 14 tangu alipofariki dunia. Kuna haja ya kumuenzi Mwalimu kwa kukuza michezo ya jadi ili nayo iwe na nafasi kama ilivyo michezo mingine.

Wakati wa Mwalimu kulikuwa na timu za mashirika ya umma kama vile RTC Kagera, NMC, timu za benki, Pamba ya Mwanza na nyinginezo. Zilikuwa zinafanya vizuri na hatimaye kutoa wachezaji wazuri na wenye uwezo wa kufanya vizuri. Haya yote yamesahaulika, kilichobaki ni maslahi mbele na visingizio lukuki.

Soka limepewa kipaumbele sana, lakini pia kumekuwa na upungufu mwingi ambao unahitaji kufanyiwa marekebisho. Kuna haja ya kurudi chini kutafuta vipaji ili kujenga wachezaji wazuri kwa kizazi kijacho.

Hivi karibuni, nilimsikia Rais mpya wa Chama cha Soka Afrika Kusini, Danny Jordaan, akisema kuwa kuna haja ya nchi hiyo kuweka mipango ya kukuza soka la vijana na kuwa na mashindano ya vijana kwa kila jimbo, jambo ambalo anaamini kuwa linaweza kukuza soka nchini humo. Kiongozi huyo anakubali kuwa Afrika Kusini ni nchi tajiri, lakini tatizo kubwa alilolisema ni kutokuwa na mipango thabiti ya kukuza soka.

Mipango kama hiyo ndiyo imekuwa ikisemwa na wadau wengi hapa nchini kuliko kukimbilia kuchagua wachezaji kutoka Simba, Yanga na Azam ili kuunda timu ya Taifa.

Watanzania tumetawaliwa na ile tabia ya zimamoto katika suala la kuchagua wachezaji pale wanapotakiwa kuunda timu, na hii ni katika michezo yote na wala si soka peke yake.

Wachezaji wanakaa kambini muda mfupi, baadaye wanakwenda kama ni Olimpiki au Jumuiya ya Madola. Wakirudi kutoka huko mikono mitupu visingizio huwa ni maandalizi ya muda mfupi, mara wenzetu walikuwa na uzoefu. Sasa tutaenda kwa visingizio hivi mpaka lini?

Tatizo jingine ambao linaweza kuchangia katika hili ni wadhamini  kukosa ushauri mzuri kutoka kwa viongozi wa mchezo husika. Kila kiongozi anataka apate mdhamini wa kudhamini mashindano yatakayofanyika muda mfupi, ili naye apate chake badala ya kuwa na mipango ya muda mrefu yenye lengo la kukuza vipaji.

Ni dhahiri kuwa ukuzaji wa michezo unakwenda sambamba na uwepo wa viwanja ambapo kutakuwa na uwezekano wa kuwa na mashindano ya mara kwa mara. Kuna umuhimu kwa viongozi wa vyama mbalimbali vya michezo kutoa mapendekezo kama haya kwa wadhamini pale wanapojitokeza ili wajenge tabia ya kuwa na programu za kukuza vipaji.

Kwa mfano, tatizo la ubovu wa viwanja vya kuchezea soka kwa sasa limekuwa sugu hapa nchini. Viwanja vingi vimekuwa vikilalamikiwa na baadhi ya timu kutokana na kukosa viwango na hasa pale vinapotumiwa katika mechi za Ligi Kuu za soka Tanzania Bara.

Matatizo haya ya ubovu wa viwanja hayajaanza leo, jana wala juzi bali ni ya muda mrefu na yamekuwa yakilalamikiwa bila mafanikio. Kuna viwanja vingi ambavyo viko chini ya viwango kuanzia milango yake, majukwaa, dimba na hata vingine vina kuta fupi na zenye matundu.

Kwa mtizamo wa haraka, tatizo kubwa la ubovu wa viwanja linasababishwa na matumizi mabaya ya viwanja hivyo. Kwa mfano, leo kiwanja kinatumika kwa mkesha wa tamasha la burudani, kesho mchana kuna mechi ya Ligi Kuu. Je, kwa mtindo huo tutaweza kuwa na viwanja bora au bora viwanja?

0783 106 700


1515 Total Views 1 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!