*Wanasiasa, wafanyabiashara washushiwa lawama

Maelfu ya ng’ombe na mifugo mingine imeingizwa ndani ya Pori la Akiba la Maswa.

Inakadiriwa kuwa asilimia 30 hadi 40 ya pori hilo imemezwa na mifugo hiyo. Wingi wake umesababisha wanyamapori wengi wakimbie.

Wamiliki wa vitalu vya uwindaji ndani ya eneo la Maswa wamelalamikia hali hiyo, na kwamba licha ya juhudi zao za kuwaondoa ng’ombe na mifugo mingine kwa gharama zao, hali inaendelea kuwa mbaya.

 

Walalamika kuwa uvamizi huo unafanywa kwa ushawishi wa baadhi ya wafanyabiashara, wanasiasa na viongozi wa Serikali wenye mifugo na wengine wenye malengo ya kutaka kuungwa mkono na wafugaji.

 

Imeelezwa kwamba wanasiasa, licha ya kuwa wao pia ni wafugaji, wamekuwa wakitetea wafugaji wa asili ya Kisukuma, kuingiza mifugo ndani ya pori hilo kwa lengo la kuwa nao karibu kwa manufaa yao kisiasa.

 

Uingazaji mifugo ndani ya Mapori ya Akiba, Mapori Tengefu na Hifadhi za Taifa ni kinyume cha kifungu cha 111 cha Sheria ya Wanyamapori ya mwaka 2009 na Kanuni zake za mwaka 2010.

 

Baadhi ya wamiliki wa vitalu ndani ya Maswa wameshakutana na Mkurugenzi wa Idara ya Wanyamapori, Profesa Alexander Songorwa; na kwamba bado hakujakuwapo mabadiliko yenye mwelekeo wa kupunguza na hatimaye kumaliza tatizo la uingizaji mifugo ndani ya Pori la Akiba la Maswa.

 

“Kuna wakati tunalazimika kuamini kuwa huenda faini wanazopigwa wenye mifugo wanaopatikana ndani ya Pori, zinaifanya Idara ya Wanyamapori ione ni muhimu kwa mifugo kuendelea kuwapo kwa ajili ya kuwaingizia mapato,” kimesema chanzo chetu.

Msemaji wa Wizara ya Maliasili na Utalii, George Matiko, alipoulizwa, alikiri kuwapo kwa tatizo la uvamizi wa mifugo ndani ya Pori la Akiba la Maswa, lakini akasema hali hiyo imekuwa ikidhibitiwa na askari wanayamapori.

 

“Tatizo la Maswa lipo kweli, linatokea mara kwa mara – askari wetu mara kadhaa wameuawa kwa sababu ya kulinda wanyamapori – taarifa zilizopo ni kuwa hali hiyo ilishapungua, kama imeibuka, basi itakuwa kwa sasa. Wizara iko makini kuhakikisha inalinda mapori na hifadhi, lakini pia wananchi wanapaswa watupatie ushirikiano hasa kwa kuheshimu sheria zilizopo,” amesema Matiko.

 

Hadi tunakwenda mitamboni, Meneja Mradi wa Pori la Akiba Maswa, Benjamin Andulenge, hakupatikana kupitia simu yake ya mkononi.

 

1455 Total Views 1 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!