*Alianza kwa Muumin, kisha Dimond

*Sasa amedakwa na Wema SepetuNi msanii chipukizi, kijana mdogo mwenye umri wa miaka 21. Kwa sasa amedakwa na msanii maarufu na Miss Tanzania 2006, Wema Sepetu. Huyu kijana si mwingine yeyote bali ni Best Werema maarufu kwa jina la Bestizzo. Kwa sasa ni mwajiriwa katika kampuni ya Wema Sepetu inayojulikana kama Endless Fame Production.

Katika mahojiano JAMHURI Dar es Salaam hivi karibuni, Bestizzo amesema kwa sasa ndiye msimamizi wa website ya Wema, yaani www.wemasepetutz.com

 

“Kazi yangu kubwa ni kuandaa habari, kupiga na kurekodi picha za matukio mbalimbali pamoja na za behind the scenes (nyuma ya pazia) ya Wema Sepetu na kuviweka kwenye website yake.

 

“Lakini pia Meneja wa Wema, Martin Kadinda, huwa anazipitia kazi zote kabla ya mimi kuziweka kwenye website.

 

“Hivi sasa mimi ni mwajiriwa wa Endless Fame Production. Hii ni kampuni yetu, mimi ni mtoto wa hapo kabisa,” anasema Bestizzo.

 

Anasema kwa sasa anajiona Bestizzo mpya tofauti na wa zamani. Kwamba anajisimamia kwa kila kitu.

 

“Sasa hivi ninaweza kumudu maisha, ninajinunulia nguo, ninasomesha mdogo wangu Lilian Werema na kumsaidia mama yangu mzazi, mama Best,” anasema.

 

Pia msanii huyu chipukizi anasaidia kusimamia websites za wasanii wakiwamo Barnabas Boy kutoka Tanzania House of Talent (THT) na Robby One Fashion.

 

Kwa mujibu wa Bestizzo, kabla ya kujiunga kwenye kampuni ya Wema, alikuwa akifanya kazi na msanii maarufu nchini, Diamond Platinum.

 

“Diamond ndiye aliyenionesha njia, amenitangaza, nimefanya kazi naye watu wamenijua zaidi, ninatambua mchango wake mkubwa kwangu, nilikuwa Bestizzo wa Diamond, sasa ni Bestizzo wa Wema,” anasema Bestizzo.

 

Anaendelea kueleza kuwa kabla ya kujiunga na Diamond, alitokea kwa msanii mwingine maarufu nchini, Muumini Mwinjuma, aliyemfundisha muziki kwa kipindi cha mwaka mmoja.

 

“Muumini amenifundisha muziki, sasa ninajua muziki ni nini na sifa za msanii. Ingawa sikuwa nalipwa ujira lakini nimepata mafanikio makubwa kwa msanii huyo.

 

“Nilipokuwa kwa Muumini nilitunga nyimbo nyingi lakini ulioko studio ni mmoja nilioupatia jina la ‘Mpweke’ ambao niliurekodi katika studio ya Eck Production ya hapa Dar es Salaam,” anasema.

 

Je, Bestizzo ana ujumbe gani kwa wasanii wa Tanzania? Anawahimiza kujiendeleza kielimu na kitaaluma kujijengea mazingira mazuri ya kujiinua kiuchumi kupitia fani hiyo.

 

“Wasanii tusome kwani bila elimu hatuwezi kufanikiwa ipasavyo. Siku hizi ni vigumu kwa mtu kufanikiwa kutokana na kipaji chake pekee bila kukiongezea elimu,” anasisitiza.

 

Anatunia nafasi hii kuwashauri wasanii nchini kufanya kazi kwa bidii na kujiepusha na imani potovu za ufreemason na ushirikina.


“Lakini pia wasanii tusiwe watu wa kuiga wasanii wa nje, baada ya kuwasoma kwenye mitandao, tuepuke kuiga vitu visivyoendana na utamaduni wa Kitanzania,” anaongeza.

 

Kwa upande mwingine, Bestizzo anatoa wito kwa Watanzania kuepuka kughushi na kununua kazi bandia za wasanii, badala yake wajenge utamaduni wa kununua kazi halisi za wasanii wa Tanzania ili kuwainua kiuchumi kwa manufaa ya Taifa kwa jumla.

 

Bestizzo alipata elimu ya msingi katika Shule ya Turwa kati ya mwaka 2000 na 2006 na elimu ya sekondari katika Shule ya Nkende kati ya mwaka 2007 na 2010, zilizoko Wilaya ya Tarime mkoani Mara.


Please follow and like us:
Pin Share