Nilipokuwa nchini Ghana kwa mafunzo ya vitendo mwishoni mwa miaka ya ’80, nilishangazwa na daktari mmoja. Nakumbuka ilikuwa katika Korle-Bu Teaching Hospital ya Chuo Kikuu cha Accra, na bado sijausahau mtaa wake – Guggisberg Avenue katika mji mkuu, Accra.

Ilikuwa ni muda mfupi baada ya mimi kujiunga hapo, nikiwa nimechelewa kidogo kuliko wenzangu maana bibi yangu aliugua sana nikaogopa kukosa baraka zake nikiondoka akiwa hospitalini. Ilikuwa mara yangu ya kwanza kuingia Afrika ya Magharibi niliyokuwa naiogopa bila sababu ya msingi.


Daktari huyo alikuwa anatusimamia pale. Wakati wa mapumziko tukila fufu (magimbi na viazi vilivyopondwa), alianzisha mjadala.


Aliuelekeza kwa mahakimu na majaji, akawashutumu kweli kama si kuwalaani, akasema wanahukumu watoto wa watu kwenda jela kwa sababu tu ya kukutwa na mihadarati kidogo. Akasema dawa hizo za kulevya ndizo zilikuwa zinasaidia baadhi ya familia kupata chakula na kuwapa nguvu ya kufikiri na kuchapa kazi.


Wezangu waliokwishamzoea walipompinga sana, akatoa kali na kuuliza lipi baya zaidi – kula bangi ukalima pande kubwa la ardhi au jaji anamaliza kazi anapiga mzinga wa wiski inaharibu viungo vyake vya ndani halafu anakufa wakati bado taifa lililomsomesha halijafaidi kichwa chake.


Kichwa bwana! Jamaa zangu walisema na kukubaliana na fikra yake kwa kweli. Leo Uingereza yangu naona inasogelea huko.


Wakati nipo chumbani nikichelea kutoka nje katikati ya wiki jana kwa wingi wa baridi iliyofikia hasi tano, nikasikia wabunge na tume ya mambo ya ndani wanataka mlegezo kwenye mihadarati.


Wakasema mtu akikamatwa na kiasi kidogo isiwe nongwa, aachiwe tu. Waziri Mkuu, David Cameron, alijibu kwa kifupi, akasema hakuna kitu kama hicho kitawezekana; lazima wanaobeba, kuuza, kununua, kusafirisha au kubwia mihadarati wafungwe au faini kali.


Ijumaa baridi ilipopungua na mvua kali na upepo kuchukua nafasi yake, Naibu Waziri Mkuu, Nick Clegg, akasema anaunga mkono sheria kupunguzwa makali, mambo ya mihadarati yasiwe ishu saana na kupoteza muda wa watu. Nikakumbuka yale yale ya Guggisberg Avenue na daktari wengine.


Tume imeshauri kupunguzwa kwa faini na vifungo kwa kiasi kidogo cha mihadarati baada ya kufanya kazi ya utafiti kwa miaka sita. Inasema isiwe tena jinai. Clegg anasema siku hizi watoto na vijana wanasema ni rahisi kupata mihadarati kuliko kupata na kunywa bia au kuvuta tumbaku.


Cameron alisema siku moja kwamba utafika wakati wavuta sigara watazitafuta madukani wazikose au sokoni washindwe kwa jinsi atakavyoweka udhibiti wa matumizi na bei.


Kama bia sasa inawekwa sheria na kanuni ya kiwango cha chini cha bei inayoruhusiwa ziuzwe ghali na kiwango cha juu cha mtu kutumia, ili wanywe kidogo, badala yake wachape kazi. Hapa ndipo na mimi nimeishia kutafakari bila jibu la moja kwa moja. Kama taifa, Uingereza inaogopa bia na sigara kuliko mihadarati?


Sigara zote zinazouzwa kihalali zina tangazo kuhusu madhara yake kwa afya, kuanzia kwenye meno, mfumo wa kupumua, moyo, na vifaa vingine vya mwili. Hivyo hivyo kwa bia na pombe kali, na hapa Uingereza maonyo yamebandikwa na jamaa wa ‘Drink Aware’ wanafuatilia sana.


Kwenye mihadarati kama bangi na mingine, ripoti ambayo wabunge wengi, baadhi ya mawaziri na hata naibu waziri mkuu wanaunga mkono, wanasema Uingereza inapoteza hadi paundi bilioni tatu kupambana na dawa za kulevya.


Kwa ujumla wao wanaona pesa hizo zitumike kwenye maendeleo, wa kula mihadarati iwe lake, afe lwake kwa kujitakia maana maonyo yameshatolewa.


Wanajenga hoja kwamba matumizi ya mihadarati na matatizo yake yamepungua sana Uingereza, hasa England na Wales wanaoguswa zaidi kisheria, japokuwa kuna vifo vya watu takriban 2,000 vinavyotokana na wabwia unga 380,000 ambao ni tatizo.

 

Watu karibu 42,000 wa England na Wales wanahukumiwa kila mwaka kwa kukutwa na dawa, na karibu 160,000 hupewa maonyo ya cannabis. Haya mambo, tume na wabunge wanasema yanapoteza muda na pesa nyingi kwa ajili ya polisi, waendesha mashitaka, mahakama na kupotezea pia washitakiwa muda wa kufanya mambo mengine.


Tumefikishwa hapo njia panda wadau, sigara na bia zinawekewa karantini, halafu mihadarati inataka kufunguliwa mlango. Watajua wenyewe, lakini na ndugu zetu wengi wako huku mjue.


leejoseph2@yahoo.com


955 Total Views 1 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!