Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu Huria cha Tanzania (OUT), Profesa Elifas Bisanda, amezungumza na Gazeti la JAMHURI kuhusu historia, mafanikio, changamoto na hatima ya chuo hicho. Mwandishi MANYERERE JACKTON, aliyezungumza naye, analeta maelezo ya Profesa Bisanda neno kwa neno. Endelea…

 

Uhaba wa fedha

Basically wanafunzi tunao, unaona operesheni yetu ni kubwa sana. Vituo 30 si kwamba tuna majengo – tunapanga, tunalipia umeme, tunalipia walinzi na idadi ya wanafunzi si kubwa sana kuweza kukidhi gharama zote. Hatupati ruzuku kutoka serikalini. Tunachokipata kutoka serikalini ni mishahara tu, hatuna OC. Kwa hiyo lazima nijue namna ya kulipia umeme (na huduma nyingine), hapa umeme ukikatika lazima niwashe jenereta, sina hela ya kununua magari. Mwaka jana (2017) nilinunua magari mawili (Land Cruiser 2), na mwaka huu nimenunua Ford Everest 2 za viongozi na tunakusudia mwaka ujao tununue magari mawili. Kila mwaka tumepanga kununua magari mawili.

Kwanini hawana OC?

Ni maagizo ya serikali. Vyuo vingine, kwa mfano vinapata hela za kujenga majengo. Tangu chuo kimeanza hela tuliyopata ni kutoka Benki ya Dunia, basi. Serikali haijawahi kutoa hela yoyote. Hatujapata pesa kutoka serikalini ya kujenga majengo, ukisikia tumejenga mikoani tumejenga kweli kwa fedha zetu.

OUT inafanya nini kuziba mapengo?

Tunapambana sana tuongeze idadi ya wanafunzi bila kuongeza ada. Hatutaki kuongeza ada. Tunataka elimu yetu iwe affordable (inayohimilika). Tumekuwa tunatoza ada hiyo hiyo tangu mwaka 2012. Haijaongezeka mpaka leo (2018). Digrii ni kama Sh milioni 2.7 hivi ukiweka pamoja na gharama za mitihani. Kwenye diploma iko kama Sh milioni 1.2, inaweza ikazidi kidogo kulingana na masomo. Masters (Uzamili) iko kwenye Sh milioni 3.5. Phd (Uzamivu) iko kwenye Sh milioni 6. Hii ada si kwa mwaka, ni ada kwa programu yote – kuanzia mwanzo mpaka mwisho. Sisi tunaamini kwamba elimu ni kama mtu anavyopakua chakula hotelini. Ukienda hotelini kula chakula haulipii kwa muda uliokaa restaurant. Unalipia kwa kile ulichokula. Ukikaa nusu saa umelipia chai, utalipa hela ile ile, ukikaa dakika 10 ni hela ile ile, kwa hiyo tunaamini ukija kwetu ukasoma digrii hatuangalii muda uliokaa, lakini umepokea digrii.

Tunamruhusu mtu kusoma digrii kuanzia miaka mitatu hadi minane, ni free – utaamua wewe mwenyewe utamaliza kwa kasi ipi, lakini ada utakayolipa ni ile ile. Ukisoma miaka mitatu, miaka minane ada ni ile ile.

Mbinu ya pili kwa ajili ya kuongeza mapato ya chuo, tunajaribu kuhamasisha wana taaluma wetu waingie kwenye kazi za ushauri ingawa kwa kweli fursa za research ni ndogo sana na tuna ushindani mkubwa na ma-consultant ambao wako mitaani ambao wao wanaziona fursa mapema kabla yetu. Kwa hiyo hatupati hela nyingi sana kutoka kwenye njia hiyo ya consultancy au kwa ajili ya research. Tumeandika bits nyingi za kuomba hela za utafiti, lakini hata mara nyingi zikiingia chuo kinapata asilimia 15. Kwa hiyo mtu akifanya consultancy akapata Sh milioni 100, chuo kitapata Sh milioni 15 – nyingine zote atachukua yeye consultancy na wenzake. Kwa hiyo si chanzo kikubwa cha mapato.

Lakini pili, tumejaribu kuongeza programu za kozi za Uzamili. Kwa kweli ndizo zimetushikilia mpaka sasa. Watu wengi wakishakuwa kazini ni rahisi zaidi kusoma Masters – Open University kuliko kwenye vyuo vingine, kwa sababu hawaachi kazi zao. Tunawawezesha kusoma Masters wakiwa wako kazini. Kwa hiyo kwa kweli hizo programu ndizo zimekishikilia chuo kwa sasa hivi.

Programu za undergraduate zina tatizo. Tatizo la kwanza, wengi wanaotaka kusoma ni watu waliomaliza form VI, lakini wakitaka kusoma hakuna bweni. Wale vijana wanataka wakae bwenini wawe free from their parents.

Pili, hakuna mkopo. Mkopo kwa kweli kwa miaka miwili sasa wanapata mikopo. Wanafunzi mmoja au wawili ambao ni walemavu ndio wanapata mkopo. Sera ya kutoa mkopo mwanzoni ilikuwa inatafsiriwa kama Open University Part Time Study, kwa hiyo walikuwa hawapewi mkopo. Sasa hivi ndiyo tumejaribu kuzungumza na Mkuu wa Bodi ya Mikopo, amekubali kuwa kama wapo wanafunzi watakaoweza kupewa mkopo wapewe. Mkopo tunaoomba sisi ni hela kidogo sana. Ni hela kwa ajili ya tuition na vitabu. Hatulipii bweni wala chakula. Mtu anayechukua mkopo kwenda kusoma University of Dar es Salaam anataka alipiwe ada, bweni na hela ya kula ambayo ni gharama kubwa kuliko kusomesha. Ada ya tuition ni kama Sh 800,000 kwa mwaka. Zile Sh milioni 2.7 ukizigawa kwa tatu ni kama Sh 900,000 kwa mwaka kama atasoma kwa miaka mitatu, na wengi sana wanasoma kwa miaka mitatu. Wengi wanaohitimu sasa wanasoma kwa miaka mitatu. Hata watu wazima wamekuwa challenged, wakitoka kazini utaona wanakuja hapa library ili nao wamalize ndani ya miaka mitatu pamoja na wahitimu wa kidato cha sita ambao wengine hawana kazi. Kwa hiyo wanashinda hapa (chuoni). Hata ukienda sasa hivi utawakuta. Vyuo vingine kwa sasa vimefunga, lakini huku Open University hakufungwi – huwa hatufungi. Ukimaliza kozi ya mwaka huu unaanza kozi ya mwaka unaofuata.

Pia mitihani yetu tunaitoa wakati wowote. Mwanafunzi akitaka mtihani anapewa, si lazima usubiri kile kipindi cha mitihani. Ukisema ‘mimi niko tayari kufanya mtihani’ tunakupa mtihani. Kwa hiyo unaweza mwenyewe kuamua umalize kwa muda gani, lakini lazima uwe ndani ya ule muda wa TCU ambao ni miaka mitatu kwa digrii.

Kwenye Masters, minimum ni mwaka mmoja, lakini maximum ni miaka minne. Kwenye research watu wengi wanachelewa kwa hiyo tunaweka miaka minne kumaliza Masters.

Ukodishaji majengo

Sisi kama chuo tumefanya ushirikiano na mikoa. Karibu mikoa yote kuna kitu kinaitwa Regional Advisory Committee (Kamati ya Ushauri ya Mkoa) ya Open University ambayo mwenyekiti wake ni mkuu wa mkoa. Mkuu wa mkoa anakaa katika kamati yake, moja ya kazi zake ni kuainisha kama ndani ya mkoa wake kuna majengo ambayo ni ya serikali, ambayo sisi tunaweza kupewa tukayatumia kwa muda mrefu au mfupi.

Wakiyaainisha majengo sisi tunatafuta hela za kuyakarabati tunaweka ofisi. Hiyo tumefanya Mwanza. Mkuu wa mkoa alitupatia majengo na sasa wanataka kutumilikisha. Tuliyakarabati kwa shilingi zaidi ya milioni 100. Sasa ndiyo tunayatumia kwa Kituo cha Mwanza. Kabla ya hapo tulikuwa tunapanga jengo la PPF. Tulikuwa tunalipa Sh milioni 200 kwa mwaka. Tukaona hatuwezi kumudu.

Sehemu nyingine ya mfano ni Dodoma ambako tulipewa majengo, yalikuwa Wilaya ya Bahi, tukayafanyia ukarabati. Singida tulipewa majego yalikuwa ya Makumbusho ya Taifa. Tukamilikishwa lile eneo tukakarabati. Tunaendelea nayo. Mkoa wa Njombe bado tunatumia jengo la dharura chini ya Ofisi ya Wilaya ya Njombe kabla ya kuwa mkoa. Tunalitumia, lakini wametupa na eneo ili tujenge. Tanga tuna ubia na TUCTA wa miaka 20. Tukalikarabati tunaendelea kulitumia. Musoma kuna jengo lilikuwa la Kituo cha Utamaduni wakatupatia, tukalikarabati sasa tunatafuta umiliki wake. Kwa sasa tunaendelea kushirikiana matumizi yake na mkoa (Mara).

Sehemu nyingine ambayo ni interesting ni Iringa. Tulinunua majengo yaliyokuwa ya Relwe, tulinunua kwa hela zetu. Mbeya tulinunua jengo lilikuwa la CRDB. Tulinunua kwa mkopo kutoka TEA. Tumeshalilipia. Rukwa tulinunua majengo yalikuwa ya RETCO. Mpanda (Katavi) walitupatia majengo ya halmashauri, tukayafanyia ukarabati majengo matatu na ndiyo tunaendelea kuyatumia. Mtwara tulinunua baa, tukaigeuza kuwa kituo – ule ukumbi waliokuwa wanautumia (wanywaji) tukautengeneza vizuri ukawa wa kufanyia mitihani –tukajenga ofisi na maabara. Ni karibu na Hospitali ya Mtwara, kwa hiyo tumepunguza kelele za disko kwa wagonjwa. Songea tulipewa godown, tukalikarabati, kwa hiyo nalo tunalimiliki.

Kibaha (Mkoa wa Pwani) tulikuwa tumekusudia kujenga makao makuu. Tuna eneo la ekari 105 ambalo tulifikiri tunaweza kujenga Makao Makuu ya Open University. Lakini tukawa tunaomba hela kila mwaka. Tangu nimekuja mimi mwaka 2007 kila mwaka tunaomba hela, haikuwahi kutoka hata senti tano. Kwa juhudi zetu wenyewe tukajenga majengo mawili – stoo na ofisi. Lakini baada ya kuona hatupati pesa na msukumo umekuwa ni kwenda Dodoma, tukapata mawazo kwamba hata sisi inabidi kwenda Dodoma kwa sababu ni chuo kikuu cha kitaifa, na kuendesha shughuli zetu kutokea Dodoma ni nafuu zaidi kuliko kutokea Kibaha. Kama mimi ninataka kusafiri kwenda Kagera kutokea Dodoma, siku hiyo hiyo ninafika. Tuna mpango sasa wa kujenga makao makuu Dodoma. Yale majengo tuliyokuwa tumeshajenga tumekabidhi Kituo cha Mkoa wa Pwani. Kituo cha Pwani kilikuwa pale kwenye Taasisi ya Elimu Kibaha, sasa kimehamia kwenye majengo yetu kule Kwa Mathias.

By Jamhuri